Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA KESHO NA WAANGOLA….FADLU ALIMALIZA KILA KITU KWA PAMBA….

KUELEKEA MECHI YA KESHO NA WAANGOLA….FADLU ALIMALIZA KILA KITU KWA PAMBA….

Habari za Simba- Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa juzi kati ya timu yake dhidi ya Pamba Jiji na kushinda bao 1-0, Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, imempa mwanga na mbinu za kuwaangamiza wapinzani wao, Bravos do Maquis kutoka Angola.

Simba itawaalika Bravos do Maquis katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Fadlu alisema aliihitaji mechi hiyo kwa malengo ya kujiimarisha kuelekea mechi hiyo ya kimataifa na kile ambacho alikitaka amekipata na sasa akili yake iko tayari kuwavaa Waangola.

“Ilikuwa lazima tucheze mchezo huu, ulikuwa muhimu mno kwa ajili ya kuweka vyema wachezaji kwa ajili mechi yetu ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos do Maquis.

Aina ya mchezo ulivyochezwa, ushindani ulioonyeshwa na Pamba Jiji nilikuwa nauhitaji sana kwa sababu nilitaka wachezaji wangu wawe tayari, miili yao iwe timamu kwa ajili ya mchezo huo, na imekuwa kama nilivyojitaji. Tofauti na kama usingekuwepo kwa sababu baadhi ya wachezaji ukiacha waliokwenda kwenye vikosi vya timu za taifa, walikuwa wamepumzika bila miili yao kuwa na utayari wa mchezo,” alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema kwa sasa miili ya wachezaji wote imekaa vyema kwa ajili ya kuusubiri mchezo huo wa kwanza wa hatua ya makundi.

“Nimefarijika, nimeona wapi nitaanzia na kuishia kwenye mchezo ujao, ndiyo maana ndani ya dakika 55 za mchezo, tayari nilikuwa nimeshafanya mabadiliko mara nne, baadhi ya wachezaji nilikuwa nawahifadhi kwa ajili ya mchezo huo, wengine wameshapata utimamu kwa mwili walikotoka katika timu za taifa,” Fadlu alisema.

Kuhusu mchezo huo, alisema haukuwa wa kuonyesha ufundi zaidi ya kuwaweka fiti nyota wake na kusaka pointi tatu muhimu za Ligi Kuu.

“Najivunia vijana wangu kwa kuwa tayari kupambana, tulicheza mchezo huu kwenye uwanja ambao haukuwa rafiki kwa wachezaji, uwanja ambao nyasi zilikuwa zimeliwa, matope na ulikuwa unateleza, wachezaji wangu hawakuonekana kuwa tayari kucheza kwenye hali hii ya hewa, hawakuwa na spidi, hawakuonyesha ufundi, wakati mwingine unacheza mechi kwa ajili ya kushinda, siyo mpira mzuri,” alisema kocha huyo.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ili wajionee soka safi na ushindi pia.

“Hatutacheza hivi Jumatano, ikumbukwe tunacheza Benjamin Mkapa, tutacheza na timu ngumu lakini yenye kuonyesha ufundi, na sisi tutaonyesha ufundi,” aliongeza Fadlu.

Naye Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fred Minziro, alisema waliingia kwa kuiheshimu Simba, lakini kipindi cha pili waliamua ‘kujilipua’ kwa kushambulia zaidi.

“Tuliiheshimu Simba, tuliingia kwa kutengeneza mfumo wetu wenyewe kulingana na Simba ilivyo, kipindi cha kwanza hatukuwa vizuri, lakini cha pili tuliikamata mechi kwa sababu nilibadilisha mfumo na kucheza na mastraika watatu ili tushambulie zaidi, kama kutufunga mengine wacha tu watufunge, nashangaa mwamuzi kuongeza dakika mbili, kwa jinsi ilivyokuwa ilibidi ziongwezwe hata dakika 10,” alisema Minziro.

Bao pekee la penalti iliyopigwa na Leonel Ateba, liliwapa ushindi Simba ambayo inaendelea kukaa kileleni na pointi 28 kibindoni, ikishuka dimbani michezo 11 huku Pamba Jiji ikisalia nafasi ya 15 na pointi nane, wamecheza mechi 12.

Ligi Kuu Bara inatarajia kuendelea tena leo kwa JKT Tanzania kuwakaribisha Tanzania Prisons wakati Tabora United itawaalika Singida Black Stars huku KMC FC itawafuata Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma.

SOMA NA HII  ZORAN MAKI KULISUKA BENCHI LA UFUNDI SIMBA KIULAYA ULAYA...AKUBALIWA OMBI LAKE LA KULETA MAKOCHA WAARABU...