Home Habari za michezo MIAKA 10 YA ZIMBWE Jr NDANI YA SIMBA SC….HIVI NDIVYO ALIVYOANZA NA...

MIAKA 10 YA ZIMBWE Jr NDANI YA SIMBA SC….HIVI NDIVYO ALIVYOANZA NA ANAVYOENDELEA….

Habari za Simba leo

JUNI 23, 2014, mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe (sasa marehemu), alitangaza kumsainisha nyota wa miaka 18 kutoka Kagera Sugar, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Nyota huyo ‘mtoto wa Magomeni’, alisaini mkataba wa miaka mitatu ambao ulitakiwa kuwa hai kuanzia Julai mosi mwaka huo. Kutoka tarehe hiyo hadi leo Desemba 10, 2024 ni miaka kumi, miezi mitano na siku tisa. Au miezi mia moja ishirini na siku tisa, au majuma 545, au siku 3815 za kalenda.

Mohamed Hussein alisaini Simba SC wakati Rais wa nchi akiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akaja John Joseph Pombe Magufuli, na sasa Samia Suluhu Hassan.

Mohamed Hussein alisaini Simba SC iliyomaliza ligi katika nafasi ya nne, nyuma ya mabingwa Azam FC, Yanga SC na Mbeya City FC.

Mohamed Hussein alisaini Simba SC jezi yake ikiandikwa ‘Tshabalala’, sasa ni Zimbwe Jr.

Mambo mengi yametokea ndani ya hii miaka kumi ya Mohamed Hussein na Simba SC, ndani na nje ya klabu yake.

WACHEZAJI ALIOSAJILIWA NAO

Simba SC ilimaliza msimu wa 2013/14 katika nafasi ya nne na kufanya msimu huo kuwa mbaya zaidi kwao tangu mwaka 2000, walipomaliza katika nafasi kama hiyo, nyuma ya mabingwa Mtibwa Sugar, Yanga na Kajumulo World Soccer.

Simba walijipanga kurudisha makali yao kwa kuhakikisha wanafanya maboresho ya kikosi chao.

Walianza kwa kuwapa mkono wa kwaheri wachezaji saba ili kupisha maingizo mapya.

Wachezaji walioondoka walikuwa Ramadhan Seleman Chombo ‘Redondo’, aliyetimkia Villa Squad ya Magomeni. Mrundi Gilbert Kaze aliyetimkia Vital’O ya nchini kwao. Kigi Makasi aliyetimkia Ndanda SC. Edward Christopher Shija aliyetimkia Polisi Dodoma. Henry Joseph Shindika aliyemtikia Mtibwa Sugar na Donald Musoti aliyetimkia Tusker ya Kenya.

Halafu wakaanza kushusha vyuma kuziba nafasi hizi. Mchezaji wa kwanza kabisa kusainiwa alikuwa Joram Mgeveke, kijana wa miaka 22 aliyenaswa kutokea timu ya taifa ya Tanzania, lakini akiitumikia klabu ya Lipuli ya Iringa iliyokuwa madaraja ya chini kabisa.

Kisha akafuata Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kijana wa miaka 18 aliyefanya vizuri sana msimu wa 2013/14 akiwa na Kagera Sugar.

Usajili mpya wa Simba kwa ajili ya msimu wa 2014/15 ulikuwa kama ifuatavyo:

Joram Mgeveke kutoka Lipuli FC

Mohamed Hussein kutoka Kagera Sugar

Abdi Banda (Tanzania) kutoka Coastal Union

Murshid Juuko (Uganda) kutoka Victoria Uni.

