Home Habari za michezo KANOUTE AJIPATA UPYA SIMBA….BENCHIKHA AMPA JUKUMU LA ‘FEI TOTO’ YULE WA YANGA…

KANOUTE AJIPATA UPYA SIMBA….BENCHIKHA AMPA JUKUMU LA ‘FEI TOTO’ YULE WA YANGA…

Habari za Simba

Wakati anatua Simba miwili iliyopita kuchukua nafasi ya Taddeo Lwanga, kuna watu walimchukulia poa, lakini kadri alivyoanza kucheza watu walimuelewa sana.

Alionekana ni kiungo mgumu ambaye hana mambo mengi, lakini anazuia na kuwagonga sana wapinzani uwanjani ili kuwanyima uhuru wa kuisumbua ngome ya Simba.

Ndio maana haikushangaza kuona ni nadra sana kumaliza mechi bila kupewa kadi nyekundu. Uimara na uhodari wake uwanjani, uliifanya Simba itulie eneo la kiungo cha ukabaji.

Hapa tunamzungumzia Sadio Kanoute, kiungo mkabaji kutoka Mali. Aliyewafanya wanasimba kuwa na utulivu kila walipomuona uwanjani kwani aliifanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.

Umahiri wa Kanoute ulimfanya Simba kumkaushia Jonas Mkude aliyekuwa mfalme wa muda mrefu kwenye eneo hilo ndani ya Simba. Alimpa wakati mgumu Mzamiru Yassin, kwani alikuwa ni panga pangua katika kikosi cha kwanza cha Simba.

Hata hivyo sasa unaambiwa baada ya ujio wa Fabrice Ngoma na kuimarika kwa Mkongoman huyo kwenye eneo hilo sambamba kuanza kulizoea soka la Tanzania kwa kiungo Msenegali Babacar Sarr kumemfanya kocha wa Simba Abdelhak Benchikha kutafuta kilicho bora zaidi kwa kumbdilishia Kanoute majukumu kikosini.

Ndio. Utabisha nini wakati, kwa sasa Kanoute amekuwa akichezeshwa kama kiungo mshambuliaji na sio mkabaji tena? Umeliona hilo? Tangu kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao Simba ilicheza na JKT Tanzania hadi ule wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas kule Ivory Coast pamoja na uliopita juzi kati kwenye ASFC, Kanoute hatumiki tena kama kiungo mkabaji badala yake amesogezwa mbele na huko amekuwa mtamu kinoma!

Katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania na hata ASEC Mimosas, Kanoute alionyesha kuwa na uwezo wa kutekeleza vyema kile ambacho Benchikha alikuwa akihitaji licha ya kuonekana kushindwa kutumia nafasi aliifanya timu kuwa na nguvu ya kuutafuta mpira kuanzia juu ambako amekuwa akishirikiana vizuri na wapishi wa kikosi hicho, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

Kutaka kuonyesha kwamba eneo hilo ndilo linalomfaaa, juzi kwenye mechi ya TRA katika mechi ya ASFC alifunga hat trick, mbali na mabao aliyofunga dhidi ya Al Ahly zilipochuana michuano mipya ya African Football League (AFL).

STAILI YAKE

Kasi, uwezo wa kukaba na usahihi wake wa maamuzi ni miongoni mwa vitu ambavyo inawezekana Benchikha ameviona kwa kiungo huyo kiasi cha kuamua kumbadilishia majukumu hata hivyo kitendo cha kumtumia zaidi eneo la kukaba pengine Simba isingenufaika naye kwenye eneo la ushambuliaji.

Benchikha anatukumbusha Nasreddine Nabi ambaye alimtoa Feisal Salum ‘Fei Toto’ kutoka nafasi ya ukabaji hadi kumtumia kama namba 10 na hapo ndipo tulipoanza kuona moto wa fundi huyo wa Kizanzibar aliamua mechi nyingi za Yanga na hadi sasa amekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha Azam FC.

Makocha wa kisasa wamekuwa na tabia za kuwasoma wachezaji kulingana na sifa zao kwenye uwanja wa mazoezi na kuwabadilisha kiuchezaji ili kupata kilichobora, mfano mwingine ni kwa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kuna mechi amekuwa akimtumia beki wake wa kushoto Oleksandr Zinchenko kwenye eneo la kiungo, Pep Guardiola akiwa Bayern Munich alimbadili Joshua Kimmich kutoka beki wa kulia hadi nafasi ya kiungo ambayo anaendelea kutamba nayo.

Inawezekana tukaona mengi kutoka kwa Kanoute hasa katika upachikaji mabao maana mbali na kasi aliyonayo, uwezo wa kufanya maamuzi kwa haraka lakini pia ni mrefu hivyo anaongeza namba ya wachezaji wenye vimo virefu kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo bado haijakaa sawa licha ya kusajiliwa kwa Freddy Michael ‘Fungafunga’ na Pa Omar Jobe.

BENCHIKHA MJANJA

Baada ya kuisuka Simba kuwa na ukuta imara, Benchikha amejaribu kutafuta namna ambayo inaweza kuifanya timu kufunga mabao ya kutosha huku akiwapa muda washambuliaji wake wapya, Freddy Michael na Pa Omar Jobe kuonyesha makali yao.

Pamoja na kwamba washambuliaji hao tayari wameanza kucheka na nyavu bado hawajaonyesha kile ambacho kocha huyo alikuwa akitegemea kutoka kwao hivyo Kanoute anaonekana kuwa anaweza kuwa msaada na ameanza kuthibitisha hilo.

Miongoni mwa vitu ambavyo Benchikha alikwazika wakati akiwa kwenye benchi lake la ufundi kwenye mchezo wa ligi dhidi ya JKT Tanzania ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Chama ni pamoja na Freddy kushindwa kukaa na mpira mara nyingi hilo limekuwa pia likijitokeza hata kwa Jobe. Hilo limekuwa likimfanya kocha huyo raia wa Algeria kuwa mkali.

KWANINI HIVI

Hakuna kingine ambacho Benchikha anataka kwenye kikosi chake zaidi ya uwajibikaji na sio tatizo kumsugulisha benchi mchezaji ikiwa atashindwa kufanya kile ambacho anapaswa kufanya.

Kama ulikuwa hujui, Benchikha ni kocha mwenye misimamo na mkali, unaambiwa anawanyoosha kwelikweli mastaa wa timu hiyo ili kuhakikisha timu inakuwa kwenye mstari kila mchezaji ananafasi sawa na mwingine kwenye kikosi chake.

MWENYEWE AFUNGUKA

Akizungumza Kanoute amesema anapambania timu ili ipate ushindi.

“Naweza kucheza eneo lolote ambalo mwalimu anahitaji kunitumia, kazi yangu ni kuhakikisha nakuwa msaada kwenye timu,” anasema Kanoute aliyezaliwa Oktoba 21, 1996 katika mji wa Bamako, Mali na kuanza kucheza soka la ushindani kupitia klabu ya Stade Malien ya Mali kabla ya kusajiliwa Al Ahli Benghazi ya Libya.

Simba ilivutiwa naye na kumpa mkataba wa miaka miwili Agosti 20, 2021 kisha kumuongezea mwingine utakaomalizika Juni 20, 2024 kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market.

Tangu atue Simba ameifungua jumla ya mabao matatu katika Ligi Kuu Bara, yakiwamo mawili ya msimu huu na moja la msimu wa kwanza kuichezea timu hiyo, mbali na yale ya kwenye michuano ya CAF.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUSEPA YANGA...MUKOKO ASHINDWA KUJIZUIA..AANIKA YA MOYONI ...AWATAJA VIONGOZI...