Home Habari za Yanga Leo SIRI YA USHINDI WA YANGA UGENINI IKO HAPA

SIRI YA USHINDI WA YANGA UGENINI IKO HAPA

HABARI ZA YANGA

Unaweza kusema Kocha Miguel Gamondi amekuja Yanga kwa ajili ya kufanya yasiyowezekana yawezekane kwani hadi sasa ameifanya timu hiyo kuwa tishio katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

Tangu msimu uliopita alipoanza kuifundisha Yanga akichukua mikoba ya Nasreddine Nabi, hadi sasa Wanayanga wanafurahia kile kinachofanywa na kocha huyo raia wa Argentina.

Msimu uliopita, Gamondi aliipeleka Yanga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita takribani miaka 25, hawakuishia hapo kwani walikwenda hadi robo fainali wakiondolewa na Mamelodi Sundowns kwa penalti 3-2 baada ya matokeo ya jumla kuwa 0-0.

Juzi Jumamosi pale Uwanja wa Abebe Bikila uliopo Addis Ababa, Erhiopia, Gamondi akiwa na vijana wake waliweka rekodi mpya.

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya CBE SA ni rekodi mpya kwa Yanga kwani imekuwa mara ya kwanza kupata ushindi nchini humo dhidi ya Wahabeshi.

Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935, kabla ya juzi ilikuwa imeenda Ethiopia mara nne kucheza na timu za nchi hiyo katika michuano ya CAF lakini haikuambulia ushindi zaidi ya sare mbili na vichapo viwili.

Bao la Prince Dube dakika ya 45+1 juzi lilivunja mwiko huo na kumfanya Gamondi kuiongoza Yanga kushinda nchini Ethiopia baada ya kupita takribani miaka 55.

Licha ya kwamba Yanga imeshinda mchezo huo na kuweka rekodi, lakini ni kama Wananchi hawakuridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yao kwani wamekosa nafasi nyingi za wazi kufunga mabao. Pengine kama zingetumiwa vizuri, wangerudi Dar na mtaji mkubwa sana wa mabao.

Ukiweka kando yote haya, hapa kuna uchambuzi wa mchezo huo na kinachofanywa na Yanga kabla ya kurudiana Jumamosi ya Septemba 21 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kuanzia saa 2:30 usiku.

CBE SIO WANYONGE

Yanga waliuanza mchezo kwa taratibu kitu ambacho kiliwafanya wenyeji CBE kutawala kwa kiasi kikubwa kipindi cha kwanza ingawa kipindi cha pili kulikuwa na mabadiliko kidogo kwa Yanga kushambulia sana.

Kama ilivyo kawaida ya timu za Ethiopia, CBE nayo ilicheza soka safi la kumiliki mpira muda mwingi na utulivu wa hali ya juu hata wakiwa kwenye boksi lao na kudhihirisha kwamba si timu ya kubezwa.

DUBE KAICHELEWESHA

Licha ya kwamba ndiye aliyefunga bao pekee, lakini Prince Dube haepuki lawama za kuchelewesha ushindi huo kwani kabla ya kufunga alikosa nafasi tatu za wazi.

Ya kwanza ilikuwa dakika ya tatu baada ya kuupokea mpira mrefu uliotoka kwa kipa Djigui Diarra, lakini uimara wa kipa wa CBE, Firew Getahun Alemayehu akazuia shambulio hilo ambalo Dube alikuwa akitazamana naye.

Baada ya hapo, Dube akapata nafasi nyingine dakika ya 12, krosi iliyopigwa kutokea upande wa kulia, ikamkuta akiwa ndani ya boksi la wapinzani kushoto kidogo, mpira aliupiga ukagonga nguzo ya pembeni kwa juu kidogo na kurudi uwanjani.

Haikuishia hapo, dakika ya 40, akiwa tena yeye na kipa, Dube alikosa kufunga jambo ambalo lilionekana kumkasirisha Kocha Gamondi.

Hata hivyo, baada ya majaribio hayo matatu kutoka kwa Dube, mshambuliaji huyo Mzimbabwe akafanikiwa kuuweka mpira kimiani muda mfupi kabla ya mapumziko.

Mbali na Dube, Maxi Nzengeli, Clatous Chama, Clement Mzize na Stephane Aziz Ki nao walikosa nafasi kadhaa za kufunga ambazo zilionekana kuwa ni za wazi.

Katika hilo, Kocha Gamondi anapaswa kulifanyia kazi ili mchezo wa marudiano au hata wakienda hatua ya makundi hawapaswi kuzichezea nafasi kama hizo kwani huwa hazitokei mara nyingi.

