Unajua kwanini aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali aliitwa Field Marshal?
Ni jina la utani alilopachikwa na Wanasimba lakini kumbe lilibeba maana ya kufanya vitu vigumu na vikubwa ili kuhakikisha klabu hiyo, inafanikisha malengo yake.
Field Marshal ni Kiingereza lakini maana yake kwa wepesi ni cheo kikubwa Jeshini ambacho kina nguvu ya kufanya maamuzi ya jeshi na kuongoza, hivyo mashabiki na wanachama walimpachika, baada ya kuona anafanya mambo makubwa katika klabu ya Simba.
Gazeti la Mwanaspoti lilifika nyumbani kwake eneo la Nyumba Nyeupe, Mbagala, Dar es Salaam na kufanya nae mahojiano ambapo miongoni mwa mambo aliyozungumza ni chanzo cha anguko la Simba iliyopoteza makombe mengi ndani ya misimu mitatu;
Anasema baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika misimu mitatu iliyopita, Simba iligawanyika katika makundi mawili, lilikuwepo la Murtaza Mangungu dhidi ya mpinzani wake aliyemshinda Moses Kaluwa.
“Viongozi wa Simba waliniomba niende kuondoa tofauti kwenye matawi, nilianza na Zanzibar ambako walikiri kuwepo kwa makundi hayo nikawapatanisha na baada ya kupatana,ikachinjwa mbuzi tukala tukafurahia, hadi tukafanikiwa kuchukua ubingwa wa Kombe la Muungano,”anasema na kuongeza;
“Baada ya hapo, nilienda mkoani Morogoro nilikutana na wanachama zaidi ya 100, huku kiliwaka haswa, watu walipigana ngumi laivu laivu, nikawaambia piganeni mkimaliza hasira zenu tupatane, lakini mwisho ukawa mwema tukapatana ndipo ikagundulika sababu ya kufungwa mabao 2-1 na Prisons kisha nikaenda Mbeya na kule nikamaliza tofauti zilizokuwepo.
“Plani za sasa ni kuzunguka Tanzania nzima, kuzungumza na wanachama ili turudishe umoja na kumaliza migogoro, Yanga inafanikiwa kwa sasa, wapo kitu kimoja,penye umoja pana baraka za Mungu.
“Hakuna kitu kilichoniuma, kama kufungwa mabao 5-1 na Yanga, nilikaa uwanjani hadi saa 4:00 usiku, watu wakawa wananiuliza mzee Dalali vipi mbona upo hapa hadi muda huu, nikawa sielewi.
HUMWAMBII KITU KWA LAKRED
“Kati ya wachezaji waliofanya vizuri, ukiacha Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ basi kwa hawa wageni ni Ayoub Lakred anastahili pongezi kubwa,”anasema.
Anaulizwa kuhusiana na Clatous Chama maoni yake kwa kinachoendelea huenda msimu ujao asiwe sehemu ya Simba?
Anajibu; “Mnaweza mkang’ang’ania mchezaji kubaki, lakini ni kitu gani atakachokuwa anakizalisha uwanjani, sina maana kwamba ni mchezaji mbaya, amecheza kwa kiwango cha juu, ila kuhusiana na mambo mengine siwezi kuyajibu.”
KAMATI YA USAJILI
“Ninachoshauri ni viongozi wa Simba kuwa na kamati imara ya usajili, itakayokuwa inafuatilia wachezaji kabla ya kuwasajili na siyo kuchukua kila mtu kuja kucheza Simba.
“Nakumbuka kipindi yupo kocha Patrick Phiri, maji yalikatika, nikawa nakwenda kuchota kisimani na ndoo, kisha nawawekea wachezaji bafuni, waoge jambo ambalo lilimshangaza kocha kuona kwa nafasi yangu (Mwenyekiti), nawezaje kujishusha kiasi kile, nikifanya hivyo, nawaambia wachezaji nataka ushindi, walikuwa kina Juma Kaseja na wote walinikubali na kufanya vyema kazi,” anasimulia Dalali aliyesisitiza viongozi wa sasa wawe karibu zaidi na timu kuanzia kambini hadi viwanjani akijinasibu kwenda uwanjani mechi zote za Simba kipindi ni mwenyekiti wa klabu hiyo.
AHMED ALLY KAKULIA SIMBA
Anasema anashangazwa kuona watu wanasema msemaji wa Simba, Ahmed Ally ni Yanga, anawajuza wasichofahamu kuhusu msemaji huyo.
“Ni kijana aliyekulia Msimbazi, alikuwa anakuja klabuni na kutununulia machungwa wazee, akaja akapotea miaka mitatu kumbe alikwenda kusomea uandishi wa habari, baada ya kumaliza masomo yaka akaja kutuhoji,” anasema na kuongeza;
“Japokuwa Simba inafanya vibaya, Ahmed anastahili tuzo yake, amefanya kazi kubwa sana ya kuitetea kwenye nyakati ngumu, Binafsi namkubali sana yule kijana.”
