Home Habari za michezo BANGALA…KUTOKA UFALME YANGA MPAKA KUFUKUZWA AZAM FC…SABABU HIZI HAPA…

BANGALA…KUTOKA UFALME YANGA MPAKA KUFUKUZWA AZAM FC…SABABU HIZI HAPA…

MZEE wa kazi chafu. Yannick Bangala. Jina alipewa na rafiki yetu, Baraka Mpenja. Namna gani maisha yalivyookwenda kasi kwake. Hauwezi kuamini. Najaribu kumtazama kwa karibu. Juzi tu mkataba wake na Azam umesitishwa.

Aliibadili Yanga alipoingia na Khalid Aucho. Wakaichukua timu kutoka katika mikono ya Mukoko Tonombe na Zawadi Mauya. Kiungo cha Yanga kikaenda juu zaidi. Kitu cha kufurahisha ni namna alivyomudu nafasi mbili kwa ufasaha.

Ungempenda kama kiungo na ungempenda kama beki wa kati. Katika msimu wake wa kwanza tu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu. Katika dunia ya leo iliyotawaliwa na mambo ya takwimu Bangala hakuwa amefunga bao wala kupiga pasi za mwisho, lakini watu walikubaliana alistahili kuwa mchezaji bora wa msimu.

Ni kwa sababu ya namna alivyokuwa anacheza kwa uhakika kama kiungo wa chini. Jina la Mzee wa kazi chafu alilopewa na Mpenja likaanza kuambatana na jina la MVP. Hata hivyo, msimu wake wa pili alianza kuonekana kuwa mchezaji wa kawaida.

Nini kilimtokea msimu wake wa pili, licha ya kwamba Yanga walishamuongezea mkataba? Akaanza kuwa mchezaji wa kawaida. Taarifa za ndani zinadai alikuwa na mambo mengi ya nje ya uwanja ambayo watu wa ndani wa Yanga walidai alikuwa anawahujumu.

Habari za Yanga SCMwisho wa msimu yeye na Djuma Shaban wakaachwa. Yeye alikuwa na mkataba mkononi na Yanga walitumia nafasi kupata kiasi cha Sh100 milioni kutoka kwa Azam. Kuondoka kwake kuliwashangaza wengi. Ni kwa sababu tu mashabiki wa Yanga walimuamini Injinia Hersi Said na maamuzi yake, lakini ni namna gani ungeweza kuachana na Wacongo hawa. Djuma na Bangala.

Kuanzia hapo Bangala hakufuatiliwa sana na mashabiki kwa sababu anacheza Azam. Nilikuwa namuona anapambana uwanjani na jezi ya Azam, lakini wakati huu mkataba wake ukiwa umebakiza miezi sita Azam na yeye wamekubaliana kusitisha mkataba.

Kisa cha kwanza naambiwa Azam wanadai wana wachezaji wengi wa nafasi mbili ambazo Bangala anacheza uwanjani. Kuanzia katika ulinzi hadi katika kiungo. Hapo hapo wanataka kumrudisha Alassane Diao ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha huku wakitaka kusajili mchezaji mwingine wa kigeni katika timu.

Namna ambavyo maisha yamekwenda katika soka. Misimu mitatu iliyopita ungeweza kudhani Bangala angeweza kutua Azam, halafu baada ya msimu mmoja akawa mchezaji wa kupisha nafasi ya mchezaji Habari za Michezo leomwingine?

Kwamba pale katikati Azam wameona ni bora wabaki kina Sos Bajana na wamemtoa kafara Bangala? Kabla hata ya hapo habari za ndani ni Bangala mwenyewe alikuwa analalamika kutopata nafasi kubwa ya kucheza kikosini.

Sasa tumeuona mwisho wake Azam. Hali hii inasababishwa na nini? Nadhani wakati mwingine huwa tunawapokea wachezaji wakati wakiwa wanaelekea mwishoni. Aprili mwakani Bangala atakuwa anatimiza miaka 31 kwa mujibu wa ule ukurasa wake wa pasipoti. Kama anasema kweli basi alipaswa kuwa wa moto katika umri huu wa miaka 30 ambao anao.

Kuna mambo mawili hapa. Kukatishwa kwa mkataba wa Bangala, Azam kunaweza kuthibitisha labda Injinia Hersi ana jicho tofauti na sisi wengine linapokuja suala la kuwatazama wachezaji. Aliwaacha Bangala na Djuma katika nyakati ambazo tuliamini hakupaswa kuwaacha.

Baada ya hapo Djuma akajishikiza Azam kwa ajili ya kusubiri jina lake liongezwe katika usajili baadae, lakini Azam wakachezwa na machale na kuamua kuachana naye. Akaenda zake Namungo. Hii simulizi ya Djuma nayo inashangaza. Namna Yanga walivyoteseka kumpata kutoka Vita, lakini sasa ameangukia Namungo.

Lakini kwa Bangala nahisi kinatokea kitu kile kile. Muda si mrefu anaweza kuanza kuzurura katika hizi timu zetu. Baada ya mkataba wake kukata roho Azam, atakwenda nje au atabakia nchini? Nahisi anaweza kubakia nchini. Kuna raha yake kuishi Tanzania.

Wachezaji wengi wa kigeni wanapenda kuishi hapa. Watazame kina Obrey Chirwa na wengineo. Wanazurura tu nchini kwa sababu hii ni nchi tamu kuishi. Wapo Heritier Makambo na rafiki yake Yacouba Songne. Wapo pale Tabora. Usingetazamia siku moja wangekuwa Tabora.

yannickLakini vile vile rafiki yangu Bangala kama hawezi kupata timu Afrika Kaskazini anaweza kupata timu wapi? Tanzania imekuwa ikitoa mishahara mizuri kwa wachezaji wa kigeni. Hizi timu zetu tusizichukulie poa. Zimekuwa zikitoa mishahara mizuri kwa wachezaji wake na ndiyo maana wengi wapo hapa.

Muda si mrefu unaweza kusikia Bangala ametua zake Singida Black Stars au Namungo. Ni miezi 72 tu iliyopita alikuwa MVP na usingewaza anaweza kupanda basi kwenda zake Singida au Ruangwa Lindi. Hata hivyo, maisha ya soka Tanzania huwa yanakwenda kasi.

Kitu ambacho wachezaji wa kigeni huwa wanachelewa kujua ni namna ya kujitunza katika hizi timu mbili kubwa za Kariakoo. Wakati wanacheza wakiwa katika ubora wao huwa wanaanza kuzichukulia poa lakini mambo yakiharibika wanajikuta wameangukia kusikojulikana. Ni kama rafiki yetu, Bernard Morrison ambaye alizichukulia poa, lakini kwa sasa ni wazi anajuta.

Hizi timu usizichukulie poa sana. Wakati unachezea unapaswa kuziheshimu na kufanya kazi yako kwa ufasaha. Kuna wakati unajikuta mfalme, lakini ghafla unaweza kujikuta ukiwa katika basi la Namungo ukienda kucheza pambano la Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union pale Tanga. Namna maisha yalivyokwenda kasi kwa Bangala ni funzo kidogo kwa wengine.

NT:-Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la MwanaSpoti.

SOMA NA HII  JAMA JAMA HII YANGA YA INJINI HERSI NI MWISHO WA NJAA KWA KWELI....MADILI YA UDHAMINI YAZIDI KUMIMINIKA...