Home Habari za michezo GAMONDI:- SIWALAUMU WASAUZI…

GAMONDI:- SIWALAUMU WASAUZI…

Habari za Yanga leo

Yanga imepoteza mchezo wa robo fainali kwa penalti mbele ya Mamelodi Sundowns, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amekubali yaishe na kuwapongeza wachezaji kwa kucheza mchezo mzuri na kwamba uamuzi uliotolewa hauwahusu kwani kazi aliyowaagiza wameifanya vyema.

Yanga imepoteza mchezo huo juzi usiku kwenye Uwanja wa Liftus Versfeld, jijini Pretoria Afrika Kusini kwa penalti 3-2 mbele ya Mamelodi ambayo imetinga hatua ya nusu fainali baada ya matokeo ya jumla kuwa sare isiyo na mabao kwani ilitoka 0-0 jijini Dar es Salaam na juzi usiku huko Sauzi.

Gamondi amesema Yanga ilitengeneza nafasi nyingi licha ya Mamelodi kufanikiwa katika umiliki wa mpira, lakini wachezaji wake walicheza mchezo mzuri.

“Sitaki kuzungumza mengi kwa sababu naamini kila mmoja ameshuhudia mchezo wetu nasikitika mwamuzi ameshindwa kwenda kuangalia kama Yanga imepata bao halali,” amesema Gamondi na kuongeza;

“Mwamuzi anachukua uamuzi wa kuangalia madhambi ya Joyce Lomalisa kama anastahili kadi nyekundu au njano, lakini anashindwa kuangalia bao halali lililofungwa na Yanga kupitia Aziz KI (Stephane).”

Amesema wameshinda mchezo kwa bao la wazi kabisa anafikiri watu wote walioangalia mpira wanaungana naye kuwa walifunga bao na kama kuna mtu ambaye yupo tofauti na maoni yake aseme.

“Kama kuna watu wa Mamelodi wanafuraha kwa kilichotokea hana shida, Shirikisho la Mpira Duniani (FIFA) linahimiza uungwana michezoni nina maumivu sana kwa mchezo usio wa kiungwana uliofanywa na mwamuzi aliyechezesha mchezo wetu,” amesema kocha huyo raia wa Argentina na kuongeza;

“Siwalaumu watu wa Afrika Kusini namlaumu mwamuzi aliyechezesha mchezo naelewa na yeye ni binadamu lakini amefanya uamuzi mbaya kwanini hajaenda kuangalia uamuzi wa mwisho akisisitiza kuwa anauhakika na uamuzi wake.

“Nashukuru kuiongoza Yanga kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tumecheza na Mamelodi timu kubwa tukipambana kuhakikisha tunapata matokeo lakini uamuzi mbaya wa kudhulumiwa umetoa maamuzi tofauti.”

Tayari uongozi wa Yanga umeandika barua kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kulalamikia maamuzi ya Dahane Beida aliyelikataa bao hilo la Aziz kupitia wasaidizi wanaosimamia VAR wakituhumu uwepio wa viashiria vya upangaji matokeo na kuwabeba wenyeji Mamelodi iliyoenda nusu fainali.

SOMA NA HII  KAMA UTANI VILEE...AZAM FC WAHAMIA SIMBA SC...KAKOLANYA 'AUNDIWA KAMATI'....