Mwinyi Kazimoto (Tanzania) kutoka Al Markhiya ya Qatar

Shaaban Kisiga (Tanzania) kutoka Mtibwa Sugar

Pierre Kwizera (Burundi) kutoka klabu ya AFAD ya Ivory Coast

Elias Maguri (Tanzania) kutoka klabu ya Ruvu Shooting

Ibrahim Hajibu Migomba (Tanzania) kutoka Akademi aliyekuwa kwa mkopo Mwadui FC

Emmanuel Okwi (Uganda) kutoka Yanga

Jerry Santo (Kenya) kutoka klabu ya Coastal Union

Raphael Mungai (Kenya) kutoka klabu ya KCB

Paul Kiongera kutoka KCB ya Kenya.

Usajili huu ukaleta matumaini makubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo na ikasubiriwa siku ya utambulisho wa wachezaji hawa, Simba Day.

Lakini bahati mbaya kwao, Simba wakapoteza 3-0 mbele ya Zesco ya Zambia na kutoa ishara mbaya ya msimu uliokuwa mbele yao.

Kujibu mapigo, mabosi wa klabu wakamtimua kocha mkuu kumuondoka kocha mkuu Zdravko Logarusic kutoka Croatia na kumleta mzambia Patrick Phiri. Seleman Matola, nahodha wa zamani wa klabu hiyo, akaendelea kuwa kocha msaidizi.

MAKOCHA WALIOMFUNDISHA

Habari za Simba leoMohamed Hussein aliingia moja kwa moja kwenye kikosi, akichukua nafasi ya majeruhi Rashid Issa ‘Baba Ubaya’ katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu, dhidi ya Coastal Union.

Mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Mkapa), Septemba 21, 2014, haukuwa mzuri sana kwa Zimbwe Jr.

Hadi mapumziko timu yake ilikuwa inaongoza 2-0 kwa mabao ya Shaaban Kisiga dakika ya sita na Amissi Tambwe dakika ya 36.

Coastal Union walirudi kwa kasi ya ajabu kipindi cha pili na kusawazisha mabao yote mawili. Bao la kwanza lilifungwa na Mganda Lutimba Yayo Kato dakika ya 69.

Ni bao la pili ndilo lililokuwa na kumbukumbu mbaya kwa Mohamed Hussein kwani katika dakika ya 83 aliunawa mpira nje kidogo ya kisanduku cha hatari.

Mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Mkenya Rama Salim wa Coastal dakika jiooni ukazaa bao la pili na la kusawazisha kwa Coastal Union, na kuwaacha Simba SC vichwa chini, lakini zaidi Mohamed Hussein mwenyewe.

Sare hiyo ni kama ilifungulia milango ya sare nyingine tano mfululizo kabla Simba haijashinda mechi ya kwanza ya msimu katika mzunguko wa saba, dhidi ya Ruvu Shooting.

Hata hivyo, Desemba 26, 2024 Simba SC ikapoteaa mchezo uliofuata dhidi ya Kagera Sugar, kwa bao moja kwa bila, jwenye Uwanja wa Taifa.

Huu ulikuwa mwanzo mbaya zaidi kwa Wekundu wa Msimbazi, ndani ya karne ya 21.

Desemba 29, 2014 mabosi wa klabu hiyo wakaitisha kikao cha dharura kilichofanyika kwenye hoteli ya Double Tree Masaki jijini Dar es Salaam, na kufikia uamuzi wa kumfukuza kocha Patrick Phiri na msaidizi wake Seleman Matola, ambaye alikuwapo tangu utawala wa kocha aliyepita, Zdravko Logarusic.

Uamuzi huu ulitangazwa Desemba 30, na siku moja baadaye yaani Desemba 31, akawasili kocha mpya Goran Kapunovic, raia wa Serbia aliyekuwa akiifundisha Polisi ya Rwanda.

Ndani ya miezi minne, Tshabalala akawa tayari ameshafanya kazi na makocha watatu, Logarusic, Phiri na sasa Kopunovic.

