Home Habari za michezo SIKU CHACHE BAADA YA KIPIGO CHA WAARABU…FADLU ATAJA WALIOIFELISHA SIMBA….

SIKU CHACHE BAADA YA KIPIGO CHA WAARABU…FADLU ATAJA WALIOIFELISHA SIMBA….

Habari za Simba leo

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amefunguka kuwa kichosababisha timu yake kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya CS Constantine ya Algeria ni makosa madogo kwenye eneo la ulinzi, pamoja na wachezaji kutofuata maelekezo yake aliyowapa watakapoingia kipindi cha pili.

Simba ilipoteza mechi hiyo ya raundi ya pili, Kombe la Shirikisho hatua ya makundi iliyochezwa, Uwanja wa Mohamed Hamlaoi jijini Constantine kwa mabao ya kujifunga ya Abdulrazack Hamza dakika ya 46 na Brahim Dib dakika ya 50, ambapo kabla ilipata bao la kuongoza dakika ya 24, lililowekwa wavuni na Mohamed Hussein ‘Tshabalala.’

Fadlu alisema katika mechi ya juzi ilipaswa kumalizika kwa Simba kushinda au pengine sare kama walinzi wake wasingefanya makosa na kutofuata maelekezo dakika za mwanzo za kipindi cha pili.

“Mechi ilikuwa nzuri, ilipaswa kuisha kwa ushindi au pengine sare, tumepoteza mchezo kwa makosa madogo ya eneo la ulinzi, magoli yote ya wapinzani yalikuwa mepesi ya yanayozuilika, naamini wachezaji wangu wataendelea kujifunza na nina imani wataimarika,” alisema kocha huyo.

Alisema katika dakika zote 90, wapinzani wao hawakutengeneza hatari yoyote kwenye lango lao, badala yake walikuwa wanategemea mipira iliyokufa na kona tu.

“Costantine hawajatengeza nafasi yoyote ya hatari dhidi yetu, tuliimiliki mechi kwa kiasi kikubwa, wao walikuwa wazuri kwenye mipira iliyokufa na niliwaambia wachezaji wangu kwenye dakika tano za mwanzo kipindi cha pili hatupaswi kuruhusu kona wala faulo, lakini hawakufanya hivyo na ndicho kilichotokea,” alisema.

Kipigo hicho kinaifanya Simba kushika ya tatu kwenye msimamo wa Kundi A, CS Constantine ikiongoza ikiwa na pointi sita, Bravo do Maquis ya Angola, baada juzi kuifunga CS Sfaxien ya Tunisia mabao 3-2 inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu kama Simba, lakini iko juu kwa kufunga mabao matatu, huku Watunisia wakiburuza mkia wakiwa hawana pointi.

Simba itashuka tena dimbani Jumapili ijayo, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kuwakaribisha waburuza mkia wa kundi hilo, CS Sfaxien.

Meneja Habari na Mawasiliano, Simba, Ahmed Ally, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kusahau matokeo ya juzi, badala yake kujiandaa kuujaza uwanja kwa ajili ya kusaka ushindi wa pili nyumbani, baada ya ule wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya Bravo do Maquis.

“Matokeo si mazuri, lakini haina athari yoyote katika kampeni yetu ya kuvuka hatua ya makundi, msingi katika michezo hii ya Afrika ni kwamba kila mmoja lazima ashinde nyumbani kwake, kushinda ugenini inakuwa kama ni bonasi kama siku hiyo utakuwa upo vizuri.

“Tulikuwa kwenye ubora wetu wa hali ya juu, tungeweza kushinda na tulistahili kwa aina ya mpira ambao tumecheza, lakini makosa tuliyoyafanya wapinzani wetu wakatuadhibu, pamoja na kupoteza, lengo letu lipo pale pale ni lazima kuchukua pointi tisa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Hii tunaiacha, akili yetu sasa ni mchezo wa Jumapili ijayo dhidi ya CS Sfaxien, nichukue fursa hii kuwambia wanachama na mashabiki wa Simba kuwa wasiwaze tena kuhusu mchezo huu, maandalizi yaanze sasa kujiandaa na mchezo huo,” alisema.

Kikosi cha Simba kilitarajia kuwasili alfajiri ya leo, na kinatarajiwa kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa na mchezo wa Jumapili.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA JUMAMOSI DHIDI YA UGANDA...TAIFA STARS WAAPA KUIWAFANYIA UMAFIA 'THE CRANES'...MIKAKATI IKO HIVI...