Home Habari za Simba Leo SPIDERMAN CAMARA AMTISHIA DIARRA…MWENYEWE AFUNGUKA

SPIDERMAN CAMARA AMTISHIA DIARRA…MWENYEWE AFUNGUKA

habari za simba-camara

KIPA mpya wa Simba, Moussa Camara ameweka wazi malengo yake msimu huu na kutangaza vita dhidi ya Djigui Diarra wa Yanga na Lay Matampi kutoka Coastal Union.

Camara ambaye ametua Simba msimu huu akitokea Horoya AC ya Guinea na ndiye kipa aliyedaka mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Tabora United akitoka bila ya kuruhusu nyavu kutikiswa ikiwa ina maana kuwa tayari ana Clean Sheet ya kwanza.

Nyota huyo amekuwa na rekodi ya kuchukua Tuzo ya Kipa Bora mara mbili kwenye Ligi ya Guinea akiwa na Horoya, akiisaidia timu hiyo kuchukua  mataji manne ya Ligi, FA (3) na Super Cup (2).

Uwepo wa Camara akiwa kipa namba moja kwa sasa, unamaanisha kuwa timu tatu kubwa ndani ya ligi, Simba, Yanga na Azam zina makipa namba moja kutoka nje ya nchi kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Camara ambaye anatajwa kuwa mmoja wa makipa wa kisasa kutokana na uwezo wake wa juu wa kutumia miguu, alisema msimu huu anataka kuwa ndani ya makipa watatu bora kwenye Ligi ya Tanzania kwa kuwa anaamini kuhusu uwezo wake.

Aidha alieleza kuwa, anatambua kwenye ligi kuna makipa wengi bora akiwemo Diarra ambaye anamjua tangu akiwa kwao Guinea huku Matampi akimjua kwa mbali na ili awe bora ni lazima apambane na wazoefu hao kwenye ligi.

“Diarra, Matampi wote ni makipa wazuri lakini nataka kuwa na mwanzo mzuri ndani ya kikosi cha Simba na kuwa miongoni mwa makipa watakaokuwa wakiongoza kwenye chati Ligi Kuu Bara.

“Malengo yangu haya yanatokana na ubora wa kikosi chetu licha ya kwamba ni kipya, lakini naamini kadiri tunavyoendelea kuzoeana tutakuwa na timu nzuri huko mbele,” alisema Camara.

KUHUSU UKUTA WA SIMBA

Kipa huyo ambaye alisajiliwa na Simba baada ya uongozi wa timu hiyo kutoa taarifa za kuumia aliyekuwa kipa namba moja kikosini hapo, Ayoub Lakred, alisema: “Ukuta wetu nao ni sababu ya pili ambayo inanipa imani kwamba nitaweza kufikia malengo yangu ndani ya ligi na kikosi kwa ujumla kwa kuwa nimeshaona jinsi ambavyo tumekuwa na maelewano mazuri uwanjani.

“Lakini pia ili nitimize malengo hayo nataka kuendelea kupigania nafasi ndani ya Simba ambayo nayo ina makipa wenzangu bora wakiwemo mzoefu Aishi Manula, Hussein Abel na Ally Salim, wote hawa nawaheshimu kwa kuwa wameshafanya mambo makubwa sana wakiwa na Simba,” alisema Camara ambaye kwenye michezo mitatu ya mashindano aliyocheza amesharuhusu bao moja alilofungwa na Maxi Nzengeli kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

SOMA NA HII  DUCHU AOMBA KUONDOKA SIMBA...HAJASAFIRI NA TIMU