Home Habari za michezo KUHUSU UKAME WA MAGOLI KWA KIBU….UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA….

KUHUSU UKAME WA MAGOLI KWA KIBU….UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA….

Habari za Simba

Kibu Denis, Kibu Denga, Kibu Mkandaji. Yote ni majina maarufu ya staa huyu wa Simba ambaye mambo yake pale Msimbazi yanaonekana kubadilika, huku mkataba wake ukiisha mwisho wa msimu huu.

Nyota huyu aliyejiunga na Simba Oktoba 3, 2021 akitokea timu ya Mbeya City, alianza maisha kwa kishindo katika msimu wa kwanza alipofunga mabao manane na kumaliza akiwa mfungaji bora wa Simba katika msimu huo wa 2021-22 ambao ubingwa wa Ligi Kuu ulienda kwa mahasimu wao Yanga.

Msimu uliofuata wa 2022-23, yaani msimu uliopita, Kibu hakuanza vyema akikosolewa na mashabiki wa soka wakiwamo wa timu yake ya Simba.

Wengi walionekana wakitaka atemwe na waliamini angetemwa baada ya msimu huo ambao Yanga ilianza kwa kishindo kutetea taji lake huku ikiweka kila ya aina ya rekodi ikiwamo ya kucheza mechi 49 bila ya kupoteza mchezo.

Na kati ya mambo ambayo wanaSimba hawakupendezwa nayo ilikuwa ni kupoteza mechi zote za misimu miwili mfululizo za Ngao ya Jamii (1-0 na 2-1) dhidi ya Yanga ambayo wakati huo safu yake ya ushambuliaji ilikuwa ikiongozwa na Fiston Mayele.

Mashabiki walikuwa wakionyesha kutofurahishwa na matokeo hayo na mwenendo wa timu yao ambayo walizoea kuiona ikitawala soka la Bongo kwa miaka minne mfululizo ilipotwaa ubingwa wa Bara kuanzia msimu wa 2017-18, 2018-19, 2019-20 hadi 2020-2021.

Mashabiki na hata wachambuzi katika vyombo mbalimbali vya habari walionekana kutoridhishwa kiwango cha Kibu kutokana na kutofunga kama msimu uliotangulia na kuonekana kuwa ni sehemu ya matatizo ya Simba ya kuwa wanyonge mbele ya wapinzani wao wa Kariakoo, Yanga.

Lakini katikati ya lawama, kukosolewa na kutoaminiwa, Kibu Dennis aliibuka shujaa wa Kariakoo Derby pale alipofunga bao tamu, la shuti kali la kutokea nje ya boksi lililomshinda kipa ‘mdaka mishale’ wa Yanga, Djigui Diarra, ambaye aliishika kudaka hewa katika mechi iliyopigwa kwenye uwanja uliojaa mvua wa Benjamin Mkapa Aprili 16, 2023.

Bao jingine katika mechi hiyo lilifungwa na beki wa kati, Henock Inonga akimalizia kwa kichwa krosi ya Shomary Kapombe ‘Baba Esther’ aliyepokea kona fupi ya Saido Ntibazonkiza.

Stori ya mwaka ikawa ni ushindi wa Simba, ambayo ilikuwa haijaifunga Yanga kwenye ligi kwa zaidi ya miaka minne, tangu Februari 2019.

Ndio sababu ushindi huo ulikuwa na maana kubwa kwa timu Wekundu wa Msimbazi na ‘m-goli’ ule wa Kibu ambaye alikandamiza mshuti kama anaua nyoka, ukawapa mashabiki cha kuvimbia mjini. Na akapewa jina la Mkandaji.

Udhaifu wa Kibu wa kutofunga mabao ya kutosha ukawekwa kando na sasa mashabiki wakapata nafasi ya kumuangalia mshambuliaji huyo mchango wake mwingine kwenye timu kando ya mabao.

Na kila mmoja akakubali kwamba Kibu mbali ya kuwa ni mkandaji, lakini pia ni mpambanaji. Na hiyo ilimfanya hata kuitwa mfululizo kwenye timu ya taifa, Taifa Stars.

Lakini hiyo haikuondoa ukweli kwamba hadi msimu uliopita ulipomalizika, Kibu alikuwa amefunga mabao mawili tu ya Ligi Kuu Bara. Alizidiwa na hata baadhi ya mabeki.

Kiujumla takwimu hizo za ufungaji haziridhishi kwa mchezaji anayecheza nafasi ya ushambuliaji.

Unaweza kusema kwamba uwapo wa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ Msimbazi ulikuwa ni neema kubwa kwa Kibu. Mbrazili huyo alimuamini na Kibu akazidisha kupambana kuisaidia timu kwa upande mwingine.

Katika mechi iliyopita ya Kariakoo Derby, Kibu alifunga bao la kichwa na kuisawazishia Simba baada ya Kennedy Musonda kuitanguliza Yanga kwa bao la kichwa pia. Kibu akashangilia kwa kuwaziba mdomo wanaomkosoa ama Yanga.

Lakini haikuwa siku njema kwa Simba kwani ililala 5-1 na kuamsha upya hasira za mashabiki wa Msimbazi wakikosoa mengi katika kikosi chao, lakini Kibu hakujumuishwa kwa sababu bao lake ndilo lilikuwa kitu pekee cha Simba kujivunia katika kipigo hicho cha kihistoria.

Kocha Robertinho akafutwa kazi kutokana na kipigo hicho na Simba ikamtangaza Mualgeria Abdelhak Benchikha, ambaye amekuja na falsafa zake ambazo wengine wanaona zinafanya umuhimu wa Kibu kupungua kikosini.

Katika mechi za siku za hivi karibuni, Kibu hata akianzia benchini hakuna anayeshangaa na hata akiwa uwanjani haonekani kuuwasha kama alivyokuwa chini ya Robertinho.

Kuna mabadiliko makubwa kati ya Kibu wa Robertinho na Kibu wa Benchikha. Kitu ambacho hamna mabadiliko kwa Kibu ni kwamba hadi sasa amefunga mabao mawili tu kwenye Ligi Kuu Bara, sawa na msimu uliopita.

Wakati mkataba wake umebakiza miezi mitatu kumalizika Juni 30, mashabiki wanatamani kuona juhudi zake za upambanaji zikifanana na idadi ya mabao anayofunga.

Robertinho akiwa Msimbazi aliwahi kukaririwa akisema Kibu ndiye mchezaji wake bora kutokana na kumpa kile anachokihitaji uwanjani, ikiwamo kusaidia kukaba na kuwanyima nafasi wapinzani kutokana na kuwa na kasi na kujituma.

SOMA NA HII  SHOW ZA NGOMA ZAMFANYA BENCHIKHA KUIBUKA NA HILI...AWAPA MAAGIZO MABOSI SIMBA..