Saa chache baada ya kutemwa na Simba, mshambuliaji Freddy Michael amevunja ukimya na kufunguka akisema alichofanyiwa imekuwa ni kama sapraizi kwani alikuwa amejipanga kufanya makubwa baada ya kujipata mwishoni mwa msimu uliopita.
Pia mshambuliaji huyo wa zamani wa Green Eagles ya Zambia, amesema licha ya kuwaheshimu na kuwakubali mastraika wapya waliotua Msimbazi, lakini amewaponda kwamba hakuna yeyote wa kumfikia kwa kazi ya kufunga, hata kama alianza na mguu mbaya aliposajiliwa katika dirisha dogo la msimu uliopita.
Freddy alitua Msimbazi katika dirisha hilo akitokea Zambia alipoacha akiwa na mabao 11 katika mechi 17 za Ligi Kuu ya nchi hiyo, mbali na mabao mengine matatu ya michuano mingine na akiwa Simba aliifungua mabao sita ya ligi, mawili ya Kombe la Shirikisho na moja lile la Muungano.
Hata hivyo, licha ya kusaini mkataba wa miaka miwili, lakini nyota huyo raia wa Ivory Coast ametemwa pamoja na kuwa mmoja ya wachezaji walikuwapo katika kambi ya maandalizi ya msimu mpya (pre season) ili kumpisha nyota mpya kutoka USM Alger ya Algeria, Lionel Ateba kutokana na kanuni ya wachezaji 12 wa kigeni kwa kila klabu ndani ya msimu mmoja.
Akizungumza mara baada ya juzi kupewa ‘thank you’ na Simba, Freddy alisema amekubaliana na uamuzi, japo ameumizwa kwani alikuwa anaamini msimu huu angefanya vizuri zaidi baada ya kumaliza ligi akiwa hana rekodi mbaya.
Freddy alisema Ligi ya Bara isingemshinda kama angeaminiwa, kwa sababu alikuwa na malengo ya kupigania kiatu cha Mfungaji Bora msimu huu baada ya msimu uliopita kukwama.
“Imenishtua mno, kwani malengo niliyokuwa nayo msimu huu ilikuwa ni kufika mbali hata kubeba kiatu cha mfungaji bora, kwa vile nilishaizoea ligi ilivyo na hata namna ya kucheza. Nilihitaji mechi nyingi tu, kuonyesha kile nilichokuwa nacho kwa kuwa, sikuwa na kiwango kibaya msimu uliopita ndio maana nilimaliza na mabao mengi kuwazidi waliocheza kwa msimu mzima,” alisema Freddy na kuongeza:
“Nawaheshimu washambuliaji waliobaki Simba, lakini nilikuwa na uwezo wa kufanya kitu bora kuliko wao, najua kipaji changu na wenyewe mliona nilivyoizoea ligi.
Hata hivyo kwa sasa nasubiri kumalizana na timu moja ya Algeria kwenda kuendeleza ubora wangu huko.” Licha ya Freddy kutoweka wazi, lakini taarifa kwamba nyota huyo aliyenyakua tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi ya Zambia akiwa anakipiga Tanzania, yupo hatua za mwisho kumalizana na MC Alger ya Algeria iliyomnyakua Kipre Junior aliyekipigaAzam FC kwa misimu miwili iliyopita.
REKODI ZA WALIOBAKI
Steven Mukwala (24) kutoka Asante Kotoko ya Ghana, ni raia wa Uganda alisajiliwa hivi karibuni akiwa na rekodi ya kufunga mabao 14 na asisti mbili msimu uliopita, huku akiwa na sifa ya kufunga mabao ya aina zote.
Valentino Mashaka (20) kutoka Geita Gold, msimu uliopita alifunga mabao sita na kuasisti moja kupitia mechi 24 ikiwa ni sawa na dakika 1499, huku Lionel Ateba kutoka USM Alger ametua Msimbazi akitoka kufunga bao moja kutokana na kutopata nafasi ya kitumikia timu hiyo msimu uliopita.
Ateba alijiunga na USM Alger Januari, mwaka huu akitokea Dynamo Douala FC ya kwao Cameroon na msimu uliopita alihusika na mabao tisa akiwa na timu hiyo, akifunga moja na kuasisti manane katika michezo 16.