ALIMGOMEA KAWAWA
Aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu, Rashidi Mfaume Kawawa, aliwahi kumuita ofisini kwake na kumwambia Athuman Idd Chuji anatakiwa kwenda Yanga ili kuitwa Taifa Stars.
“Kawawa alikuwa Simba mimi ndiye niliyempa kadi ya uanachama, nikamjibu kiongozi kwani akicheza Simba hawezi kuichezea Stars, akasema kocha mkuu Marcio Maximo ndiye kataka hivyo, nikamjibu haiwezekani, akasema unapata wapi ujasiri wa kubishana na mimi, nenda nje, fikiria halafu rudi unipe jibu,”anasema na kuongeza;
“Nikatoka nje, akaniita tena, kabla sijamjibu nikamuomba kumuuliza swali ambalo kama atanijibu vizuri basi nitakubaliana naye, nikamuuliza, je unaweza ukahama CCM na kwenda CUF, ili ugombee Urais wa nchi? Akajibu kamwe haiwezi kutokea, baada ya hapo nikamwambia wewe ni Simba unawapaje silaha watani wako, akasema nimekuelewa, mwambie Chuji akaendelee na kazi.
“Ajabu tukakutana na zengwe lingine TFF, wakasema usajili wa Chuji kuwepo Simba ni batili hivyo anatakiwa kwenda Yanga, ikabidi aende nikawa sina namna ya kufanya,”alisema muasisi huyo wa Simba Day.
“Katika uongozi wangu nilifanya vitu vingi kama kuanzisha Simba B, Simba Queens, Simba Day, uwanja wa Mo Arena, Matawi, kadi za kisasa na kuboresha ada ya uwanachama na kupata udhamini wa timu,”anasema na kuongeza;
“Kuna kiongozi mkubwa wa serikali aliniona nimepanda Daladala, akawatuma watu ili niende kukutana naye Dodoma, nikasafiri hadi huko, baada ya kufika ofisini kwake, akaniambia mimi ni mtu mkubwa sana kwanini napanda Daladala.
“Kisha akasema nitaje gari ninalopenda kutembelea, nikamjibu sitaki gari, akasema nitoke nje nikatafakari, alifanya hivyo kama mara tatu, ikabidi aniulize nataka nini, nikamjibu nataka udhamini kwenye timu yangu, jambo ambalo lilimshangaza, akaniandikia barua kwenda kwa kiongozi wa kiwanda cha Bia.
“Maana ilikuwa jioni, magari ya kawaida yalikuwa hakuna, niliona kama nachelewa nikapanda Lori usiku kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, mkono wangu haukubanduka mfukoni nilikuwa nahofia barua isije ikadondoka, saa 12:00 asubuhi nikafika katika ofisi Breweries, nikakutana na mlinzi aliyeniambia hawafungui muda huo, nisubiri hadi saa 2:00.
“Saa 2:00asubuhi mabosi wakaanza kufika ofisini, nikawapa ile barua, baada ya kuona mhuri wa serikali, hawakutaka kuniuliza mengi, waliniambia wamekubali kunipa udhamini ila nikaongee na viongozi wa Yanga ili watupe kwa pamoja, nikampigia simu Imani Madega akaja tukasaini mikataba, moja ya vitu walivyotoa ni yale mabasi ya timu.”
Nje na hilo, anasema wakati wa uongozi wake, tawi la Friends of Simba, lilifanya kazi kubwa ya kusajili wachezaji wenye vipaji vikubwa kwa asilimia kubwa, walikuwa wanatoa fedha zao mfukoni.
“Japokuwa nilikuwa tawi la Ngurumo za Simba na baada ya kuanzishwa gazeti la timu lilipoanzishwa liliitwa jina hilo, ambapo kwa sasa tawi hilo linaitwa Mpira Pesa,” anasema na kuongeza;
“Baadhi ya viongozi ambao walikuwepo kwenye tawi la Friends Of Simba na walifanya kazi kubwa ya kupata wachezaji wazuri ni Zacharia Hanspope,Godfrey Nyange ‘Kaburu’ na Evans Aveva.
“ Viongozi hao ndio waliotengeneza Simba B iliyowatoa Jonas Mkude, Christopher Edward, Ibrahim Ajibu, Abdallah Seseme, Said Ndemla, Haruna Chanongo na wengine wengi.”
Anasema mbali na hao, meneja wa Simba Patrick Rweyemamu alihusika kwa asilimia kubwa kuwalea vijana hao, akitoa pesa, muda jambo analoshauri uongozi kumtazama kwa jicho la pekee.
