YANGA imeingia kambini jana kuendelea na maandalizi kabla ya kukutana na TP Mazembe, Jumamosi Januari 4, lakini tayari imepewa mwamuzi wa bahati atakayeamua mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Idara ya mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imewakabidhi waamuzi watatu kutoka Mauritius kusimamia sheria 17 kwenye mchezo huo wakiongozwa na Ahmad Imtehaz Heeralall atakayekuwa pale kati kwenye Uwanja wa Mkapa.
Heeralall atasaidiwa na mwamuzi wa kwanza msaidizi Ram Babajee, wapili akiwa Aswet Teeluck wote kutoka Mauritius huku wa nne akiwa Noris Aaron Arissol kutoka Seychelles.
Heeralall ana uzoefu na mashindano ya Afrika akichezesha mechi 14 za Ligi ya Mabingwa, lakini pia akisimamia mechi 13 za Kombe la Shirikisho.
Takwimu za mwamuzi Heeralall zinaonyesha amechezesha mechi 20 za CAF ngazi ya klabu ambapo kati ya hizo 15 timu zilizocheza zikiwa nyumbani zilishinda.
Ndani ya mechi 15 amewahi kusimamia mchezo wa Yanga ikiwa nyumbani dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho na wenyeji kupoteza kwa mabao 2-3 dhidi ya Wakenya, Julai 29, 2018.
Mwamuzi huyo pia alikuwa mezani wakati Yanga ikipoteza nyumbani kwa mabao 2-1 dhidi ya USM Alger ya Algeria kwenye fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho iliyopigwa Mei 28,2023 kabla ya kwenda kushinda ugenini kwa bao 1-0, lakini ikalikosa kombe hilo.
Yanga inatakiwa kuwa makini na Heeralall ambaye mpaka sasa ameshatoa kadi za njano 61 huku akiwa na mbili nyekundu zilizotokana na kadi za njano mbili.
TP Mazembe nao wana kumbukumbu naye nzuri ambapo amewahi kuhusika kwenye mechi zao mbili za mashindano mawili tofauti zote wakishinda walipocheza nyumbani dhidi ya RS Berkane, Aprili 23,2022, mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika kisha ile ya African Football League wakishinda tena dhidi ya ES Tunis zote kwa bao 1-0, lakini akiwa mwamuzi wa nne.