Home Habari za michezo KUELEKEA YANGA vs SIMBA KESHO….HAYA HAPA UNAYOPASWA KUJUA KABLA YA MECHI…

KUELEKEA YANGA vs SIMBA KESHO….HAYA HAPA UNAYOPASWA KUJUA KABLA YA MECHI…

Habari za Michezo leo

ILE Siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa sasa imewadi yamesalia masaa chache mchezo wa Kariakoo Derby uchezwe huku Yanga wakiwa wenyeji, uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, kesho saa 11:00 jioni.

Katika mchezo wa kesho Yanga watakuwa wenyeji wa mchezo huo baada ya Simba kuwa mwenyeji katika mchezo wa mzunguko wa kwanza na kukubali kichapo cha mabao 5-1, ambayo yalifungwa na Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Maxi Nzengeli aliyefunga mawili huku bao la Simba likifungwa na Kibu Denis.

Kwa mwezi Aprili kuanzia mwaka 2010, rekodi zinaonyesha timu hizo zimekutana mara nne kwa mwezi huo Simba walifanikiwa kushinda mara mbili na sare mbili huku Yanga hawakufanikiwa kumfunga mpinzani wake.

Aprili 18, 2010, Simba alifanikiwa kushinda mabao 4 -3 , yalifungwa na Uhuru Suleiman dakika 3, Mussa Mgosi dakika 53 na 74, Hillary Echesa dakika 90+ kwa upande wa Yanga alifunga Athumani Iddi dakika 30, Jerry Tegete dakika 69 na 89 .

Kesho wanakutana mara tano na nani ambaye ataweza kufanya vizuri, Simba kuendeleza ubabe wake au Yanga kuvunja mwiko wa mwezi wa Aprili kwa kuendeleza kuchapo kwa mara ya pili kwa msimu huu wa ligi hiyo.

Mchezo wa kwanza ulichezwa Aprili 19, 2014 , uliisha sare ya bao 1-1, Simba walitangulia kuoata bao likifungwa na Haruna Chanongo , dakika ya 75 na 86 Yanga walisawazisha bao kupitia Simon Msuva, nyota ambao hawapo tena katika vikosi vya timu hizo.

Msimu wa 2017/18 , Aprili 20, Simba alifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, limefungwa na Erasto Nyoni dakika ya 37, mchezo mwingine uliwakutanisha wakongwe hao wa ligi ni kumalizika kwa suluhu.

Kipindi hicho kocha wa Yanga, akiwa Cedric Kaze na Simba kipindi hicho kikinolewa na Pablo Franco ambao makocha wote hawapo tena katika mabenchi ya hizo timu.

Mchezo wa mwisho uliochezwa Aprili, 16, 2023 , Simba ilishinda 2-0, mabao yamefungwa kupitia beki Henock Inonga dakika ya kwanza kwa kichwa na Kibu Denis akifunga bao la pili dakika 32 , wachezaji wote bado wapo na kuitumikia Simba kwa sasa.

Mechi ya ya kesho haitakuwa ya kinyonge kutokana na rekodi za timu hizo hivi karibuni, mechi tano za mwisho walizokutana Simba ilishinda mbili na Yanga moja na sare mbili.

Michezo hiyo ni Aprili 19, 2014 Yanga wakiwa nyumbani walitoka sare ya bao 1-1 Simba na 19, 2018 Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Yanga.

Aprili 30, 2022 Yanga wakiwa nyumbani walisuluhu na 2023, 16, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0. Hivyo Katika mchezo wa kesho ni aidha Simba ataendeleza ubabe wao kupata matokeo mazuri au Yanga kuharibu rekodi hiyo kwa mwezi wa nne.

Yanga inashuka dimbani ikiwa na safu ya  ushambuliaji imara inayoongozwa na kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki ambaye hadi sasa ametikisa nyavu mara 14 na Nzengeli amefunga tisa (9)wakati Simba, Clatous Chama amefunga mabao 7 sawa Saido Ntibazonkiza.

Yanga na Simba, zote zipo katika mbio za ubingwa, Yanga wakiongoza msimamo kwa alama 55, Simba wakiwa nafasi ya tatu na alama 46 na Azam FC wakiwa nafasi ya pili kwa alama 51 katika msimami wa ligi hiyo.

