Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara amesema kuwa familia yake ilimzuia kukata rufaa kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS) baada ya kufungiwa na Kamati ya Maadili ya TFF kujihusisha na masuala ya soka kwa muda wa miaka miwili.
Manara amemaliza adhabu yake aliyofungiwa kujihusisha na mpira ndani na nje ya nchi. Manara alifungiwa miaka miwili pamoja na faini ya milioni 10 baada ya kukutwa na hatia ya kumkosea nidhamu Rais wa TFF, Wallace Karia.
Manara aliyekuwa ameambatana na familia yake kwenye kikao hicho amesema sambamba na kutumikia ‘kifungo cha soka’ cha miaka miwili pia amelipa faini ya shilingi milioni 10 za Tanzania iliyokuwa imeambatanishwa kama sehemu ya adhabu yake.
“Kwanza kabisa niwashukuru wote kwa kipindi cha miaka miwili niliyofungiwa, na kwa hili nipeleke shukrani zangu za dhati kwa familia yangu hususani mama yangu.
“Wakati nafungiwa kuna watu waliniambia nikate rufaa CAS lakini mama yangu akaniambia miaka miwili sio mingi nisikate rufaa na kweli miaka miwili imeisha na leo niko hapa kuzungumza na watu wa mpira,” amesema Manara.
Manara aliyekuwa ameambatana na familia yake kwenye kikao hicho amesema sambamba na kutumikia ‘kifungo cha soka’ cha miaka miwili pia amelipa faini ya shilingi milioni 10 za Tanzania iliyokuwa imeambatanishwa kama sehemu ya adhabu yake.
“Mkataba wangu na Yanga SC ulikuwa unaisha 2025, lakini GSM waliniita na kuniongeza mkataba mpya ambao unaisha 2026, nilishangaa maana nilikuwa sifanyi kazi. Lakini nimeongezwa mkataba na nimeongezewa mshahara. Namshukuru sana Ghalib, licha ya kufungiwa nilikuwa naendelea kulipwa mshahara,” amesema Manara.
Aidha, Manara amethibitisha rasmi kushiriki katika matukio yote ya Yanga ikiwemo uzinduzi wa jezi na siku ya Mwananchi.