WINGA wa JKT Tanzania, Shiza Kichuya amesema zama alizokuwa nazo za ubora kwa sasa zimeisha na anawaona Ladack Chasambi na Edwin Balua wanaokipiga Simba kuwa ndio wachezaji wazuri wanaoweza kurithi ufalme wake, iwapo tu kama watapata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwani wanajua.
Kichuya aliyewahi kutamba na Mtibwa Sugar, Simba na Namungo mbali na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, aliliambia Mwanaspoti kuwa haoni mabadiliko ya uchezaji alionao ndani ya JKT Tanzania huku akiweka wazi yeye sio mchezaji mzuri sana, ila alipata bahati ya kufanya matukio makubwa yaliyombeba.
Alisema kipindi anafanya makubwa hakuwahi kukubali kipaji alichonacho zaidi alikuwa anaona anafanya mambo makubwa, hivyo hawezi kusema ameshuka kiwango au la, lakini anaamini kila msimu kunaibuka vipaji vipya na kwa jicho lake amewaona mawinga wawili chipukizi walipo Simba.
“Msimu huu haraka haraka nimeona wameibuka kina Chasambi na Balua ambao wana vipaji vikubwa na makocha na wadau wa mpira wanaojua ndio wanaweza kutambua, ila wengine hawawezi kuona,” alisema Kichuya aliyewahi kuifunga Yanga mara tatu mfululizo likiwamo bao la mpira wa kona alioupiga na kwenda moka kwa moja wavuni hadi kuimbwa na wasanii wa Bongofleva wakimtaja kama ‘Kichuya kona’.
“Pia ili majina yao yakue wanatakiwa kufanya matukio makubwa ambayo yatawaweka midomoni mwa watu kama ilivyokuwa kwangu lakini kama wataendeleza vipaji vyao hivyo kwa timu waliyopo wanatakiwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.”
Kichuya alisema Chasambi hapewi tu nafasi lakini ni mchezaji mzuri ni mpambanaji lakini ametumia nafasi hiyo kusifu upambanaji wake akimtaka aendelee kupambana na kutumia nafasi anazopewa ili kujiweka kwenye nafasi.
“Kupata nafasi ya kucheza Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikiamini zaidi wachezaji wa kigeni anatakiwa kuongeza juhudi zaidi ili aendelee kuaminiwa hilo linawezekana,” alisema Kichuya na kuongeza;
“Chasambi pia bado ana nafasi, umri unamruhusu hapaswi kukata tamaa, akipambana anaweza kuingia kwenye mfumo na kufanya kile ambacho wengi wanakitarajia kutoka kwake.”
[…] ni jina kubwa kwenye anga ya michezo nchini kutokana na winga Shiza Ramadhan Kichuya ambaye kwasasa anakipiga JKT Tanzania kutambulika zaidi kwa jina hilo, lakini unaambiwa jina hilo […]
[…] ni jina kubwa kwenye anga ya michezo nchini kutokana na winga Shiza Ramadhan Kichuya ambaye kwasasa anakipiga JKT Tanzania kutambulika zaidi kwa jina hilo, lakini unaambiwa jina hilo […]