Home Habari za michezo MATAMPI KUTUA SIMBA…? ISHU YA MANULA NA LAKREDI UTATA HUU HAPA….

MATAMPI KUTUA SIMBA…? ISHU YA MANULA NA LAKREDI UTATA HUU HAPA….

Tetesi za Usajili Simba

Simba inahaha kumbakisha kipa wake namba moja, Ayoub Lakred ambaye anatingisha anataka kuondoka na kurejea Morocco lakini kukabiliana na presha hiyo, Wekundu hao wameanza mazungumzo na kipa namba mbili kwa ubora kwenye ligi kwa sasa, Ley Matampi.

Uamuzi huo wa Simba unakuja huku kukiwa na sababu tatu zinazombeba Matampi kuwa na nafasi kubwa ya kuvaa jezi ya Simba msimu ujao.

Kwanza kinachowafanya Simba kumuwahi fasta Matampi ni kutokana na kutokuwa na uhakika wa Lakred kuendelea kuwa mchezaji wao kwa msimu ujao kwani Mmorocco huyo ana ofa mbili mezani kutoka kwa klabu kubwa mbili za nchini kwake, Wydad Athletic na Raja Athletic ambazo zote zinamtaka mlinda mlango huyo zikivutiwa na mabadiliko yake makubwa ndani ya Simba.

Lakred ambaye mkataba wake wa mwaka mmoja wa Simba unaisha mwisho wa msimu huu, amebainisha ofa alizonazo zinamshawishi kuondoka Simba kitu ambacho klabu hiyo inapambamana kumbakisha kutokana na kuvutiwa na namna anavyoendelea kuliweka salama lango lao kipindi ambacho Aishi Manula amekuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha licha ya kwamba kuna ugumu wanakutana nao.

Sababu ya pili kwa Matampi kutakiwa na Simba ni namna alivyothibitisha ubora wake akiwa pale Coastal Union kwani ndiye kipa anayeshika nafasi ya pili kwa ubora ndani ya ligi akiwa na clean sheet 11 huku nafasi ya kwanza ikiwa kwa kipa bora mara mbili wa Ligi Kuu Bara mfululizo, Djigui Diarra wa Yanga mwenye clean sheet 13.

Tatu kilichowafanya Simba kumuwahi mapema Matampi ni namna mkataba wake na Coastal Union kuwa ukingoni kumalizika ambapo utaisha mwisho wa msimu huu ukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine zaidi lakini kipa huyo wa zamani wa TP Mazembe, AS Vita na Motema Pembe za kwao DR Congo hataki kuachana na ofa hiyo ya Simba kirahisi akiona ndio klabu ya hadhi yake huku kubwa zaidi ni kipa wa kigeni ambaye atavaa viatu vya Lakred ambaye naye ni kipa wa kigeni.

Simba haitaki kuingia gharama kubwa zaidi ya kutafuta kipa wa kigeni ambaye akija atahitaji kwanza kuzoea mazingira ndiyo maana wakakimbilia kwa Matampi kutokana na kuifahamu ligi baada ya kucheza kwa msimu mmoja.

Bosi mmoja wa juu na ndani ya Bodi ya Simba amefichua kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri kati yao na Matampi na yatashika kasi zaidi kama mwafaka wa Lakred utapatikana hataendelea kuwa kwao kwa msimu ujao.

“Unajua ishu hapa ni kama Ayoub atakubaliana na ofa yetu ya kubaki lakini nani anajua maamuzi yake ya mwisho na mnaona anaaga hata mashabiki kwa kuwaachia vitu kama kumbukumbu? Ukiangalia kwa makipa wanaocheza sasa hapa ndani ukiondoa Diarra basi ni Matampi,” alisema bosi huyo.

“Hiyo ndiyo imetufanya harakaharaka tumemtafuta huyu (Matampi) ili aje kushika nafasi hii na kwa ubora wake kipa huyu kuwa Coastal ni kama pesa imekwenda sehemu isiyokuwa na matumizi makubwa.”

Licha ya kukosa mechi sita za kwanza za ligi msimu huu lakini Matampi ameipa utulivu mkubwa Coastal Union ikiendelea kuifukuzia nafasi ya nne ikiwa imefungwa mabao machache msimu huu ambayo ni 18 tofauti na msimu uliopita iliporuhusu mabao 35.

Simba inaona Mkongomani huyo endapo atakuwa langoni kwao watakuwa wameziba kwa usahihi nafasi ya Lakred pindi Mmorocco huyo ataondoka mwishoni mwa msimu huu.

Wakati hayo yakiendelea Simba inataka kuendelea kumuamini kipa wao namba tatu Ally Salim kuwa kipa namba mbili endapo itapata mwafaka wa nani atakuwa kipa namba moja kati ya Lakred na Matampi wakati huu ambao Manula yupo nje akiuguza majeraha.

SOMA NA HII  HIVI NDIVYO MAXI ALIVYOMPOTEZA SKUDU KIBABE NDANI YA YANGA...