Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA TP MAZEMBE….HIZI HAPA DK 270 ZA YANGA KUSUKA AU...

KUELEKEA MECHI NA TP MAZEMBE….HIZI HAPA DK 270 ZA YANGA KUSUKA AU KUNYOA CAF…

Habari za Yanga leo

YANGA inafahamu kuwa ina dakika 270 sawa na mechi tatu ili kuamua hatma ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Ili hilo litimie, kazi kubwa iliyopo ni kuhakikisha mchezo wa Jumamosi, wiki hii dhidi ya TP Mazembe ni lazima kushinda ili kufikisha pointi nne ambazo zitazidi kuipandisha juu kutoka ilipo.

Hiyo inatokana na iwapo Yanga itapoteza mchezo huo utakaochezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, basi suala la kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu litakuwa finyu. Katika Kundi A wakati Yanga ikiwa na pointi moja mkiani, TP Mazembe inazo mbili, Al Hilal inaongoza na pointi tisa ikifuatiwa na MC Alger (4).

Yanga ikiwa na hesabu za kuichapa TP Mazembe kufufua zaidi matumaini, wapinzani wao nao pia wana hesabu hizo kwani wakiimaliza Yanga, vita yao kubwa itakuwa na timu moja pekee – MC Alger kutokana na Al Hilal kubakisha hatua chache kufuzu robo fainali.

Wanaingiaje katika mchezo huo?

Ili kuhakikisha malengo na mikakati inatimia, Yanga imeamua kuingia katika mchezo dhidi ya TP Mazembe na mambo makuu mawili.

Jambo la kwanza ambalo Yanga wameliona linaweza kuwafanya kucheza mechi hiyo vizuri na kushinda ni kuwaondolea presha wachezaji wao ambayo ilionekana kuwatesa baadhi akiwemo Prince Dube ambaye hivi sasa anaonekana ameanza kujipata.

Katika kuondoa presha hiyo, Yanga imetangaza ule utaratibu wa kumpa mechi mchezaji, haupo na badala yake wameirudisha kwa mashabiki ambao wanaweza kuwapa hamasa wachezaji kuipigania nenmbo yao.

Kuhusu hilo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema jana : “Mechi hii hatujampa mchezaji yeyote bali tumeichukua wenyewe Wanayanga kwani ni yetu sote kwa sababu tukianguka tumeanguka wote.”

Uamuzi huo umetafsiriwa ni kuwashushia mzigo wachezaji wasicheze kwa presha kubwa hasa wale wanaopewa mechi hizo kama ilivyokuwa dhidi ya Al Hilal ambayo ilikuwa maalum kwa Prince Dube.

Dube alipewa mechi hiyo kutokana na kucheza muda mrefu mechi za ligi bila ya kufunga huku ikionekana anakwenda kujisafisha na kuanza kufunga, lakini ikawa tofauti na matokeo yake Yanga ikachapwa nyumbani mabao 2-0.

Ikumbukwe kwamba, mechi za Yanga kimataifa msimu uliopita zile za nyumbani zilipewa majina ya wachezaji tofauti kama Maxi Day (vs ASAS Djibout), Pacome Day (vs CR Belouizdad), Aziz Ki Day (vs Al-Merrikh) ambapo nyota hao walifanya makubwa ikiwemo kufunga na kutengeneza mabao kusaidia timu zao kuondoka na ushindi lakini ilivyokuwa tofauti kwa Dube imeonekana alicheza kwa presha ili kufanya kama wenzake.

Lakini pia waliwahi kumpa mfadhili wao, GSM mechi dhidi ya Medeama, huku pia mara moja mechi ya ligi msimu uliopita dhidi ya Dodoma Jiji, ilikuwa maalum kwa aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Miguel Gamondi na kuitwa Gamond Day.

Ukiachana na ishu hiyo, jambo la pili Yanga wameliweka mezani kwao kwenda kuikabili TP Mazembe ni kuichukulia mechi hiyo kama fainali kwao huku wakisisitiza ndiyo imeshikilia hatma yao ya kufuzu robo fainali.

