Home Habari za michezo KUHUSU KIWANGO WA MAVAMBO …FADLU AVUNJA UKIMYA SIMBA…ATAJA KINACHOMFELISHA…

KUHUSU KIWANGO WA MAVAMBO …FADLU AVUNJA UKIMYA SIMBA…ATAJA KINACHOMFELISHA…

Habari za Simba- Mavamo

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaahidi wanachama na mashabiki wa timu hiyo ushindi Jumapili dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, huku wapinzani wao hao wakiwasili nchini mapema tayari kwa mchezo huo.

Akizungumza jana alfajiri wakati kikosi cha timu hiyo kikiwasili nchini kutoka Algeria kilipocheza mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine katika Uwanja wa Mohamed Hamlaoui na kufungwa mabao 2-1 Jumapili iliyopita, kocha huyo alisema anawaahidi wanachama na mashabiki wa Simba si ushindi tu peke yake bali na soka safi.

“Nawaahidi wanachama na mashabiki wa Simba ushindi na soka safi, waje kwa wingi Benjamin Mkapa Jumapili, najua wakijaa pale uwanjani huwapa hamasa wachezaji kufanya vizuri, mechi tuliyopoteza ugenini mmeona hata ninyi tumepoteza kwa bahati mbaya, lakini tunaahidi kufanya vema mchezo ujao,” alisema kocha huyo.

Akizungumzia mechi iliyopita na makosa yaliyofanywa na mabeki wa timu yake, alisema binadamu hujifunza kutokana na makosa, na anadhani wachezaji wake wameshaona madhara na hawatakiwi kuyafanya tena.

“Tulikuwa na kiwango kizuri kwa kipindi chote cha dakika 45, hatukuwa vema dakika tano za kwanza kipindi cha pili, tukaruhusu mabao yaliyoamua mchezo, lakini baada ya hapo, tulirejea mchezoni, imetuhuzunisha sana kupoteza mchezo, ila imetufunza kuwa kwenye michezo ya kimataifa makosa madogo madogo, yanaweza kusababisha madhara, hivyo hatutakiwi kuyafanya, na sisi inabidi tuyatumie kama wapinzani wetu wakiyafanya.

“Kwa bahati nzuri tuna mchezo mwingine nyumbani dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia, tunaweza kusawazisha makosa yote kwenye mchezo huo,” alisema kocha huyo.

Kocha huyo alisema sababu ya kumweka nje, Debora Fernandes Mavambo, kwenye mchezo huo na kumuingiza kipindi cha pili, ni kutokana na ushindani wa namba kikosini, huku wachezaji kama Augustine Okejepha na Fabrice Ngoma wakionesha kiwango kizuri kwa siku za karibuni, hivyo hakuona vibaya kuwatumia na kumpumzisha Mavambo ili aingie kipindi cha pili.

“Okejepha yupo kwenye kiwango cha juu, Ngoma pia, hii ni nzuri kwenye kuleta ushindani na kuwania namba, ndiyo maana nilimweka nje ili aje kusaidia kipindi cha pili, ukweli kila kitu kilikwenda sahihi, ni makosa tu yaliyojitokeza tukaruhusu mabao rahisi ndiyo yaliyoharibu kila kitu,” alisema Fadlu.

Wakati huo huo, wapinzani wa Simba, CS Sfaxien, walitua nchini jana wakitokea nchini Angola ambako Jumapili iliyopita walicheza mchezo wa Kombe la Shirikisho Kundi A, na kuchapwa mabao 3-2 dhidi ya Bravo do Maquis ya nchini humo.

CS Sfaxien imetua mapema, ambapo taarifa zinaeleza sababu za kijiografia ndizo zimesababisha kuwasili mapema, kwani isingewezekana kutoka Angola kurudi Tunisia na kuja nchini, huku zingine zikieleza wamewahi kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya Dar es Salaam ambayo ni joto, kabla ya mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Simba.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo umetangaza viingilio vya mchezo huo kuwa ni Sh. 3,000 kwa mzunguko, Sh. 5,000 rangi ya machungwa, Sh. 10,000 VIP C, Sh. 20,000 VIP B, Sh. 30,000 VIP A na Sh. 150,000 kwa upande wa Platinum huku Tanzanite ikiwa ni Sh. 200,000.

SOMA NA HII  REKODI YA MNIGERIA WA SIMBA IPO HIVI