Home Habari za Simba Leo LAWI AJIUNGA TIMU YA SAMATTA ULAYA.

LAWI AJIUNGA TIMU YA SAMATTA ULAYA.

HABARI ZA SIMBA-LAMECK LAWI

WAKATI Coastal Union ikiendelea kupambana na Simba juu ya nani ana haki ya umiliki wa kimkataba wa Lameck Lawi, beki huyo ametua rasmi Ubelgiji kumalizia taratibu za kujiunga na K.R.C Genk ya nchini humo.

Simba na Coastal zimeburuzana Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kila moja ikipigania uhalali wa kummiliki beki huyo.

Hata hivyo, bado hatma ya beki huyo haijajulikana kufuatia kamati hiyo kuzitaka klabu hizo kukaa mezani na kumalizana kufuatia sakata hilo.

Wakati klabu hizo zikiwa mezani Lawi, ametua Genk kumalizia taratibu za kujiunga na miamba hiyo ya soka ya Ubelgiji.

Jana Lawi alikuwa anasubiri mchakato wa kupima afya, ili asaini mkataba wa miaka mitatu na Genk iliyowahi kutumikiwa na nyota wawili wa kimtaifa wa Tanzania, Mbwana Samatta na Kelvin John ‘Mbappe’.

“Amefika salama Ubelgiji (Lawi), leo (jana) alikuwa afanye vipimo vya afya, safari yake tuliifanya ya kimyakimya ili kuondoa mazingira ya ukwamishaji kwa kuwa hata alipopata visa tu kuna watu walitaka asiipate, bahati nzuri wakakuta tayari ilishatoka,” alisema bosi mmoja wa juu wa Coastal.

COASTAL HIYOO PEMBA

Wakati sakata la Lawi likichukua sura hiyo mpya, klabu ya Coastal Union imeendelea na maandalizi ambapo baada ya ratiba ya mechi za Ngao ya Jamii kutoka imebadilisha hesabu na sasa imepanga kwenda Pemba kuweka chimbo kabla ya kuivaa Azam FC Agosti 8 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, mjini Unguja.

Coastal na Azam zitavaana visiwani humo mechi itakayopigwa saa 10:00 jioni kabla ya saa 1:00 usiku watetezi Simba kukabiliana na Yanga katika mchezo mwingine utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ambao pia utatumiwa kwa pambano la fainali ya michuano hiyo siku ya Agosti 11.

Kutokana na mechi kupigwa visiwani, Coastal imebadilisha ratiba ya kwenda kuweka kambi fupi jijini Mombasa, Kenya sasa itaenda Pemba.

Coastal itaondoka Tanga muda wowote kuanzia leo kwenda huko ili kujiweka fiti kwa mchezo huo ambao mshindi atavaana na yule wa Dabi ya Kariakoo ili kupata bingwa na kuzinduliwa rasmi kwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025. Msimu uliopita Simba iliitambia Yanga kwa penalti 3-1 mechi ikipigwa jijini Tanga.

SOMA NA HII  KAPOMBE, MANULA WASHUSHA PRESHA SIMBA...AHMED ALLY AFUNGUKA 'MBILINGE KAKARA' LILIVYO KABLA YA J/MOSI...