Home Taifa Stars MOROCO ALIVYOIPELEKA TANZANIA MOROCCO….RAIS SAMIA ‘AZIZIMA’ KWA MIL 700…

MOROCO ALIVYOIPELEKA TANZANIA MOROCCO….RAIS SAMIA ‘AZIZIMA’ KWA MIL 700…

Taifa Stars

BAO la dakika ya 60 lililofungwa na winga wa kimataifa, Simon Msuva, anayecheza soka la kulipwa Klabu ya Al Talaba ya Iraq, limeipeleka Tanzania fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Katika mchezo huo wa raundi ya sita hatua ya makundi, uliochezwa jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, dhidi ya Guinea, Msuva alipachika bao kwa kichwa na kuifanya Taifa Stars kutoka na ushindi wa bao 1-0, katika mchezo huo wa Kundi H.

Lilionekana shambulizi lisilo na madhara lililotengenezwa taratibu ukiguswa na wachezaji kadhaa wa Stars mpaka ndani eneo la hatari, ukamkuta Mudathir Yahaya akaunyanyua mpira juu na Msuva kuuzamisha mpira kimyani kwa kichwa.

Beki wa kati wa Guinea, Ibrahima Conte, alijitahidi kuruka juu kutaka kuokoa, lakini ulimzidi kimo, mbele ukatua kidogo usawa wa kichwa cha Msuva ambaye hakufanya ajizi, akajitwisha na mpira ukajaa wavuni, licha ya jitihada za kipa Moussa Camara anayeichezea Klabu ya Simba kutaka kuokoa.

Bao hilo liliamsha shangwe, hoihoi na nderemo kwa mashabiki wa soka waliokuwa uwanjani ambao walijazana kwa wingi kuangalia mchezo huo na kuipa nguvu Stars.

Ushindi huo unaifanya Stars kufuzu fainali hizo ikimaliza kwenye nafasi ya pili nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ikikusanya pointi 10, mabao matano, ikifungwa nanne, ikishinda michezo mitatu, sare moja na kupoteza miwili.

DR Congo imeshafuzu ikiwa na pointi 12, jana ikitarajia kucheza mchezo wake wa mwisho wa kumalizia dhidi ya Ethiopia.

Kipigo hicho kimeifanya Guinea kumaliza michezo sita ikiwa na pointi tisa, ikishika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo.

Timu mbili zitakazomaliza nafasi za juu katika makundi yote 12, yaliyopangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), zitafuzu fainali hizo, huku nyingine zikiwa tayari zimeshafuzu.

Hii ni mara ya nne kwa Stars kufuzu fainali hizo, mara ya kwanza ikiwa ni 1979, ambapo fainali zake zilipigwa nchini Nigeria mwaka 1980, mara ya pili ikiwa ni 2019, ambapo fainali zake zilichezwa nchini Misri na ya tatu ilikuwa 2023 ambapo fainali zake zilichezwa mwaka huu nchini Ivory Coast.

Katika mchezo huo wa jana, dakika ya kwanza tu, tayari Stars ilikuwa imeshafika langoni mwa Guinea kwa shambulizi lililofanywa na nahodha Mbwana Samatta, lakini kipa Camara akikaa imara la kuzima jaribio hilo.

Guinea ilijibu kwa shambulio hilo dakika moja baadaye kupitia kwa Sylla Morlaye, lakini mabeki wa Stars wakiongozwa na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ walikaa imara na kuokoa hatari.

Dakika ya nne, Stars ilirejea tena langoni mwa wageni wao, safari hii, Samatta alimpa pasi ya kurudisha Mudathir, nje kidogo ya eneo la hatari, alipiga shuti kali ambalo liliwababatiza mabeki wa Guinea na kuwa kona tasa.

Krosi ya Clement Mzize ilikosa muunganishaji dakika ya sita, na dakika ya 10, Msuva alikosa bao la wazi akiwa ameliangalia lango huku mashabiki na watu wa benchi la ufundi wakiwa tayari wamesimama kushangilia.

Ilikuwa ni krosi safi kutoka kwa Shomari Kapombe, iliyomkuta akiwa kwenye nafasi nzuri kabisa, lakini shuti lake lilikwenda pembeni kwa mshangao wa wengi akiwa hatua sita tu kutoka langoni.

Camara alilazimika kufanya kazi ya ziada dakika ya 15, kwa kuokoa krosi ya Kapombe iliyokuwa inakwenda kutua kwenye kichwa cha Samatta.

Mzize itabidi ajilaumu mwenyewe kwa kukosa mabao mawili ya wazi, dakika ya 27 na 33, huku baadaye akionekana kuumia na benchi la ufundi lilitaka kumtoa nafasi yake ichukuliwe na Kibu Denis, lakini alikataa kutoka. Pamoja na kukataa kutoka nje, alikosa tena bao la wazi dakika 40.

Hata hivyo, hakurejea tena kipindi cha pili nafasi yake ikachukuliwa na Kibu ambaye kwa kiasi kikubwa aliongeza uhai akisaidia ulinzi na kuanzisha mashambulizi mengi hadi ilipofika dakika iliyokuwa inasubiriwa na mamilioni ya Watanzania kuona Taifa Stars ikifuzu AFCON kwa mara ya nne.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Msuva ambaye hilo ni bao lake la 24 kuifungia Stars tangu aanze kuichezea, alisema analitoa zawadi bao hilo kuwafariji waathirika wote wa ajali ya kuangukiwa na ghorofa Kariakoo, lakini pia akimshukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwaunga mkono na kuwafanya mashabiki kuujaza uwanja kuwasapoti.

“Tulipanga kupambana na tumepambana mpaka mwisho, tunashukuru kupata bao hili,” alisema Msuva ambaye ni mfungaji namba mbili wa wakati wote Taifa Stars, akiwa nyuma ya Mrisho Ngassa mwenye mabao 25, huku wa tatu akiwa ni Mbwana Samatta na mabao yake 22.

Kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’, alisema: “Haikuwa kazi nyepesi, wachezaji walipambana sana, nashukuru tumefanikiwa”.

MIL 700 ZA SAMIA HIZI HAPA..

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa zawadi ya Sh Milioni 700 kwa timu ya Taifa (Taifa Stars), kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wageni wao Guinea, katika mchezo wa mwisho wa kuwania kufuzu fainali za AFCON mwaka 2025.

Katika mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Stars imeshinda bao 1-0 lililofungwa na Simon Msuva na kukata tiketi ya kufuzu fainali hizo mwaka 2025.

Akizungumza baada ya kukamilika kwa mchezo huo uliohudhuriwa maelfu ya mashabiki, Waziri wa Utamadunia Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro, amesema Rais Samia ametoa fedha hizo kama sehemu ya kupongeza mchango wa wachezaji na benchi lote la ufundi la Taifa Stars.

“Rais Samia anathamini kazi kubwa na mchango uliotelewa na wachezaji hao, hivyo ameamua kutoa kiasi hicho cha fedha kama zawadi ambapo tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya Wizara ya mchezo,”Amesema Ndumbaro.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndumbaro amesema wachezaji wa Taifa Stars wamealikwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baadaye mwezi Febuari, mwaka 2025.

SOMA NA HII  FT: TANZANIA 2-1 SOMALIA....SOPU AENDELEA KUITAKATISHA STARS...BADO UGANDA KISHA HAOOO CHAN KIULAIINI KABISA...