SIMBA ameitupia dogo Yanga. Uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi umeeleza sababu ya kusimamisha zoezi la kutoa `Thank You` kwa wachezaji wengi ni kuhofia kuingia katika orodha ya Shirikisho la mpira wa miguu la Kimataifa (Fifa).
Hivi Karibuni Yanga ilifungiwa mara mbili na Shirikisho hilo la Kimataifa FIFA na Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutosajili hadi kuwalipa baadhi ya wachezaji ambao waliachana nao ambao hawajalipwa haki zao.
Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuna wachezaji bado wana mkataba na klabu hiyo na wanamalizana nao kwa kuvunja mkataba na kuwalipa haki zao.
Ahmed amesema wanatarajia kuwapa Thank You wachezaji wengi kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na michuano ya Kimataifa.
Amesema zoezi hilo litaendelea baada ya kumalizana na wachezaji wao ambao wanaowatema kwa kumalizana vizuri ili kuepuka kupelekana fifa kwa ajili ya madai.
“Wapo wengi ambao watapewa Thank You kuliko waliopewa ambao ni sita, lakini zoezi limesimama na tunataka kuwalipa wale tunaovunja nao mikataba kwa sababu hatutaki kuingia kwenye orodha ya wadaiwa sugu na kufungiwa kusajili,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa baada ya kumaliza na wachezaji hao zoezi hilo litaendelea kwa kutangaza wanaoachwa na baadae kuweka wazi nyota wapya ambao watakuwepo kwenye kikosi cha msimu ujao.
Katika hatua nyingine Ahmed ametangaza rasmi kilele cha Simba Day inayotarajiwa kufanyika uwanja wa Benjamin Mkapa, Agosti 3, mwaka huu.
Amesema kawaida ya Simba day hufanyika Agosti 8, ya kila mwaka lakini kulingana na kuwepo kwa michuano ya Ngao ya Jamii siku hiyo wamerudisha nyuma tamasha lao.
“Kabla ya kilele chake kutanguliwa wiki ya Simba, itakayoanza Julai 24, itakuwa na matukio mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuchangia dabu na kutoa kwa wenye mahitaji maalum.
Siku hiyo kutakuwa na matukio makubwa ya burudani kabla ya kuanza mchezo wenyewe. Tutautumia kutambulisha kikosi chetu kuelekea msimu wa 2024\25 wa ligi,” anasema Ahmed.