Home Habari za Simba Leo ALIYETAMBULISHWA SIMBA AZUA BALAA ZITO…VALENTINO MASHAKA

ALIYETAMBULISHWA SIMBA AZUA BALAA ZITO…VALENTINO MASHAKA

habari za Simba, Mashaka

Wakati Geita Gold ikiijia juu Simba kumtambulisha mchezaji Valentino Mashaka ikidai hawakufuata utaratibu kwa madai bado ni mali yao, nyota huyo ameiruka timu hiyo akieleza mkataba wake ulikuwa umeisha.

Simba imemtambulisha Mashaka leo Julai 5 akiwa ni mchezaji wa tano kusaini kandarasi kwa wachezaji wapya, jambo ambalo limeonekana kuwashtua Geita Gold wakidai kuwa bado nyota huyo alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa Mwanaspoti Mashaka amesema mkataba wake ulikuwa umeisha na hata hivyo kipo kipengele cha kuwa iwapo timu itashuka daraja ikija ofa ataweza kuondoka.

“Kwanini waje kueleza sasa hivi baada ya mimi kupata timu?” amehoji na kuongeza:

“Mimi mkataba wangu ulikuwa umeisha na pia kulikuwa na kipengele cha kwamba timu ikishuka daraja ninaweza kuondoka hivyo waniache,” amesema nyota huyo.

Kwa upande wake Afisa Habari wa Geita Gold, Samuel Dida amesema Simba imekiuka utaratibu katika kumsajili mchezaji huyo akieleza kuwa bado alikuwa na mkataba.

Dida amesema katika kandarasi ya miaka miwili aliyokuwa nayo mchezaji huyo, alikuwa ameitumikia msimu mmoja na kwamba Wekundu hao walipaswa kuwasiliana na uongozi wa Geita Gold kabla ya kufikia uamuzi huo.

“Mashaka alisaini miaka miwili ambapo mpaka saaa tumeshamlipa asilimia 90 ya fedha ambazo tumekubaliana, ametumikia mwaka mmoja bado mmoja hivyo Simba wametukosea kumsajili bila sisi kujua”

“Mkataba aliosaini Mashaka unasema mkataba utavunjika pale timu itakapofilisika kwa maana ya kushindwa kumlipa au timu ikishuka daraja kutoka Ligi kuu kucheza ligi za chini,” amesema na kuongeza:

“Lakini mkataba haukuishia hapo ukaweka kipengele ambacho kinasema ili mchezaji aondoke lazima pande mbili zijadiliane ndipo aondoke kwa mantiki hiyo kipengele hicho hakijafuatwa hadi yeye kusajiliwa Simba.”

Dida ameongeza kuwa mchezaji huyo aliipeleka timu hiyo shirikisho la soka nchini (TFF) akidai malipo ya asilimia 10 ambayo aliyadai kwenye mkataba wake aliousaini na sasa wanashangazwa kuona utambulisho wake Simba mtandaoni na kwamba uongozi utawaburuza Wekundu hao kwa sakata hilo.

Lakini inaelezwa kwamba katika mkataba wa Mashaka na Geita kulikuwa na kipengele kinachovunja mkataba wao, endapo timu itashuka daraja na sasa timu hiyo haipo Ligi Kuu ya NBC.

Ukurasa namba 7 kifungu cha 29 kuhusu Kuvunjika kwa Mkataba kwenye kipengele cha (6) kinasema:

“Mkataba utavunjika endapo Geita Gold Football Club itashuka daraja”

SOMA NA HII  VITUO VYA TIKETI MECHI YA SIMBA SC VS HOROYA AC...TIKETI ZA MZUNGUKO BUKU 3 TU...TWENZETU KWA MKAPA