Home Habari za michezo KUELEKEA DIRISHA DOGO….HIVI HAPA VYUMA 3 VIPYA ANAVYOTAKA GAMONDI …KIBWANA MHH..

KUELEKEA DIRISHA DOGO….HIVI HAPA VYUMA 3 VIPYA ANAVYOTAKA GAMONDI …KIBWANA MHH..

Habari za Yanga leo

WAKATI kikosi chake kesho usiku kitashuka kucheza mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Chamazi Complex ,Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ameanza kupiga hesabu za kuongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuhitaji kusajili wachezaji watatu wapya.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema, Gamondi amepeleka maombi kwa uongozi wa klabu hiyo akipendekeza anataka kufanyika kwa mchakato wa kusajili nyota watatu wakati dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa ili kukiimarisha kikosi chake.

Chanzo chetu kilisema Gamondi amebaini kikosi chake kina mapungufu katika nafasi ya beki wa kulia, winga na mshambuliaji wa kati.

“Kocha Gamondi ameona kuna haja ya kukiongezea nguvu kikosi chetu, kuna mapendekezo amewapa viongozi ili wakati wa dirisha dogo wasajiliwe wachezaji watatu, na ameainisha maeneo ya kufanyiwa kazi, lengo anahitaji kupata mafanikio zaidi kwenye mashindano ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika,” kilisema chanzo chetu.

Kiliongeza kocha anatambua ushindani uliopo katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa wanayoshiriki, hivyo lazima anahitaji kukiimarisha zaidi kikosi chake.

“Uongozi umeanza kufanyia kazi mapendekezo ya kocha, mambo yanafanywa chini kwa chini na ikifika dirisha dogo kila kitu kitakuwa wazi, wachezaji wanaofuatiliwa sasa watajulikana hapo baadaye muda rasmi ukifika,” kiliongeza chanzo chetu.

Kilisema Gamondi anataka kuongeza nguvu katika eneo ushambuliaji ambalo kwa sasa straika, Clement Mzize, amekuwa akipata nafasi mara kwa mara pamoja na Mzambia Kennedy Musonda huku upande wa beki ya kulia, amekuwa zaidi akimtumia, Yao Kwasi.

“Kuna wakati mwalimu amekuwa akimpa nafasi Shomari Kibwana, lakini ameona inafaa kuwaongezea nguvu katika maeneo hayo,” alisema.

Mapema wiki hii straika, Kelvin Nashon alitajwa kukamilisha mazungumzo ya kujiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars lakinio nyota huyo ameweka wazi bado hajafanya mazungumo yoyote na mabingwa hao watetezi.

Yanga pia inahitaji kujiimarisha ili kufanya vyema katika mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Yanga imepangwa Kundi A pamoja na Al Hilal ya Sudan, TP Mazembe (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DR Congo) na MC Alger ya Algeria.

SOMA NA HII  YANGA WATUA MTWARA KWA NDEGE