“Simba B yenye nguvu amehusika asilimia kubwa,mkuwauliza kina Mkude, Ajibu, Ndemla, watasema namna alivyowalea kama watoto wake,”anasema.
Kitu kingine anachojivunia ni rekodi ya kuchukua ubingwa bila kufungwa msimu wa 2009/10, huku akitaja siri kubwa kwamba alijenga umoja wa kila mwanachama kuhusika na timu moja kwa moja.
“Tangu hapo hakuna timu ambayo imewahi kuvunja rekodi hiyo, najivunia hilo na siyo rekodi inayohusika na Simba pekee, bali timu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, sijaona ambayo imechukua ubingwa bila kufungwa,”anasema.
UMAFIA ALIANZA KITAMBO
Haikuwa safari rahisi ya Dalali kuwa mwenyekiti wa Simba mwaka 2006-2010, alianzia kwenye ukomandoo miaka ya 80, ambapo alifanya mambo mengi ya kuisaidia timu, hadi akaaminiwa na wanachama kuona anafaa kuongoza.
“Nimefanya umafia mwingi kipindi ni komandoo, Simba ilifungwa na Mecco ya Mbeya mabao 2-0 ilikuwa ya moto ambapo kina Abeid Kasabalala ndio walikuwa mastaa, viongozi walikuwa hawataki kuachia ngazi wakati matokeo tuliyapata mabaya kwa mfululizo, nikafanya mapinduzi,”anasema Dalali na anaongeza kuwa;
“Tulikwenda Tukuyu kwenda kuiteka timu, tulienda na dreva Hassan Mbashiri tukiwa na fimbo za kuwatandikia viongozi, tukachukua timu na kuja nayo Dar es Salaam, ambapo tukaiweka Temeke katika hoteli ya Hazal, yote hayo nilijitoa kuhakikisha timu inafanya makubwa.
“Ukiachana na hilo, nimefanya mapinduzi mengi ya kuwaondoa viongozi madarakani baada ya timu kufanya vibaya.”
Mbali na ukomandoo, alikuwa Mwenyekiti wa Matawi ya mkoa wa Dar es Salaam kwa muda wa miaka 20, ambapo aliutumia kujifunza mengi hasa kiu ya wanachama kuhusu timu yao.
“Niligombea mara nane kwenye nafasi tofauti sikubahatika kuwa kiongozi hadi ilipofika 2006 ambapo nikawa mwenyekiti nikastaafu 2010,”anasema.
MASHABIKI KUMJAZIA KINYESI KWAKE
Anasema mwaka 2008 hatausahau katika maisha yake, anasimulia tukio baya alilofanyiwa na mashabiki baada ya Simba kufungwa na Azam FC mabao 2-0 wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.
“Zilikuja Coaster tatu zilizojaza mashabiki ambao walikuja kunifanyia vurugu nyumbani, ila kuna mtu alinipenyezea taarifa, basi wakashuka kwenye gari wakaanza kupiga mawe nyumba, nikaificha familia yangu, baadaye nikatoka ndani kwenda kuzungumza nao,”anasema na kuongeza;
“Nikawauliza mnataka nini? Wakanijibu ujiuzulu kwasababu umefungwa na Azam, nikawaambia zimebakia mechi nyingi na tupo nafasi ya pili, wakasema hatukutaki, nikawajibu sijiuzulu haya mnataka nini kingine wakasema kujisaidia ndani kwako, nikawafungulia milango.
“Waliingia walikunya kila sehemu nadhani watakuwa walipita kariakoo kula mapera, nikawaambia mmemaliza nendeni mkajisafishe uwani kuna jaba la maji, wakajisafisha wengine walienda mbali kujisaidia sehemu ambapo naswalia wengine hadi juu ya bati”anasema.
Anasema baada ya kufanya tukio hilo wakaondoka na siku ya pili akaenda makao makuu ya klabu, akawakuta mashabiki akawaambia amejiuzulu.
“Kuna waziri aliona tukio hilo akanipigia simu nirudi kazini, akanisaidia kuwapeleka mashabiki polisi, baada ya kuwabana wakamtaja kiongozi mwenzangu aliyewakodisha aliwapa laki tatu (300,000) wakaniomba msamaha nikawasamehe, kwani kiongozi huyo alikuwa kati ya watu ambao niliwapindua wakati anaongoza,”anasema.
Anasema baada ya wiki mbili alirejea tena klabuni na kufuta kauli yake ya kuachana na uongozi na kwakuwa hakuandika kwa maandishi hadi alipostaafu 2010.
“Wale ambao walijisaidia sehemu ambayo nilikuwa naswalia walikufa kama sita, baadhi wakaja wakaniomba msamaha niliwaambia wamuombe Mwenyezi Mungu, hayo ni baadhi ya matukio niliyokutana nayo,”anasema.
