Home Habari za Simba Leo TSHABALALA ASHUSHIWA MPINZANI WAKE…VALENTINO NOUMA

TSHABALALA ASHUSHIWA MPINZANI WAKE…VALENTINO NOUMA

Habari za Simba

Baada ya miaka zaidi ya sita kupita uongozi wa Simba umefanya uamuzi mgumu kwa kusajili beki wa kushoto mgeni wakinasa saini ya Valentino Nouma aliyekuwa anakipiga Saint Eloi Lupopo ya DR Congo.

Nouma anaungana na Tshabalala ambaye alijiunga na Simba Juni 2014 akitokea Kagera Sugar ya Bukoba baada ya awali kuchezea pia akademi ya Azam FC.

Tshabalala ndiye mkongwe aliyebaki kwenye kikosi cha Simba ambaye anacheza nafasi hiyo mara ya mwisho kuletewa changamoto ya kigeni ni kipindi timu hiyo ilipomsajili Asante Kwasi akitokea Lipuli ambaye alifanikiwa kutwaa taji akiwa na timu hiyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeeleza kuwa wamefanya uamuzi wa kumsajili mchezaji huyo akiwa huru baada ya kumaliza mkataba wake na timu yake kwa lengo la kuongeza nguvu eneo hilo.

“Tshabalala ni beki bora na amekuwa akifanya vizuri kwenye timu yetu na timu ya taifa tunatambua thamani yake kumuongezea nguvu ni kuhakikisha tunampa muda mzuri wa kupumzika ili aendeleze ubora,” kilisema chango hicho na kuongeza;

“Ujio wa beki huyo utaongeza chachu ya ushindani na ubora eneo hilo hasa kipindi hichi ambacho timu inatengeneza timu bora na ya ushindani, lakini pia itatoa mwanya kwa kocha kufanya mabadiliko kulingana na ubora wa mchezaji.”

Alipoulizwa juu ya mkataba waliompa beki huyo alisema wamemsainisha miaka miwili kutokana na umri alionao na wanaamini ni chaguo sahihi kwao na wanatarajia mambo makubwa kutoka kwake haswa kwenye Kombe la Shirikisho.

“Kwasasa unasomeka mwaka mmoja ambao utamfanya amalize wa pili kama ataonyesha kiwango bora ambacho tunakitarajia kutoka kwake lakini hadi sasa kila kitu kimekamilika anaungana na timu muda wowote kuanzia sasa kabla ya timu aijasafiri kwenda nchini Misri tayari kwa kambi maalum ya msimu mpya.”

Kwa sasa Tshabalala ana miaka 10 ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi na amekuwa na ubora ule ule wa kiwango chake licha ya kuletewa wachezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi ila walichemka mapema na kumuacha nyota huyo akiendelea kupeta hadi sasa.

Wachezaji walioletwa kikosini Simba wanaocheza nafasi yake ya beki wa kushoto ni wengi na wameshindwa kufurukuta ila tu baadhi yao walikuwa ni Jamal Mwambeleko aliyesajiliwa na kikosi hicho akiwa na kiwango bora wakati akiitumikia Mbao FC.

Mwambeleko licha ya kiwango bora alichokuwa nacho wakati akiwa na Mbao ya jijini Mwanza ila ujio wake Simba ulikuwa kama kaa la moto kwani alishindwa kupenya kwa ‘Tshabalala’ na mwishoni aliomba kuondoka na kujiunga zake na Singida United.

Mwingine ni Mghana, Asante Kwasi ambaye naye alionekana huenda akapindua ufalme wa ‘Tshabalala’ Simba wakati anasajiliwa mwaka 2017 akitokea Lipuli ya Iringa kutokana na ubora wake wa kuzuia na wakati huohuo kuanzisha mashambulizi ya hatari.

Kwasi alionekana ni mchezaji tishio ingawa naye alijikuta akishindwa kupigania namba na nyota huyo na baada ya kudumu misimu miwili aliondoka ndani ya kikosi hicho 2019 na kujiunga na klabu ya Hafia ya Guinea.

Nyota mwingine aliyeingia kwenye mtego wa ‘Tshabalala’ ni Gadiel Michael ambaye alijiunga na kikosi cha Simba 2019 akiwa ni chaguo namba moja akitokea Yanga ila mambo yalikuwa magumu kwake na baadaye kuondoka na kujiunga na Singida Fountain Gate sasa anakipiga Cape Town Spurs FC ya nchini Afrika Kusini.

SOMA NA HII  OKWI AWAPA MTU WA MAANA SIMBA...STEVE MUKWALA DEAL DONE