Hadi sasa akiwa katika mwaka wake wa 10, Mohamed Hussein amefundishwa na makocha:

1. Zdravko Logarusic – 2013-2014

2. Patrick Phiri – 2014

3. Goran Kopunovic – 2014-2015

4. Dylan Kerr – 2015-2016

5. Jackson Mayanja (wa mpito) 2016

6. Joseph Omog – 2016-2017

7. Pierre Lechantre – 2017-2018

8. Patrick Aussems – 2018-2019

9. Sven Vandenbroeck – 2019-2021

10. Didier Gomes De Rosa – 2021

11 Zoran Manojlovic – 2022

12. Juma Mgunda (wa mpito) 2022

13. Roberto Oliveira Goncalves do Carmo – 2023

14. Abdelhak Benchikha – 2023/24

15. Juma Mgunda – 2024

16. Fadlu Davids – 2024

MATAJI ALIYOSHINDA

Habari za MichezoJanuari 2015 Simba ilishinda Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa penalti 4-3 kufuatia sare tasa ndani ya dakika 90.

Kombe hili lilikuwa la kwanza kwa klabu hiyo tangu washinde Ligi Kuu msimu wa 2011/12, msimu ambao Tshabalala aliondoka akademi ya Azam FC na baadaye kujiunga na Kagera Sugar.

Kombe hili likafungua milango ya makombe mengine 11 yaliyofuata baada ya hapo:

Kombe la Mapinduzi – 2015

Kombe la Shirikisho la Azam Sports – 2017

Ngao ya Jamii – 2017

Ligi Kuu – 2017/18

Ngao ya Jamii – 2018

Ligi Kuu – 2018/19

Ngao ya Jamii – 2019

Ligi Kuu – 2019/20

Kombe la Shirikisho la Azam Sports – 2020

Ngao ya Jamii – 2020

Ligi Kuu – 2020/21

Kombe la Shirikisho la Azam Sports – 2021

KIMATAIFA

Ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports mwaka 2017 ukairudisha Simba SC kimataifa kupitia Kombe la Shirikisho la CAF.

Hata hivyo, klabu hiyo ikashindwa kufuzu hatua ya makundi baada ya kutolewa kwa sharia ya bao la ugenini na Al Masry ya Misri.

Hii ilifuatia sare ya 2-2 nyumbani na 0-0 ugenini.

Msimu wa 2018/19 Simba ikashiriki Ligi ya Mabingwa na kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2003.

Zaidi ya hatua ya makundi, Simba ilisonga mbele hadi kufika robo fainali ya kwanza kwenye mashindano hayo tangu 1994 ilipotolewa na Nkana Red Devils (sasa Nkana FC) ya Zambia.

Mafanikio ya Mohamed Hussein kimataifa:

Kombe la Shirikisho 2017 – 16 bora

Ligi ya Mabingwa 2018/19 – robo fainali

Ligi ya Mabingwa 2019/20 – 16 bora

Ligi ya Mabingwa 2020/21 – robo fainali

Ligi ya Mabingwa 2021/22 – 16 bora

Kombe la Shirikisho 2021/22 – robo fainali

Ligi ya Mabingwa 2022/23 – robo fainali

African Football League – 2023 – nusu fainali

Ligi ya Mabingwa 2023/24 – robo fainali

Kombe la Shirikisho 2024/25 – hatua ya makundi

BINAFSI

Habari za SimbaMsimu wa 2016/17, Mohamed Hussein alishinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu akiwa amecheza mechi zote 30 za Ligi Kuu Bara msimu huo.

Na sasa yeye ndiye nahodha wa klabu hiyo kongwe, akirithi usinga kutoka kwa John Rafael Bocco, aliyetimkia JKT Tanzania msimu huu.

Hiyo ndiyo miaka 10 ya Mohamed Hussein Zimbwe Jr ndani ya Simba SC, ambaye juzi alifunga bao pekee kule Algeria wakati Simba ikilala 2-1 dhidi ya St Constantine katika mechi ya Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika 2024-25.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  SIMBA YAANZA KUZITAFUTA 5-0 ZINGINE KWA AJILI YA SINGIDA BIG STARS...