Nani alifanya usafi baada ya mashabiki hao kuchafua nyumba yake! Anajibu “Nilimuomba mke wangu anisamehe anivumilie na akubaliane na kazi yangu, alifanya usafi ingawa familia ilinikataza nisiendelee kufanya kazi hiyo ila haikuwezekana.”
MASHABIKI WAKIMBIZA WADHAMINI
Anasema miaka 2006 alipata udhamini wa benki ya Afrika Kusini, ambayo walikubaliana kujenga gorofa 25, ili wao wazifanyie kazi miaka 10 na baadaye kuwaachia Simba lakini mashabiki walitibua dili hilo.
“Walikubali kutujengea ghorofa 25 pale Msimbazi na masharti ilikuwa ndani ya miaka 10 tuwape ghorofa tano kuanzia chini wazitumie wao, 20 zilikuwa za kwetu baada ya hapo tungeachiwa kabisa, pia aliahidi kujenga hospitali, kuna mzungu alitumwa kupiga picha, wakaja wanachama na kuanza kumpiga hadi camera ikavunjika, wakidhani tunataka kuuza jengo,” anasema na kuongeza;
“Walianza kusema Dalali na tawi lake la Friends of Simba wanataka kuuza mali za klabu, kitu ambacho nisingeweza kukifanya kwasababu lazima ningewaita wanachama kuwaambia nini nawaza, basi baada ya kuwaelewesha wakaelewa, ilinibidi niende tena kwenye hiyo benki wakakataa kurudi wakaona sisi ni watu wa vurugu,”anasema.
MATUKIO MAGUMU
Anasema mwaka 1975, walifungwa na Yanga bao 1-0 fainali za Afrika Mashariki, matokeo yaliomuumiza shabiki mmoja aliyemtaja kwa jina la Malenda alijiua.
“Fainali hizo zilipigwa Zanzibar, Malenda alikuwa anafanya kazi katika kiwanda cha nyuzi, katika kiwanda hicho chini kulikuwa na mapipa ya maji ya moto ambayo yalikuwa yanachuja nyuzi, akajitumbukiza humo na kufa kifo kibaya sana,”anasema na kuongeza;
“Tukio lingine lililoniumiza nililiona kupitia kwenu Mwanaspoti la mtoto wa miaka tisa Joshua, aliyejinyonga miaka miwili iliyopita baada ya Simba kufungwa bao 1-0 na Yanga, ndio maana nakuwa najitoa kwa kila hali, kuona Simba inafanya vizuri.”
SOKA NA ELIMU
Anasema baada ya kuwa mwenyekiti wa Simba, mwaka 2006 alibadilisha katiba ya kiongozi wa kujitolea angalau awe na elimu ya kidato cha nne, ambayo ndiyo inayotambulika TFF.
“Wakati nabadilisha katiba elimu yangu ilikuwa darasa la saba,japokuwa baadaye nilikwenda kusoma hadi kidato cha nne na nikafaulu, baadaye ikaja anayetakiwa kuwa kiongozi awe na digrii, basi hadi nifikie levo hiyo, ningekuwa kibabu cha miaka 100, walidhani nataka nirejee kwenye uongozi, jambo ambalo halikuwa kweli,” anasema Dalali na anaongeza;
BENDERA YA SIMBA JANGWANI
“Kuna mwaka nilikwenda kwenye klabu ya Yanga usiku, nilikuwa nimevalia baibui, nikawakuta wazee ambao wanakunywa kahawa, basi nikapanda hadi juu ya jengo lao, nikafunga bendera ya Simba ikawa inapepea, asubuhi wakakutana nayo, wakaanza kushangashangaa nakuona kama uchawi, kumbe nilikuwa nawachezea akili tu,” anasema na kuongeza;
“Nilifanya hivyo kwani mbele yetu, kulikuwa na mechi na tukashinda, maana wakaanza kutumia muda mwingi kuhangaika na bendera, badala ya kuweka nguvu kwenye timu.”
ANACHOTAMANI KIFANYIKE
“Natamani kuona uwanja wa Bunju unamalizika, kwani timu aina ya Simba inapaswa kumiliki uwanja wake, mfano timu kubwa zinamiliki uwanja, ndio maana zina maendeleo makubwa,”anasema.
“Mimi Simba nimeifanyia kila kitu kwakuwa naipenda kutoka moyoni. Sina inachonidai lakini mimi napendekeza waandike vyema historia na ikiwezekana jina langu liwekwe makumbusho kuwa nilianzisha tamasha la Simba Day, pia niliifanya klabu kupata eneo la uwanja bila kuzisahau timu za vijana za Simba na ile ya wanawake,” alihitimisha Dalali.