WAKATI Simba ikiianza wiki ya Dabi ya Kariakoo kinyonge baada ya sare ya 1-1 na Ihefu katika mechi ya jana, watani wao Yanga wameongeza mzuka baada ya jana kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 42 kupitia kwa mshambuliaji Joseph Guede aliyeuchekecha ukuta wa Singida baada ya kupokea pasi ndefu kutoka kwa Joyce Lomalisa na kupiga shuti lililombabatiza beki Laurian Makame kuzama moja kwa moja nyavuni ukimpoteza maboya kipa Benedict Haule.
Singida ilikianza kipindi cha kwanza nidhamu na kuibana Yanga, lakini ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza na kujikuta ikienda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote na dakika ya 66, Aziz Ki aliiandikia Yanga bao la pili kwa kombora kali nje ya eneo la 18 na kukaa wavuni likimuacha kipa, Benedict Haule aliruka bila mafanikio. Bao hilo lililotokana na pasi tamu ya Clement Mzize, likiwa ni la 14 kwa Aziz Ki msimu huu katika Ligi Kuu akimuacha Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao 13 ambaye usiku huu anajiandaa kushuka uwanjani kukabiliana na Namungo.
Dakika tatu baadae Guede aliiandikia Yanga bao la tatu dakika ya 67 kwa kichwa akiunganisha vyema pasi ya Mzize, bao hilo lilikuwa ni la pili kwa mshambuliaji huyo katika mchezo huo na kwenye Ligi Kuu lakini akifikisha jumla ya mabao matano yakiwamo mawili ya Kombe la Shirikisho na Moja la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ushindi huo ambao ni wa pili kwa Yanga mbele ya Singida baada ya kuichapa mabao 2-0 mzunguko wa kwanza, unaendelea kuiweka Yanga kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikijichimbia kwa kufikisha pointi 55 na kuzidi kutanua wigo wa alama na watani wao, Simba ambao wanachechemea katika nafasi ya tatu na pointi zao 46 huku Azam FC ikiwa katika nafasi ya pili na alama 47 na itashuka uwanjani saa moja lijalo ikiwa ugenini mjini Lindi dhidi ya Namungo.
Yanga iliutumia mchezo huo kurudisha heshima kwenye ligi kwani mara ya mwisho iliopoteza mchezo wa Ligi kwa kufumuliwa mabao 2-1 na Azam FC Machi 17, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo unaifanya Yanga iingie katika maandalizi ya Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Aprili 20, mwaka huu kuanzia saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikiwa na nguvu, morali na shangwe, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Simba mabao 5-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Matokeo hayo yanaicha Singida Fountain Gate katika nafasi ya nane na pointi zao 24, ukiwa ni mwendelezo wa matokeo mabovu kwa timu hiyo kwani katika mechi 11 zilizopita za Ligi Kuu imeshinda mara moja tu, sare tatu na kupoteza sita, ikiwa imefunga mabao sita na kufungwa 16.
Singida imeshindwa kujitutumua angalau ifute machozi ya unyonge mbele ya Yanga kwani haijawahi kupata ushindi au sare inapokutana na Yanga tangu ilipopanda Ligi Kuu, huku mechi zao nne zilizopita Yanga ikishinda zote.
MCHEZO ULIVYOKUWA
Kipindi cha kwanza hakikuwa na burudani iliyotegemewa kutoka kwa mashabiki kutokana na hali ya uwanja kutokuwa rafiki baada ya mvua kubwa iliyonyesha jijini Mwanza dakika chache kabla ya mchezo huo kuanza.
Ambapo wachezaji wa timu hizo walishuhudiwa wakiteleza na kuanguka ama kushindwa kutuliza mpira na kupiga krosi na kupelekea mipira mingi ya muhimu kupoteza ama kuharibu mashambulizi.
Licha ya changamoto hiyo, lakini bado Yanga ilionekana inautaka mchezo huo na kusaka mabao kwa kila namna na kufnikiwa kutengeneza mashambulizi langoni mwa Singida ikiwemo nafasi ya wazi dakika ya pili ambayo Clement Mzize alipiga shuti lililotoka nje baada ya kumegewa pasi safi na Azizi Ki.
Kipindi cha pili, Yanga iliongeza kasi katika mashambulizi langoni mwa Singida Fountain Gate na kujaribu mashuti ya mbali, ambayo yalilipa dakika ya 65 na 67 ikipata mabao mawili kupitia kwa Aziz Ki na Joseph Guede.
Timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji, Singida Fountain Gate imewapumzisha Dickson Ambundo, Iddi Khalid na Atta Agyei dakika ya 73 na 74 nafasi zao zikichukuliwa na Deus Kaseke, Frank Zacharia na Francy Kazadi.
Yanga iliwapumzisha Maxi Nzengeli, Khalid Aucho, Joseph Guede na Gift Fredy dakika ya 72 na 80 na kuwainhiza Mudathir Yahya, Makudubela, Farid Mussa na Kibwana Shomari.
AUCHO AIVA, BADO PACOME, YAO
Katika mchezo huo, kiungo wa Yanga, Khalid Aucho ambaye alikosekana kwa takribani mwezi mmoja akiuguza majeraha, alicheza kwa dakika 72 na kuisaidia timu yake kuondoka na cleensheet ambayo ni ya nane msimu huu kwa kipa, Djigui Diarra.
Ni mchezo wa pili kwa kiungo huyo kucheza mfululizo tangu atokeo majeruhi, ambapo mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Dodoma Jiji alicheza kwa takribani dakika 25, jambo ambalo linaonyesha ameiva na sasa yuko fiti kutumika kwa mchezo ujao wa Dabi ya Kariakoo bila wasiwasi wowote kwani amekuwa nguzo muhimu katika kuilinda safu ya ulinzi.
Wasiwasi sasa unabaki kwa nyota wawili, kiungo mshambuliaji, Pacome Zouzoua na beki wa kulia, Kouassi Yao ambaye katika mchezo wa juzi alikuwa jukwaani na hata siku moja kabla ya mchezo alifanya mazoezi ya maandalizi ya mchezo huo na wachezaji wenzake.
Vikosi vilivyoanza:
Yanga: Djigui Diarra, Gift Fredy, Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Jonas Mkude, Joseph Guede, Aziz Ki na Clement Mzize
Singida Fountain Gate: Benedict Haule, Nicolas Wadada, Amos Kadikilo, Laurian Makame, Carno Biemes, Aziz Andambwile, Enock Agyei, Iddi Habib, Habib Kyombo, Nicolas Gyan na Dickson Ambundo