MBINU ZA GAMONDI

Bado Gamondi anadhihirisha ana kikosi ambacho anaweza kukitumia kwa mifumo zaidi ya moja.

Juzi aliamua kumuweka nje beki wa kulia, Yao Kouassi Attohoula ambaye ametoka kuuguza majeraha, kisha nafasi yake akamtumia Dickson Job mwenye uwezo pia wa kucheza beki wa kati.

Kumtumia Job upande wa kulia ilikuwa ni kama zuga kwani wakati timu ikipandisha mashambulizi, nyuma wanabaki mabeki watatu ambao ni Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca na wakishambuliwa anaongezeka Chadrack Boka anayecheza kushoto.

Mfumo huo ulikuwa ukimpa uhuru mkubwa Boka kusaidia mashambulizi kwani muda mwingi alikuwa juu wakati Yanga ikiwa na mpira. Mfumo kama huo Gamondi aliutumia mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar na kushinda 2-0.

MECHI 6, MABAO 18

Yanga imekamilika katika idara ya ushambuliaji na ulinzi kwani msimu huu hadi sasa katika mechi za kimashindano imeshuka dimbani mara sita na kufunga mabao 18, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja pekee.

Ushindi wa juzi ilikuwa ni clean sheet ya tano kwa Yanga msimu huu katika mechi sita ilizocheza mpaka sasa.

Katika michuano ya Ligi ya Mabingwa pekee, Yanga imefunga mabao 11 ikiwa haijaruhusu bao ikicheza mechi tatu, dhidi ya Vital’O mara mbili hatua ya awali ikishinda 4-0 na 6-0, kisha moja mtoano dhidi ya CBE SA iliposhinda 1-0.

Kabla ya hapo, ilicheza mechi mbili za Ngao ya Jamii ikianza nusu fainali dhidi ya Simba ikashinda 1-0 na fainali ikaichapa Azam 4-1. Pia mchezo mmoja wa Ligi Kuu Bara ilishinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.

KIWANGO DUNI

Kilichoonekana kwa Yanga ambacho mashabiki wengi wa timu hiyo walionekana kutoridhishwa nacho ni kiwango kilichooneshwa na wachezaji wa timu hiyo katika uchezaji wao.

Ukiachana na nafasi nyingi za wazi walizokosa, lakini pia timu ilionekana kucheza kawaida na hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji walioanza kutofanya maandalizi ya pamoja kwa muda mrefu.

Kikosi kilichoanza kilikuwa hivi; Djigui Diarra, Dickson Job, Chadrack Boka, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua.

Katika kikosi hicho, wachezaji nane waliungana na timu moja kwa moja nchini Ethiopia wakitokea kwenye majukumu ya timu zao za taifa ambao ni Diarra, Job, Mwamnyeto, Bacca, Aucho, Mudathir, Dube na Stephane Aziz Ki. Waliokuwa kwenye maandalizi siku zote ni Boka, Pacome na Maxi. Kumbuka Yanga ilifika Ethiopia Alhamisi, kisha Jumamosi ikacheza mechi, kwa maana hiyo timu ilifanya mazoezi ya pamoja siku mbili pekee kabla ya mechi.

WASHINDWE WENYEWE

Kazi kubwa waliyoifanya Yanga wakiwa Ethiopia kilichobaki washindwe wenyewe kufuzu hatua ya makundi.

Hiyo inatokana na rekodi ya Yanga kuwa nzuri dhidi ya timu za Ethiopia katika michuano ya CAF inapocheza nyumbani.

Rekodi zinonyesha, Yanga katika mechi nne dhidi ya Wahabeshi kwenye michuano ya CAF, imefanikiwa kuziondosha mara tatu na moja pekee ikiangukia pua.

Katika mechi zote hizo, Wahabeshi hawajawahi kushinda katika ardhi ya Tanzania dhidi ya Yanga.

Matokeo ya Yanga nyumbani dhidi ya Wahabeshi katika michuano ya CAF yapo hivi; Yanga 5-0 St. George, Yanga 6-1 Coffee, Yanga 4-4 Dedebit, Yanga 2-0 Welaita Dicha.

Licha ya kwamba Yanga ina rekodi nzuri dhidi ya Wahabeshi, lakini hawapaswi kuona kazi imeisha kwani kama wao waliweza kuvunja mwiko wakiwa Ethiopia, wakizubaa CBE nao wanaweza kuuvunja mwiko katika ardhi ya Tanzania na kutinga makundi.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUWATUNGUA SIMBA JANA....GAMONDI KAIBUKA NA HILI KWA YANGA....