BAADA ya kuwasili salama nchini Algeria, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema hali ya hewa ya baridi kali si tatizo kwa wachezaji wake ambao wamekwenda kuivaa CS Constantine katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa keshokutwa.
Mechi hiyo kati ya CS Constantine na Simba itachezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka katika mji wa Constantine, Fadlu, alisema wamewasili salama huku wachezaji wake wakiwa katika hali nzuri licha ya kukutana na hali hiyo ya baridi kali.
“Tupo vizuri, nadhani leo (jana), saa tisa (sawa na saa 11 jioni kwa Tanzania), kwa saa za huku tutafanya mazoezi yetu ya kwanza, naamini kwa siku hizi mbili wachezaji watazoea hali ya hewa ya hapa,” alisema Fadlu.
Kocha huyo alisema mazoezi waliyofanya jana na ya mwisho yatakayofanyika leo yatampa picha kamili ya kikosi chake kuelekea mchezo huo wa pili wa hatua ya makundi.
“Baada ya mazoezi ya leo (jana) tutafanya tena mazoezi kwenye uwanja rasmi ambao tutakaotumia kucheza mechi, hayo yatakuwa mazoezi muhimu sana kwetu kuelekea siku ya mchezo, kwa sasa nafurahia hali ya wachezaji wangu, kila mmoja na anautamani mchezo huu,” alisema Fadlu.
Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, aliliambia Nipashe kutoka nchini humo, safari yao ilikuwa nzuri na hawajakutana na changamoto ya aina yoyote.
“Tunashukuru tumefika salama ingawa tuliingia usiku, Kocha Fadlu ameandaa programu yake ya mazoezi ambayo itaanza leo (jana) saa tisa, kila kitu kipo salama kabisa, Wana-Simba wasiwe na wasiwasi,” alisema Ahmed.
Aliongeza kwa kuwataka mashabiki na wanachama wa timu hiyo waendelee kuiombea dua njema timu yao ifanye vizuri katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.
Mchezo huo unatarajia kutoa kinara wa kundi hilo kutokana na timu zote kupata pointi tatu katika mechi iliyopita, Simba ikiwafunga Bravos do Maquis ya Angola bao 1-0 na CS Sfaxien ya Tunisia ikivuna ushindi kama huo dhidi ya CS Constantine.
Katika mechi hiyo, Simba itamkosa kipa wake mzoefu, Aishi Manula, ambaye aliugua ghafla la kulazimika kubakia nchini.
Makipa wawili waliosafiri katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi ni Moussa Camara, raia wa Guinea na Mtanzania Ally Salim.