Katika mchezo wa kesho  Waaamuzi ni Ahmed Arajiga (Manyara), akisaidiwa na Mohammed Mkono (Tanga), Kassim Mpanga (Dar es Salaam) na Tatu Malogo (Tanga).

Kuelekea mchezo huo Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema mechi ya dabi ni moja ya mechi kubwa sana Afrika Mashariki na kesho itakuwa ni sehemu ya mchezo mkubwa kwa Afrika.

Amesema wamejiandaa vizuri kama kawaida kwa mchezo huo, wachezaji wana morali nzuri na wapo tayari kukabiliana na mpinzani wake Simba katika mchezo wa kesho.

“kesho ni mechi nyingine na mipango yake ni mingine huu mchezo tofauti na ule uliopita na tunacheza kwa tahadhari kubwa kuhakikisha tunafanikiwa kupata matokeo chanya,” amesema Gamondi.

Ameongeza kuwa kuelekea mechi ya kesho kuna baadhi ya wachezaji atawakosa kulingana na majeraha na sababu mbalimbali lakini anaimani walikuwepo wanaweza kufanya vizuri kama ilivyo kwa mechi zilizopita.

Mwakilishi wa wachezaji wa Yanga, Dickson Job, amesema wamejiandaa vizuri na wako tayari kupambana kwa ajili ya kutafuta matokeo chanya mbele ya mpinzani wao.

“Simba ni timu mzuri na hautakuwa mchezo rahisi, mchezo utakuwa mgumu kikubwa tunahitaji pointi tatu, hatuchezi kwa presha kubwa wala matokeo ya kutaka kushinda mabao mengi kikubwa ni alama muhimu,” amesema Job na kuongeza kuwa wanahitaji kuenzi vizuri mchezo huo na kufikia malengo yao.

Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema maandalizi yaneenda vizuri siku zote hakuna mechi rahisi ya Derby, wanawaheshimu wapinzani wao Yanga na wamejiandaa kukabiliana nao katika mchezo wa kesho.

Amesema hii mechi ni mpya na tofauti na iliyopita , wachezaji wamecheza hizi mechi mara nyingi zaidi haikuwa kazi ngumu kufanya maandalizi ikiwemo kuzungumza nao juu ya mchezo huo.

“Hatuna presha kabisa , mechi ya Derby ni tofauti kabisa na michezo mingine tumefanya maandalizi mazuri kukabiliana na Yanga, Kocha Abdelhak (Benchikha), anaumia sana pale tunapotengeneza nafasi na haziwi mabao, tumeliangalia na kufanyia kazi nafasi zinazopatikana ziwe mabao,

Mbio za ubingwa zipo wazi katika mchezo wa kesho ndio unatoa taswira ya nani kubwa bingwa, tukihutaji ubingwa lazima tushinde mechi ya kesho dhidi ya Yanga,” amesema Matola.

Nahodha Msaidizi wa Simba, Shomari Kapombe amesema maandalizi yameenda vizuri wachezaji wana morali ya mchezo wa  na  benchi la ufundi limepata muda mzuri wa kuandaa timu yake.

Amesema wapo tayari kwa kufuata maelekezo waliyopewa na kila mmoja kufanya jukumu lake kwa ajili ya kutafuta pointi tatu muhimu katika mchezo wa huo.

“Moja tunaenda kufuata maelekezo tuliyoelekezwa na pili kupambania kile ambacho mashabiki wetu wanakitarajia ikiwemo kuvuna pointi tatu dhidi ya Yanga, tumefanyia kazi safu ya ulinzi na kupunguza makosa na kesho tunashuka dimbani kivingine.

Kwa sasa hatufikirii mechi iliyopita, tumefungua ukurasa mpya na hii mechi ni aina nyingine na tumekuwa na mikakati mipya kuhakikisha tunavuna point tatu,” amesema Kapombe.

Aliongeza kuwa mechi ya kesho ndio itakuwa hatma ya malengo yao ya kuendelea kusaka tiketi yao ya kutwaa taji la ubingwa wa ligi kuu anaimani hadi sasa bado hajajulikana nani bingwa hadi mwisho wa msimu.

SOMA NA HII  ZIMBWE Jr AFUNGUKA UGUMU WA MECHI DHIDI YA GWAMBINA