Home Habari za Simba Leo USAJILI WA ATEBA NI KAMA MOVIE LA KUTISHA…ULIANZIA HUKU

USAJILI WA ATEBA NI KAMA MOVIE LA KUTISHA…ULIANZIA HUKU

Habari za Simba- Ateba Simba

Wakati mchakato wa kumsajili mshambuliaji mpya wa Simba, Christian Leonel Ateba Simba unaanza skauti wa Simba, Mels Daalder alimpendekeza mshambuliaji wa Red Arrows kutoka Zambia, Ricky Banda, ingawa mchambuzi wa video (video analyst), Mueez Kajee akaweka pingamizi akidai hawezi kuendana na mfumo wa Fadlu.

Baada ya hapo Fadlu akapewa jukumu na viongozi la kuchagua mshambuliaji anayemtaka alipendekeza majina matatu ambayo ni Leonel Ateba aliyekuwa USM Alger, Muethiopia Abubeker Nassir aliyepo Mamelodi Sundowns na Mrundi, Elvis Kamsoba.

Viongozi wa Simba baada ya kuwafuatilia nyota hao wakabaini urahisi zaidi ni wa kumpata mshambuliaji, Nassir kwa sababu hana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ambacho kimesheheni nyota wengi wakali.

Licha ya kuona urahisi huo, viongozi wa Simba wakamfanyia tathimini ya haraka mchezaji huyo na ndipo wakajiridhisha kwamba, Nassir ni mshambuliaji mzuri ila ana tatizo la kupata majeraha ya mara kwa mara, hivyo wakasitisha mpango naye.

Uchambuzi ukaendelea hadi kwa Mrundi, Elvis Kamsoba ambaye ni mchezaji huru kwa sasa baada ya kuachana na Perserikatan Sepakbola Sleman ya Indonesia huku akiwahi kuzichezea timu mbalimbali za Melbourne Victory FC na Sydney FC za Australia.

Uzoefu wa mchezaji huyo ukawavutia mabosi wa Simba ila mwishoni ukaachana naye baada ya kujiridhisha hana fitinesi ya kutosha na atakapotua nchini inabidi apewe programu maalamu ya wiki moja hadi mbili, jambo ambalo hawakukubaliana nalo.

Baada ya machaguo hayo ndipo ikafikia makubaliano na USM Alger ya kumpata Ateba Simba ambaye haikuwa rahisi pia japo kitendo cha mchezaji mwenyewe kuomba kuondoka ili akatafute changamoto sehemu nyingine kilirahisisha dili.

Sababu kubwa ya mchezaji huyo kuomba kuondoka ni kitendo cha kuchezeshwa winga na mara nyingine amekuwa akicheza namba 10, nyuma ya mshambuliaji raia wa Mali, Abdoulaye Kanu, jambo ambalo limemfanya Ateba kuomba kuondoka kikosini humo.

Ateba Simba alijiunga na USM Alger Januari mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon huku msimu uliopita nyota huyo alihusika katika jumla ya mabao tisa akiwa na timu hiyo, akifunga moja na kuasisti manane katika michezo 16.

Nyota huyo aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali za Coton Sport na PWD Bamenda, anakumbukwa zaidi mwaka 2023 ambapo ndiye alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Cameroon baada ya kufunga mabao 21, yaliyomfanya kuitwa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alithibitisha timu hiyo kushusha mshambuliaji mpya na licha ya kutotaka tu kuweka wazi ila Mwanaspoti linatambua nyota huyo ni Ateba, na muda wowote kuanzia sasa atatangazwa.

SOMA NA HII  SIMBA YAHAMIA KWA MNIGERIA...DILI LA MPANZU NGUMU KUMEZA