BEKI wa Simba, Shomari Kapombe amefunguka kuwa alipewa jukumu la kuhakikisha anafanikiwa kumzuia mshambuliaji wa Al Ahly Tripol, Cristovao Mabululu kutofanya mashambuliaji katika mchezo wa kuwania kufuzu makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.
Amesema alichokifanya Mabululu kumpa mkono ndani ya dakika 45 ya kipindi cha kwanza kilipotamatika ni kwa ajili ya kumpongeza kwa kazi aliyoifanya katika mchezo huo.
.
Jumapili ya Septemba 22, Simba walifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho baada ya kumuondoa mashindanoni Al Ahly Tripol katika Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa jumla ya mabao 3-1.
Kapombe amesema alipata mshtuko alipofuatwa na mshambuliaji huyo wakati wanaenda mapumziko lakini alipofika karibu alimpongeza na kuheshimu kile anachokionesha katika mchezo huo.
“Ni kweli alivyokuja kwangu sikuweza kuelewa kabisa hata meneja wa timu alishangaa na kila mmoja akihofia kutokana na presha ya ile mechi ilivyo lakini ilikuwa tofauti kabisa.
Ilikuwa jambo nzuri kwangu kupongezwa na mchezaji wa timu pinzani, sio mara ya kwanza lakini kwa kitendo cha Mabululu kunipongeza ndani ya dakika 45 ya kipindi cha kwanza kuwa ameheshimu kile nilichokuwa nafanya uwanjani,” amesema Kapombe.
Ameeleza kuwa alikuwa na jukumu kubwa sana la kucheza pembeni kumzuia mshambuliaji huyo kupita katika njia hali ambayo niliifanya kulingana na majukumu aliyopewa na kocha Fadlu Davids.
Ameongeza kuwa aliwahi kupongezwa na beki wa Al Ahly ya Misri,Ramy Rabia na kubadilishana jezi wakati dakika 90 zimetamatika tofauti na alichokifanya Mabululu ndani ya dakika 45 kipindi cha kwanza.