Home Habari za Simba Leo TSHABALALA AWAPA SIRI WACHEZAJI WAPYA…KISA MECHI YA SIMBA NA YANGA

TSHABALALA AWAPA SIRI WACHEZAJI WAPYA…KISA MECHI YA SIMBA NA YANGA

Habari za Simba- Tshabalala

WAKONGWE wa kikosi cha Simba wameanza kuwapa semina elekezi wenzao wapya waliosajiliwa msimu huu juu ya utamaduni wa timu hiyo na na umuhimu wa mechi ya ‘dabi’ katika soka la Tanzania.

Nahodha wa kikosi hicho, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, amesema mara baada ya kufahamu tarehe na uwanja utakaochezwa mechi ya Ngao ya jamii dhidi ya watani zao Yanga, yeye na wachezaji wenzake waliopo kwenye kikosi hicho muda mrefu, wameanza kuongea na wenzao wapya hasa wale wa kigeni juu ya utamaduni wa mechi hiyo na umuhimu wa kushinda.

“Mechi dhidi ya watani tulikuwa tunaifahamu, ambacho hatukufahamu ni tarehe na uwanja tutakaocheza, sasa tumeshafahamu, kwa sasa tuna wachezaji wengi wapya hasa wa kigeni, tumeanza na tunaendelea kuwakumbusha umuhimu wa mechi hiyo.

“Tunawaaambia katika nchi yetu mechi kubwa ni ya Simba na Yanga, ni dabi na ipo katika tarehe za mwanzo kabisa kabla ya msimu kuanza, tunawakumbusha kuwa ni muhimu kushinda mechi hiyo kwa sababu itawafanya hata wao kuwa na utulivu na kutokuwa na presha kutoka kwa mashabiki kama tukipata ushindi,” alisema Tshabalala.

Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii, maalum kwa ajili ya kufungua msimu mpya wa Ligi Kuu, itachezwa Agosti 8 saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mshindi atacheza fainali Agosti 11 dhidi ya mshindi kati ya Coastal Union au Azam FC, mechi hiyo itachezwa saa 10:00 jioni kabla ya mechi ya watani, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa na idadi kubwa ya wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa kutoka sehemu mbalimbali  barani Afrika.

Pia itakuwa na wachezaji wapya wazawa ambao imewasajili kuelekea msimu mpya.

Tshabalala alisema shida ni ndogo kwa wazawa kwa kuwa wao wanafahamu mazingira na utamaduni wa mechi hiyo ambapo mbali na kwamba ndiyo kwanza watakuwa wanacheza dabi hiyo lakini wamezaliwa na kukua nchini hivyo wanaelewa mazingira na nini wanatakiwa kufanya.

Beki huyo wa kushoto alisema mbali na mkakati huo kabambe kuhakikisha wanashinda mechi hiyo, lakini pia wako kwenye maandalizi ya Simba Day, pamoja na ya msimu mzima wa mashindano.

“Pamoja na hayo, pia akili yetu ipo kwenye maandalizi ya msimu mzima, kabla ya hapo tuna mechi ya kirafiki ya ‘Simba ‘ ambayo itakuwa ni maadalizi tosha ya mchezo wa watani,” alisema nahodha huyo.

Kwa upande wake, straika Freddy Michael aliyesajiliwa katikati ya dirisha dogo la usajili, amesema anajua nini wanataka mashabiki wa Simba hivyo amejipanga kufunga magoli mengi.

“Tuna wachezaji wazuri sana, na mazoezi yamekuwa ‘sapraizi’ sana kwetu, hasa mimi nimefurahi kwa kuanza mazoezi ya maandalizi nikiwa na timu hii tofauti na nilivyokuja, nataka nionyeshe nilichonacho kwenye ligi.

“Nitajitahidi kila njia ili kuisaidia timu na kuwaridhisha mashabiki wa Simba ambao wanataka mabao zaidi kutoka kwangu,” alisema mchezaji huyo raia Ivory Coastal aliyesajiliwa kutoka Green Eagles ya Zambia.

Wakati huo huo, wachezaji Willy Onana na Awesu Awesu, wamewasili kwenye kambi ya timu hiyo nchini Misri.

Onana amerudishwa baada ya klabu hiyo kushindwa kupata saini ya Willy Mpanzu huku Awesu akiwa ni mchezaji mpya aliyesajiliwa kutoka KMC.

SOMA NA HII  GAMONDI AELEZA ALIVYOHUSIKA...KUMBAKIZA MZIZE YANGA