Home news BAADA YA KUWAONA WAKIKIWASHA JUZI…FADLU KASEMA HILI KUHUSU MANULA NA CAMARA…

BAADA YA KUWAONA WAKIKIWASHA JUZI…FADLU KASEMA HILI KUHUSU MANULA NA CAMARA…

Habari za Simba leo

BAADA ya makipa wa Simba, Aishi Manula na Moussa Camara kuuwasha moto katika mechi za kufuzu Afcon 2025, kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids amebainisha kuwa kuna kazi kubwa katika kuwania namba ndani ya timu hiyo.

Juzi Jumanne, Fadlu alikuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kushuhudia mchezo wa Kundi H la kuwania kufuzu Afcon 2025 ambako Taifa Stars iliifunga Guinea bao 1-0 na kufuzu. Katika mchezo huo, kipa wa Stars alikuwa Manula na yule wa Guinea ni Camara.

Licha ya Manula kutopata nafasi ya kutumika ndani ya kikosi cha Simba msimu huu katika mechi yoyote ya kimashindano, ameonyesha kiwango kizuri mechi mbili za mwisho za kufuzu Afcon dhidi ya Ethiopia na Guinea ambapo hajaruhusu bao.

Akizungumza Fadlu alisema, anafurahia kuona kiwango alichokionyesha Manula kwani ni wazi amerejea katika ubora wake. Alisema kuwa, kuruhusu bao kwa Camara ambaye kwa sasa ndiye anashika namba moja katika kikosi chake, hakutoi maana ya kwamba sio bora ila ni mbinu tu za Stars zilizomzidi kete.

“Kurejea kwa kiwango cha Manula kunakwenda kuongeza ushindani mkubwa ndani ya kikosi cha Simba kwani ameonyesha ukubwa wake katika mechi ngumu iliyokuwa imebeba hatma ya Stars kutinga Afcon.

“Nafahamu kuwa nina makipa wengi sana lakini ujio wangu uwanjani umeniongezea kitu cha kukifanyia kazi na nimeweza kuwasoma wachezaji wangu kwa upana zaidi,” alisema Fadlu na kuongeza.

“Camara alifanya kazi kubwa na nzuri kwani kama angekuwa na kiwango cha kawaida angefungwa zaidi ya bao moja, lakini Stars ilistahili kushinda kwani wachezaji wake walikuwa na kiwango bora, hivyo nawapongeza.”

Camara ndiye kipa namba moja wa Simba msimu huu akisimama langoni katika mechi zote 14 za kimashindano ambazo timu hiyo imecheza, Ligi Kuu Bara (10), Ngao ya Jamii (2) na Kombe la Shirikisho Afrika (2) huku akiwa kinara wa clean sheet katika Ligi Kuu ambapo anazo nane.

Kwa upande wa Manula ambaye alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akiuguza majeraha, msimu huu amecheza mechi moja pekee ya kirafiki kwa dakika 45 dhidi ya Al Hilal iliyofanyika Agosti 31 mwaka huu.

Kwa upande wa kufuzu Afcon 2025, Manula amecheza mechi mbili za mwisho ambazo zote hajaruhusu bao dhidi ya Ethiopia na Guinea, wakati Camara akicheza mechi nne kati ya sita, akiruhusu mabao mawili katika mechi mbili dhidi ya Ethiopia na Tanzania, huku akipata clean sheet mbili dhidi ya Ethiopia na DR Congo.

Manula pia amecheza mechi mbili za kufuzu CHAN ambapo Taifa Stars ilifungwa 1-0 dhidi ya Sudan na ya marudiano ikashinda 1-0 dhidi ya Sudan na hivyo kuamuliwa kwa penalti ambazo Tanzania ililala 6-5 na kung’oka.

Mbali na wawili hao, ndani ya Simba eneo la kipa kuna Ally Salim ambaye alicheza mechi nne za kufuzu Afcon 2025 akiondoka na clean sheet moja dhidi ya Ethiopia, huku akiruhusu mabao manne — moja dhidi ya Guinea na matatu mbele ya DR Congo.

Ayoub Lakred naye amerejea kutoka kwenye majeraha, huku Hussein Abel na Ahmed Feruzi wakihitimisha idadi ya makipa watano ndani ya kikosi cha Simba.

Hivi karibuni, Fadlu alizungumzia kurejea kwa Ayoub akisema amemuona kipa huyo mazoezini akifanya vizuri, lakini ni mapema sana kuizungumzia nafasi yake kikosini kwa sababu anahitaji muda zaidi wa kumuangalia baada ya kupona.

Wakati huohuo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi chao kinaendelea na maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji utakaochezwa kesho Ijumaa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

“Kikosi kwa sasa kinaendelea na programu ya mazoezi kikijiandaa na mchezo dhidi ya Pamba. Leo (jana) usiku tutaondoka kwenda Mwanza, wachezaji wanne waliokuwa Taifa Stars na Camara aliyekuwa timu ya taifa ya Guinea wameshajiunga na kambi. Steven Mukwala atawasili Dar kesho (leo) alfajiri na kuunganisha kwenda Mwanza.”

“Mchezo dhidi ya Pamba ni muhimu mno kushinda kwa sababu utatupa ujasiri kuelekea mchezo dhidi ya Bravos. Nichukue nafasi hii kuwaambia mashabiki wetu wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwamba waingalie Pamba kama mpinzani wetu mgumu kwa maana hiyo wafanye maandalizi makubwa ya kwenda kumuangamiza Pamba. Tunahitaji ushindi huo.

“Hakuna uzalendo kwa watu wa Mwanza kwenye mchezo huo, tusiposhinda itakuwa faida kwa watu wengine. Tusimame kwanza na Simba na uzalendo utarudi baada ya kushinda. Hata uwe nani simama na Simba yako, hii vita sio ya Pamba wao wametumwa tu,” alisema Ally na kuongeza. “Baada ya mchezo dhidi ya Pamba usiku huohuo wa Ijumaa tutarudi Dar kuendelea na maandalizi ya mwisho kuivaa Bravos.”

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  ISHU YA MANZOKI KULETWA KWENYE UCHAGUZI WA SIMBA...UKWELI HALISI HUU HAPA...