Home Habari za michezo HUU HAPA ‘UBAYA UBWELA’ ULIVYOIBEBA SIMBA JANA…

HUU HAPA ‘UBAYA UBWELA’ ULIVYOIBEBA SIMBA JANA…

Habari za Simba leo

BAO la dakika za majeruhi lililofungwa na kiungo mshambuaji raia wa Ivory Coast, Jean Ahoua, jana liliipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, katika mchezo mkali wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Wakati baadhi ya watazamaji wakiwa wameanza kuondoka, wengine wakiamini mchezo huo ungeisha kwa suluhu, yalitokea makosa mawili kwa wakati mmoja ndani ya eneo la hatari la JKT Tanzania na mwamuzi wa mchezo huo kuamuru mkwaju wa penalti uliokwenda kukwamishwa wavuni na kiungo huyo na kufikisha idadi ya mabao saba mpaka sasa kwenye Ligi Kuu.

Wakati Edson Katanga akionekana kuushika mpira kwenye eneo la hatari, wakati huo, Mohamed Bakari alimzuia kwa kutumia mikono Shomari Kapombe ambaye alikuwa anaifuata krosi iliyopigwa upande wa kushoto wakati wachezaji wa Simba walipokuwa wakifanya mashambulizi mfululizo langoni mwa wapinzani wao kwa dakika 10 za mwisho.

Bakari alizawadiwa kadi ya njano kwa faulo hiyo, lakini kwa sababu alikuwa ameshapewa kadi ya njano awali, akaonyeshwa tena nyekundu.

Ushindi wa jana ni wa nane mfululizo kwa timu hiyo kwenye Ligi Kuu, tangu ilipofungwa na Yanga bao 1-0, Oktoba 19 mwaka huu.

kwa sasa Simba wamefikisha pointi 37 na kuzidi kujichimbia juu ya kilele cha msimamo wa ligi ikiwa imeshacheza michezo 14 na kusalia mchezo mmoja kumaliza mzunguko wa kwanza.

Katika mechi ya jana haikuwa rahisi kwa Simba kufanya kama inavyofanya siku zote, kwani ilikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao walioonekana kuziba mianya yote na kushambulia kwa kushtukiza.

Mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, kwa kuwaingiza Josehua Mutale, Mohamed Hussein Tshabalala, Jean Ahoua na Steven Mukwala, yalionekana kuipa Simba uhai na kushambulia kwa kasi tofauti na mwanzo.

Ahoua kwa kiasi kikubwa alionekana kubadilisha zaidi mchezo kwani alionekana hatari zaidi kila anaposhika mpira, akishambulia kwa kasi, mashuti makali na pasi zake za hatari.

Hata hivyo, golikipa wa JKT Tanzania, Yakoub Selemani ndiye alikuwa shujaa kwa timu hiyo kwani aliokoa michomo mingi ya hatari langoni mwake.

Leonel Ateba ndiye aliyekosa mabao mengi kipindi cha kwanza katika mchezo wa jana.

Simba ilianza kuwashambulia maafande kwa faulo ya dakika ya saba iliyopigwa na Valentine Nouma karibu kabisa na lango la JKT Tanzania, mpira uliwababatiza mabeki na kuzua kizaazaa langoni huku wachezaji wa Simba wakichelewa kuukwamisha wavuni.

Simba ilifanya shambulio lingine dakika ya 16, pale krosi ya Elie Mpanzu ilipopanguliwa na kipa, Yakoub.

Dakika moja baadaye kipa huyo alifanya kazi ya ziada, aliporuka juu na kuupiga ngumi mpira wa kichwa uliopigwa na Leonel Ateba, akiunganisha krosi kutoka kwa Nouma hata hivyo mpira ulitoka nje na kuwa kona ambayo haikuwa na madhara.

JKT Tanzania ilipiga hodi kwenye lango la Simba dakika ya 21, pale Hassan Kapalata alipopata mpira akiwa pembeni kidogo ya lango, shuti lake kali lililoka sentimeta chache langoni.

Ateba aliruka ‘tik-tak’ dakika ya 22, kuunganisha krosi ya Kapombe, lakini aliukosa mpira na kuokolewa kwenye eneo la hatari.

Hassan Nassor, nusura aipatie JKT Tanzania bao dakika ya 28, alipounganisha kwa kichwa faulo iliyopigwa na Shiza Kichuya, akiwa hajawekewa ulinzi na mabeki wa Simba, bahati mbaya ukatoka nje kidogo la lango.

Mpanzu alilitia msukosuko lango la JKT Tanzania dakika ya 39, baada ya faulo aliyopiga kuvuka ukuta, lakini kipa Yakoub ambaye alifanya kazi kubwa jana, aliruka upande wake wa kulia na kupangua mpira kwa ustadi mkubwa.

SOMA NA HII  KISA CHAMA..YANGA NA SIMBA WAMEANZA UPYAA...SIMBA WAVAMIA TFF..WATUA NA FAILI ZITO..