Home Habari za Simba Leo KUMBE AWESU NI MNYAMA KITAMBO SANA…MWENYEWE AFUNGUKA

KUMBE AWESU NI MNYAMA KITAMBO SANA…MWENYEWE AFUNGUKA

HABARI ZA SIMBA- AWESU

KIUNGO mshambuliaji mpya wa Simba, Awesu Awesu ameshatua kambini sambamba na winga Mcameroon, Willy Onana na kuweka bayana anavyojisikia kuanza mazoezi na timu aliyokuwa akiiota kwa muda mrefu kuitumikia nchini.

Awesu aliyesajiliwa na Simba hivi karibuni kwa mkataba wa miaka miwili akitokea KMC, alitua juzi kambini na kuanza mazoezi na wenzake akiwamo Onana aliyejumuishwa kambini baada ya dili la kunaswa kwa winga kutoka DR Congo, Elie Mpanzu kutibuka mwishoni.

Mara baada ya kutua kambini jijini Ismailia, Misri nyota huyo aliyemaliza Ligi Kuu Bara msimu uliopita akiwa amefunga mabao mawili na kuasisti mabao matano mengine alifanya mahojiano na mtandao wa klabu hiyo na kuweka bayana anavyojisikia kujiunga na timu ya ndoto yake.

Awesu alisema kwa muda mrefu alikuwa na ndoto za kuitumikia Simba, lakini anashukuru kwa sasa ndoto hiyo imetimia na anaomba Mungu amsaidie aweze kuifanya kazi kwa ufanisi na kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo.

Kiungo huyo mwenye asili ya Zanzibar aliwahi kutakiwa na Simba mwaka 2017 wakati akiitumikia Madini FC iliyokuwa Daraja la Pili (sasa First Division), alipofuatwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zakaria Hans Pope (sasa marehemu), lakini mambo yalikwama na kuishia kukipiga Mwadui, Singida United, Azam FC, Kagera Sugar na KMC.

“Nimejisikia furaha kwa sababu nimekuja katika timu ambayo nilikuwa naiota, nilikuwa naiwaza siku zote na nimefurahi kukutana na wenzangu,” alisema Awesu aliyefurahishwa na mapokezi aliyopewa na wenzake aliodai sio wageni sana kwake, kwani anafahamiana nao, japo yeye ni mgeni kikosini.

Awesu alisisitiza kwa sasa anashirikiana na wenzake ili kuhakikisha wanaisaidia Simba katika michuano watakayoshiriki, lakini kubwa ni kufurahi kuwa Mnyama.

“Nimefurahi sana, unajua ukikaa kwenye kitu unachokipenda na kukiwaza, lazima uwe na amani,” alisema Awesu, aliyekamilisha idadi ya wachezaji 13 wapya wa Simba walioingia katika dirisha la usajili lililo wazi kwa sasa, wakiwamo saba wa kigeni na sita wa kizawa akiwamo yeye.

Nyota wapya waliotua Simba katika dirisha hili ni Debora Mavambo, Valentin Nouma, Augustine Okejepha, Steven Mukwala, Chamou Karabou, Joshua Mutale na Charles Ahoua wote wakiwa wa kigeni, wakati wazawa mbali na Awesu pia kuna, Mashaka Valentine, Abdurazak Hamza, Omary Omary, Kelvin Kijili na Yusuf Kagoma, huku beki Lameck Lawi aliyekuwa wa kwanza kutambulishwa dili likiingia vikwazo kutoka Coastal Union.

SOMA NA HII  SIMBA KUJIFARIJI NA KOMBE JIPYA LA CAF...AHMED ALLY AFUNGUKA A-Z VYUMA VITAVYOSHUKA...