Kuanzia viongozi hadi wachezaji wanalifahamu hilo kwani kiungo wa timu hiyo, Pacome Zouzoua, amesema mchezo dhidi ya TP Mazembe wataucheza kwa sura mbili, kufa au kupona kwani ndiyo umeshikilia hatma yao.

Pacome aliongeza kwamba wanafahamu wamebakiwa na mechi tatu ambazo ni fainali wakianza na TP Mazembe, kisha Al Hilal na mwisho dhidi ya MC Alger hivyo wamejiandaa na hilo.

“Kwa namna soka tunalocheza huku morali ikiwa juu lazima tukafanye uamuzi mzito mbele ya Mazembe. Haitakuwa mechi rahisi lakini kikosi chetu kina sura ya kupigania ushindi kwa kuwa kuna mwanga unaonekana,” alisema Pacome.

Wakati Pacome akisema hayo, mshambuliaji Clement Mzize, amesema: “Hatujaanza vizuri lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri, timu chini ya kocha Sead Ramovic ilikuwa inajitafuta, tayari wachezaji tumeanza kuzoea mfumo wake tutaendelea tulipoishia kwenye ligi ili tuendane na kasi ya Ligi ya Mabingwa.

“Tutaingia kwa kumuheshimu mpinzani wetu bila kujali ubora tulionao sasa kwenye ligi kwani ni michuano miwili tofauti, natamani kuwa mmoja wa wachezaji watakaokuwa bora kwenye mchezo huo ikiwa ni pamoja na kufunga.”

Kamwe alisema: “Tunafahamu kwamba katika kundi letu tuna pointi moja pekee tuliyoipata katika mechi tatu tulizocheza, huo ndio ukweli mchungu unaotukabili na ukweli huu hauishii hapo bali katika kundi letu tunashika nafasi ya mwisho.

“Hatukuanza vizuri michuano hii lakini miujiza tuliipata katika mchezo uliopita na kufufua matumaini yetu, hivyo nafasi hii hatutaichezea. Mechi hii ndiyo iliyoshikilia hatma yetu, hivyo lazima tuicheze kwa mkakati mzuri.”

Maandalizi yapoje?

“Timu imerudi mazoezini leo (jana), kuna program mbili, asubuhi gym na jioni uwanjani,” alisema Kamwe.

“Baadhi ya wachezaji wetu waliokuwa majeruhi na wametengemaa vizuri na wameanza mazoezi ya pamoja na timu. Djigui Diarra amerudi kwenye uwanja wa mazoezi, Maxi Nzengeli naye amerejea.

“Koussi Attohoula Yao afya yake na utimamu wake wa mwili ni nusu kwa nusu bado hajawa vizuri kufanya mazoezi ya jumla na timu ingawa anaweza kufanya ya peke yake.

“Clatous Chama aliyepata jeraha la mkono katika mchezo mwisho dhidi ya TP Mazembe, anaendelea vizuri, atakuwa sehemu ya wachezaji wanaofanya mazoezi, taarifa ya daktari inasema ana maumivu kidogo.

“Aziz Andabwile jeraha lake ni la muda mrefu, bado hajaanza mazoezi ya pamoja, Kennedy Musonda ameshapona, mchezo uliopita wa ligi alishiriki japo hakucheza lakini alikuwa benchi tayari kwa kucheza.”

Hata hivyo, kurejea kwa wachezaji hao hakutoi nafasi ya moja kwa moja kucheza mechi ijayo hasa Diarra kutokana na ripoti ya awali kuonyesha anatarajiwa kuwa nje wiki nne hadi sita kuanzia Desemba 16, 2024 hivyo matarajio ya kuanzia Januari 10 na kuendelea itategemea na uponaji wa majeraha ya kigimbi. TP Mazembe wanatarajiwa kuwasili nchini kesho Alhamisi majira ya saa 12 jioni.

Baada ya mchezo huo, Januari 12 Yanga itakuwa ugenini kukabiliana na Al Hilal kwenye Uwanja wa Cheikha Ould Boïdiya nchini Mauritania, kisha itarejea nyumbani kumalizana na MC Alger, Januari 18.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  LIGI YA MABINGWA ULAYA KINAWAKA USIKU WA LEO....