Home Habari za michezo ZILE SHOW ZA SIMBA YA FADLU NI LEO TENA …..

ZILE SHOW ZA SIMBA YA FADLU NI LEO TENA …..

HABARI ZA SIMBA-

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa wanatarajia kucheza mechi nyingine ya kirafiki leo Jumamosi ili kuzidi kukiimarisha kikosi chao kabla ya kukutana na Al Ahly Tripol ya Libya kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Wekundu hao wa Msimbazi walianza kucheza dhidi ya Al Hilal ya Sudan na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 huku bao la Mnyama likiwekwa wavuni na straika wao Lionel Ateba, kipute hicho kikipigwa dimba la KMC Complex.

Baada ya mchezo huo dhidi ya Al Hilal, Wekundu hao wa Msimbazi sasa wanajipanga kucheza dhidi ya maafande wa JKT Tanzania leo katika dimba la KMC Complex huku Kocha Mkuu wa kikosi hicho Fadlu Davids akitamba vijana wake kuonyesha soka la kitabuni.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally amesema, wanautumia muda huu Ligi ikiwa imesimama kupisha michuano ya Kimataifa kwa Timu za Taifa kuendelea kukinoa kikosi chao kuhakikisha kinafanya vizuri hasa Michuano ya Kombe la Shirikisho.

“Kwa sasa tunaendelea na program yetu ya mazoezi na tutakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki Jumamosi. Tumeendelea na program ya mazoezi kwa sababu timu yetu bado inahitaji muda mwingi zaidi kwani wachezaji wengi ni wapya.

“Tutacheza dhidi ya JKT Tanzania Jumamosi kesho (leo) katika Uwanja wa KMC Complex ikiwa ni maandalizi kuelekea mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Tripol ya Libya, wachezaji waliopo wanaendelea kujifua kwenye Uwanja wa mazoezi,” amesema Ahmed.

Akizungumzia hali ya kiafya ya wachezaji wao, Ahmed amesema mpaka sasa timu yao ipo vizuri ikiwa haina majeruhi zaidi ya kipa wao Ayoub Lakred ambaye atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiwaambia mashabiki kuendelea kuisapoti timu yao.

SOMA NA HII  WAKATI YANGA WAKITAMBA NA AZIZ KI WAO...SIMBA WAAMUA KUMSHUSHA MBABE WA MAYELE KIMYA KIMYA...