KATIBU wa Coastal Union, Omary Ayoub amesema shauri la beki wao Lameck Lawi bado lipo chini ya Kamati ya Hadhi na haki za wachezaji inayosimamiwa na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF.
Katibu huyo aliongea hayo baada ya kutoka katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika makao makuu ya TFF, Karume kujadili masuala mbalimbali ikiwemo haki na uhalali wa Lawi ni mchezaji wa Simba au kubaku Coastal Union.
Omary amesema waliitwa kwenye kamati na kusikilizwa pande zote mbili na wanasuburi shauri na maamuzi kutoka kwenye Kamati.
“Tunaimani na hivi vyombo vinavyosimamia, maamuzi yakiamulia mchezaji aende Simba bure bila Coastal Union kupata chochote tutaridhia, pia tukiambiwa Lawi abaki basi hatuna pigamizi, tunaimani na kamati,” amesema Katibu huyo.
Kwa upande wa Simba waliwakilishwa na wanasheria wao ambao baada ya kumalizika kwa shauri lao waliondoka huku Kamati ikiendelea kusikiliza mashauri mengine yaliyofika mezani kwao.