Home Habari za michezo IBENGE:- KWA YANGA HII…MHHHH !!!!!

IBENGE:- KWA YANGA HII…MHHHH !!!!!

Habari za Yanga SC

Kocha Mkuu wa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amesema, kitendo cha kupangwa kundi moja na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, kitaleta ushindani zaidi baina ya miamba hiyo kwa kuwa kikosi cha Miguel Gamondi kimekamilika kila idara.

Al Hilal imepangwa kundi ‘A’ katika hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ikiwa sambamba na timu za Yanga ya Tanzania, TP Mazembe ya DR Congo iliyochukua taji la mashindano hayo mara tano na MC Alger kutokea Algeria.

Akizungumza nasi Ibenge ambaye ni mmoja wa makocha wenye heshima kubwa kwenye soka la Afrika alisema, Yanga ni moja ya timu nzuri na bora katika hatua hii na kitendo cha kukutana nayo ni wazi itakuwa mechi ya ushindani, huku akieleza kuna mabadiliko makubwa tofauti na mara ya mwisho walipokutana kwenye michuano hii.

“Yanga ya sasa hivi huwezi kuiweka sawa na ile ya mara ya mwisho tuliyocheza nayo hii ya sasa ni bora sana, kuna ongezeko la wachezaji bora na wazoefu katika kila eneo, natarajia mchezo baina yetu utakuwa mgumu sana, hivyo jambo kubwa ni maandalizi tu ndiyo yanaweza kutupa matokeo mazuri,” alisema Ibenge Mkongomani aliyewahi kutakiwa na Simba, Yanga kwa nyakati tofauti bila mafanikio.

Ibenge ambaye alitwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na Berkane aliongeza, licha ya kuzisoma vyema timu za hapa Tanzania mara kwa mara anapokuja kuweka kambi ila haitokuwa ni rahisi kwao, huku akiweka wazi hakuna mchezaji tishio Yanga kwani wote ni hatari kutokana na aina yao ya uchezaji wao.

“Siwezi kuelezea mchezaji mmoja mmoja ila ninachotambua Yanga imekamilika kila eneo, huwezi kucheza kwa kumuangalia huyu na yule isipokuwa unapambana kuangalia ni jinsi gani utaweza kuizuia timu mzima isikuletee hatari katika eneo lako la mwisho kwa kuwa wana kikosi bora.”

Yanga ambayo ni timu tishio barani Afrika kwa sasa itaanza kampeni zake katika hatua hiyo ya makundi kwa kucheza na Al Hilal Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ukiwa ni mchezo wa kisasi kwani mabingwa hao wa Tanzania walitolewa na Wasudani hao msimu wa 2022-2023.

Katika msimu huo wa 2022-2023, timu hizo zilikutana katika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kusaka tiketi ya kutinga makundi ambapo mechi ya kwanza iliyopigwa Benjamin Mkapa Oktoba 8, 2022 timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Mchezo wa marudiano uliopigwa Oktoba 16, 2022, kwenye Uwanja wa Al-Hilal jijini Omdurman, Yanga ikachapwa bao 1-0, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 na ndipo msimu huo iliangukia Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kufika hadi fainali.

Msimu huo ambao Yanga ilifika fainali ilicheza na USM Alger ya Algeria ambapo mechi ya kwanza Dar es Salaam ilipoteza kwa mabao 2-1, Mei 28, 2023, kisha marudiano ikashinda 1-0, Juni 3, 2023 na kukosa ubingwa kwa faida ya bao la ugenini.

Yanga imetinga makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo kwa rekodi ya aina yake baada ya kufuzu kwa jumla ya mabao 17, kwani katika mechi za raundi ya awali iliweza kuiondosha Vital’O kutoka Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.

Baada ya Yanga kufuzu hatua ya hiyo ya awali, ikakutana na CBE SA ya Ethiopia ambapo mechi yake ya kwanza ikiwa ugenini ilishinda bao 1-0, huku mchezo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar ilishinda mabao 6-0.

Kwa upande wa Al Hilal ambayo ilianzia pia hatua za awali kama Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, michezo yake yote imecheza kwenye nchi mbili tofauti ingawa kwa sasa imeweka kambi Mauritania ambapo ndipo inashiriki Ligi Kuu.

Al Hilal ambayo inacheza Ligi Kuu ya Mauritania kutokana na changamoto za kiusalama nchini kwao, hatua ya awali iliiondosha Al Ahly Benghazi ya Libya kwa jumla ya mabao 2-1, kisha raundi ya kwanza ikaitoa San Pedro ya Ivory Coast kwa jumla ya mabao 3-2.

SOMA NA HII  KUELEKEA MSIMU UJAO...MANARA AFUNGUKA YANGA WATAKAVYOITIKISA AFRIKA...ATAJA MASTAA WAPYA WATAKAO SHUKA...