Home Habari za Simba Leo VALENTIN NOUMA AANZA NA TSHABALALA…BALAA LAKE USIPIME

VALENTIN NOUMA AANZA NA TSHABALALA…BALAA LAKE USIPIME

Habari za Simba- Valentin Nouma

SIMBA inaendelea kujifua ikiwa kambini Ismailia, Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano ili irudi na moto wa kurejesha mataji iliyopoteza misimu mitatu iliyopita, lakini Valentin Nouma amemshushia mkwara mzito nahodha wa kikosi hicho akimtaka akae chonjo.

Nyota huyo wa kigeni aliyepiga mkwara ni beki wa kushoto, ambaye kazi kubwa ni kuja kushindana na beki na nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye kwa misimu mitatu amejimilikisha nafasi.

Nouma ni kati ya wachezaji saba wapya wa kigeni waliotua Msimbazi na alikuwa katika msafara wa awali wa Simba kutua kambini kuanza maandalizi.

Valentin Nouma raia wa Burkina Faso, amesema anauheshimu uwezo mkubwa na hata ukarimu alionao Tshabalala na kwamba japo amemkuta ndani ya kikosi hicho, lakini anataka kupigania nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

Beki huyo aliyetokea klabu ya FC Lu-popo ya DR Congo, alisema kwa siku ambazo amekaa kambini na Tshabalala amegundua, jamaa anastahili kuwa nahodha na hata chaguo la kwanza lakini yeye hataki kuwa msindikazaji kikosini.

Nouma alisema hata alipofika FC Lupopo alikutana pia na beki Chadrack Boka aliyetua Yanga, aliyekuwa ana jina kubwa ndani ya DR Congo, lakini alipambana kutumia ubora kumpunguzia mechi za kuanza ndani ya kikosi hicho.

“Tshabalala ni beki mzuri kwa siku ambazo nimekaa naye hapa kambini, nadhani alikuwa anastahili kuanza mara kwa mara na sio kuanza tu hata kuwa nahodha wa timu hii, ni mtu mzuri na mkarimu,” alisema Nouma na kuongeza;

“Sitaki kuifanya kama vita hapa kati yetu lakini nilichopanga ni kutumia uwezo wangu kupata nafasi ya kucheza mechi za kutosha, ninachofahamu hakuna kocha anayeweza kukubali mchezaji mzuri asicheze.

“Nitakachofanya ni kama ambavyo nilifanya Lupopo nilimkuta Boka akiwa na jina kubwa pale na hata Congo nzima lakini nilifika na kuonyesha ubora wangu nikapata mechi za kucheza na yeye alicheza.”

Nouma alisema malengo ya kutaka kupata nafasi ndani ya Simba yanalenga kutafuta ushawishi wa kuendelea kuitwa timu ya taifa ya Burkina Faso.

Mbali na Nouma nyota wengine wa kigeni waliosajiliwa Simba ni Chamou Karabou, Augustine Okejepha, Debora Mavambo, Joshua Mutale, Steven Mukwala na Jean Charles Ahoua wanaoungana na kipa Ayoub Lakred, Che Fondoh Malone, Fabrice Ngoma, Freddy Michael na Willy Onana kukamilisha idadi ya 12.

SOMA NA HII  ROBERTINHO AWAPA NENO HILI MASTAA SIMBA