Home Habari za Yanga Leo KAULI 3 ZINAZOASHIRIA UWEPO WA AZIZ KI YANGA.

KAULI 3 ZINAZOASHIRIA UWEPO WA AZIZ KI YANGA.

HABARI ZA YANGA, Aziz Ki

Kumekuwa na hisia tofauti juu ya hatima ya Stephene Aziz Ki licha ya Rais wa Yanga, Hersi Said kudai kwamba bado hajasaini mkataba mpya na wanapambana kuhakikisha anabakia klabuni hapo.

Lakini kuna kauli tatu ambazo zinaendelea kuwapa matumaini mashabiki wa Yanga,  kuendelea kubaki na mchezaji bora wa Ligi Kuu wa Msimu juzi na Mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa na mabao 21.

KAULI YA KWANZA ILIYOKAA KIMKAKATI.

“Ni mkakati wa klabu kuhakikisha mchezaji anabaki na majadiliano yanaendelea vizuri na hapana shaka tutarudi kufanya utambulisho ingawa kuna klabu nyingi zinamhitaji mchezaji.”

“Hivyo majadiliano yanaendelea na ninaweza kusema kuna nafasi kubwa kwa mchezaji kubakia lakini hatujakamilisha.

“Aliweka wazi kuwa anataka kubaki unajua nilimsaini miaka miwili iliyopita na nilimsajili kutoka Asec Mimosas na nikamueleza kuhusu ‘project’ yangu na nani nataka waipeleke klabu katika ngazi za juu na akawa sehemu muhimu ya program na mpango, ambao upo hi vyo majadiliano yakawa yaleyale na alisema wazi kuwa nahitaji kubaki hapa na kuipeleka Yanga katika ngazi ambazo unataka ifike.

“Lakini mpira ni biashara sasa unaweza kusema unataka kubaki lakini hali ya kifedha ikabadilisha mawazo kwa hiyo naweza kusema ni 60/40 (uwezekano wa kubaki),” alisema Hersi.

KAULI YA  PILI YA AZIZ KI MWENYEWE.

“Dube anakuja, (Joseph) Guede yupo, nisikilize, mimi ni kiungo, nitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanakuwa wafungaji bora. Mimi ni kiungo kwa nini niwanie ufungaji bora, kwa nini ununue straika halafu utake kiungo awe mfungaji bora.

“Mimi ahadi yangu, nina matumaini straika wa Yanga atakuwa mfungaji bora msimu ujao Mungu akipenda, lakini sio Aziz, sahau kuhusu Aziz, mimi nitatoa asisti na siyo kuwa mfungaji bora,” alinukuliwa Aziz Ki katika moja ya mazungumzo yake.

KAULI YA GAMONDI.

Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alisisitiza kuwa anahitaji kumkuta kiungo huyo kambini pindi atakapojiunga nayo na sio vinginevyo.

Kumekuwa na hisia kwamba uongozi wa Yanga umeshamalizana na mchezaji huyo na unachokifanya kwa sasa kutangaza kuwa hajasaini mkataba mpya ni kujaribu kutengeneza thamani ya tukio la utambulisho wa mkataba mpya wa mchezaji huyo.

Hisia hizo zinaweza kuthibitishwa na mmoja wa wajumbe katika uongozi wa Yanga ambaye hakupenda jina lake kutajwa ambaye alifichua kuwa Aziz Ki atakuwa kwenye kambi ya timu hiyo Afrika Kusini.

“Kambi ya maandalizi ya msimu mpya tutafanya Afrika Kusini na Aziz Ki atajiunga na timu huko hatuna wasiwasi wowote,” alisema kiongozi huyo.

SOMA NA HII  KIPA ORLANDO AIGOPA SIMBA...AWATONYA HAYA WYDAD CASABLANCA