Home Yanga SC KAZE ANOGESHA SHANGWE LA UBINGWA YANGA

KAZE ANOGESHA SHANGWE LA UBINGWA YANGA


KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Cedric Kaze amenogesha shangwe la ubingwa kwa mastaa wa  kikosi hicho baada ya kuwapa mapumziko kamili bila programu yoyote ya mazoezi ili mastaa hao wapate muda wa kukaa na familia zao kabla ya kurejea tena kambini Januari 25.

Yanga Januari 13, mwaka huu ilimaliza ukame wa muda mrefu wa kutotwaa mataji baada ya kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa michuano ya kombe la Mapinduzi baada ya kuwachapa Simba kwa changamoto ya mikwaju ya Penalti 4-3.

Kocha huyo amewapa mastaa wake mapumziko mpaka Januari 25 ili kuwapa muda wa kutosha kwa mastaa hao kupumzika kwa ajili ya kuwa tayari kwa michezo ya mzunguko wa pili. 

Akizungumzia mapumziko hayo Meneja wa kikosi cha Yanga, Hafidh Saleh amesema: “Baada ya kazi kubwa ya kutwaa ubingwa wa michuano ya kombe la Mapinduzi, kocha Kaze amewapa mapumziko ya muda nyota wote wa kikosi chetu ili waende kujumuika na familia zao mpaka tarehe 25 ambapo wanatarajiwa kurejea tena kambini. 

“Kocha ameamua kuwapa wachezaji likizo isiyokuwa na program yoyote ya mazoezi ili kuwapa muda wa kutosha nyota hao kupumzika baada ya kazi kubwa waliyoifanya kwenye ligi na kombe la Mapinduzi,”

Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 44 baada ya kucheza michezo 18, hawajapoteza mchezo wowote mpaka sasa.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUONGOZA LIGI....NABI AWACHANA MASTAA YANGA...ADAI WANAPAPARA...