HABARI ZA YANGA LEO; Serikali imefikia uamuzi wa kutoa ruhusa kwa klabu ya Yanga kujenga uwanja wake wa kisasa katika eneo la Jangwani yalipo makao makuu ya klabu hiyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amebainisha hayo leo katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Yanga akionya kwamba Yanga imepewa muda maalum wa kukamilisha ujenzi huo wa uwanja na kwamba ikishindwa itanyang’anywa.
“Tumewapa muda wa kuyafanyia kazi yale ambayo tumewaambia kwenye uwanja huo, ila mkishindwa tutawanyang’anya, tumewapa kipimo, hivyo mzingatie iendane na mpango wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu, kulifanya jiji la Dar es Salaam kuwa la kisasa,” alisema.
Mbali na Yanga, alisema Tamisemi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Michezo na BMT, watachagua wachezaji bora ambao watakuwa wanakuza vipaji vya watoto.
“Nimeambiwa Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Michezo nchini, Ally Mayay na Edibily Lunyamila ni zao la UMITASHUMTA na UMISETA, ndio maana chini ya Rais Samia anawekeza nguvu katika michezo mashuleni,” alisema.
“Namshukuru rais wa Yanga, Injia Hersi Said kwa kuendesha klabu yenye mafanikio makubwa, ikiwemo uwekezaji na usajili wa wachezaji wazuri na kuleta utulivu wa Yanga, nakumbuka miaka kadhaa iliyopita kabla ya uongozi wa Injinia Hersi, tulifanya kazi kubwa na nilikuwa sehemu hiyo ya mabadiliko, utulivu huo umeleta mafanikio makubwa chini ya Injinia na sasa Yanga inafanya vizuri ligi ya ndani hadi kimataifa,” alisema.