Rais wa Klabu ya Yanga, Eng. Hersi Said amesema kuwa kama kuna mtu ambaye mashabiki wanapaswa kumpongeza na kumuombea ni mfadhili wa Klabu hiyo, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ kwani amekuwa msaada mkubwa kwa mafanikio ya klabu ambayo imekuwa ikiyapata tangu aanze kuwapa fedha.
Hersi amesema kuwa badala ya kuwaponda wadhamini hao kwa kudhamini vilabu mbalimbali, wanapaswa kuwatia moyo na kuendelea kuwapokea kwani vilabu vyote vya soka nchini vinahitaji wadhamini, wawekezaji na wafadhili ili kujiendesha na kupata mafanikio, vinginevyo hakuna klabu hata moja kwa Tanzania ambayo inaweza kusimama na kujiendesha kwa pesa zake yenyewe.
“Tumekuwa na mahusiano mazuri ya wadhamini wetu ambao kila tunapowakimbilia wanatushika mkono, nichukue fursa hii kuwashukuru sana Kampuni ya SportPesa, Azam TV na GSM kwa kuwa na sisi katika kipindi chote cha Uongozi wangu.
“Kama kuna jambo ambalo Wanayanga wanapaswa kuliombea dua liendelee ni uwepo wa GSM kwenye timu yetu, amekuwa akitusapoti katika mambo mengi mno.
“Mfano juzi kwenye Ngao ya Jamii kabla ya kuwashughulikia watu fulani, alikuja na kutuuliza bajeti ya Bonasi ikoje, tulipomwambia akasema haitoshi, akaongeza fungu la maana vijana wakaenda kupambana tukashinda,” amesema Eng Hersi Said.