Home Habari za Simba Leo AWESU AWESU NA MASHAKA BALAA JINGINE SIMBA

AWESU AWESU NA MASHAKA BALAA JINGINE SIMBA

HABARI ZA SIMBA-AWESU

MABAO mawili ya wachezaji wapya, Valentino Mashaka na Awesu Awesu, pamoja na lingine lililofungwa na Fondoh Che Malone, yaliiwezesha Simba jana kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United, ikiendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi yoyote ya mzunguko wa kwanza kwa misimu 17.

Mara ya mwisho Simba kupoteza mechi ya kwanza ya Ligi Kuu, ilikuwa ni Septemba 23, 2007, Ligi Kuu msimu wa 2007/08, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ilipochapwa bao 1-0, dhidi ya Coastal Union likiwekwa wavuni na Sunday Peter.

Misimu yote 17 iliyosalia Simba haijawahi kupoteza zaidi ya kushinda na kutoka sare.

Beki wa kati raia wa Cameroon, ameingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao la msimu kwenye kikosi cha Simba, alipofanya hivyo dakika ya 13 ya mchezo huo uliopigwa, Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam.

Malone aliipatia Simba bao baada ya kuruka juu zaidi ya wachezaji wote na kuunganisha kwa kichwa mpira wa kona fupi iliyopigwa na Jean Charles Ahoua.

Bao hilo lilifungwa baada ya kona mbili kupigwa, ya kwanza ikipigwa na Balua, ikaokolewa na Salum Chukwu, ya pili ikipigwa na Joshua Mutale, ambaye alipiga fupi kwa Ahoua, aliyeuinua langoni na kumkuta mfungaji.

Tabora United walianza mechi kwa kuwaachia Simba, wao wakikaa nyuma ya mpira kwa muda mrefu huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza mara chache, na hata hivyo hayakuwapa tabu sana mabeki na kipa wake Moussa Camara.

Simba ingeweza kuandika bao dakika ya tano kupitia kwa Steven Mukwala, lakini aliunganisha vibaya krosi ya Edwin Balua.

Baada ya bao hilo, Simba iliendelea kulisakama lango la Tabora United, lakini tatizo sugu la ukosaji wa mabao liliendelea kuwaandama.

Kuna wakati wachezaji wenyewe kwa wenyewe walionekana kukosa mawasiliano, huku pia ikionekana kila mmoja anataka kufunga licha ya kuwa kwenye eneo gumu.

Shuti la Ahoua, liligonga mwamba dakika ya 25 alipounganisha krosi fupi kutoka kwa Mutale, ambaye dakika chache baadaye aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Awessu.

Kipindi cha pili, Kocha Mkuu, Fadlu Davis, alilazimika kufanya mabadiliko ya kuwatoa kwanza Ahoua, Mukwala, Mzamiru Yassin na Shomari Kapombe, nafasi zao zikachukuliwa na Valentino, Kibu Denis, Agustine Okejepha na Kelvin Kijili, mabadiliko ambayo yaliisaidia kupata mabao mawili kipindi hicho.

Alikuwa ni straika aliyesajiliwa kutoka Geita Gold, Valentino, aliyepachika bao la pili likifungwa mara nyingine kwa kichwa.

Aliruka juu kuunganisha krosi iliyopigwa na nahodha, Mohamed Hussein ‘Tshabalala.

Wakati kila mmoja akidhani mechi hiyo ingeisha kwa mabao 2-0, kiungo mshambuliaji aliyesajiliwa msimu huu kutoka KMC, Awessu, alipachika bao la tatu kwa mpira aliopiga kwa ufundi wa hali ya juu.

Akiwa pembeni kidogo ndani ya eneo la hatari, aliupiga mpira ambao ulionekana kama unaelekea nje, lakini ulikatika na kugonga nguzo ya chini upande wa kulia kwa kipa Haroun Mandanda na kujaa wavuni.

Msimu uliopita Simba ilichukua pointi zote sita kwa Tabora United, ikiifunga mabao 4-0, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Februari 6, na mechi ya mzunguko wa pili, ikashinda mabao 2-0, mchezo uliochezwa Mei 6, mwaka huu katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

SOMA NA HII  BALEKE AWEKA REKOD YA KIBABE BONGO...PHIRI TUMBO JOTO MSIMBAZI