Home Habari za michezo PAMOJA NA KUANZA KUSHINDA….KOCHA YANGA AWAKATAA MASTAA WAKE….’BADO SANA’….

PAMOJA NA KUANZA KUSHINDA….KOCHA YANGA AWAKATAA MASTAA WAKE….’BADO SANA’….

Habari za Yanga leo

KOCHA Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amewavulia kofia wachezaji wake akisema kiwango walichoonesha kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate, kimeonekana kumshangaza hata yeye mwenyewe.

Ramovic, ambaye aliiongoza Yanga kuifumua Fountain Gate mabao 5-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa juzi katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, alisema wakati mwingine anaangalia wanavyocheza haamini kile anachokiona, kwani walionekana kuwa na kiwango bora zaidi kuliko alivyotegemea.

“Napenda kuwapa pongezi wenzangu wote, hasa watu wa eneo la utimamu wa mwili, wamefanya kazi kubwa hadi kufika leo hapa, si kazi rahisi kuifunga kila timu tunayokutana nayo kwenye ligi kwa idadi hii ya mabao, kwani nyingi zinakuja kupaki basi, zinacheza nyuma ya mpira na kujaribu kutushambulia kwa kushtukiza, ni ngumu, lakini wachezaji wangu wameweza kufanya kazi kubwa kiasi cha kunishangaza hata mimi, wakati mwingine siamini nini wanakifanya mle uwanjani, ni jambo la kujivunia sana,” alisema kocha huyo.

Kocha huyo bado anaamini kuwa wachezaji wake hawajafikia kiwango cha utimamu wa mwili ambacho yeye anahitaji wawe nao, lakini akaongeza hawapo mbali na hilo.

“Napenda mpira wa kasi, kushambulia muda wote wa mchezo, huwa inahitaji pumzi na fiziki, bado hatujakuwa fiti kwa asilimia 100, lakini tunakwenda kwenye njia sahihi tuliyoipanga,” alisema.

Alitahadharisha kuwa iwapo watafika kwenye kiwango anachohitaji anadhani kikosi kitakuwa ni hatari zaidi ya kilivyo sasa.

Kocha huyo ameiongoza Yanga kushinda michezo mitano mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akianzia dhidi ya Namungo FC, ikishinda mabao 2-0, mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa FC, 4-0 dhidi ya Prisons na Dodoma Jiji, kabla ya juzi kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Fountain Gate.

Imefikisha pointi 39, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Simba inayoongoza ligi ikiwa na pointi 40, huku zote zikiwa zimemaliza rasmi mechi zao15 za mzunguko wa kwanza.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohamed Muya, ambaye alitimuliwa kazi yeye na benchi lake lote la ufundi muda mfupi tu baada ya mchezo kumalizika, alisema ubora wa wachezaji ndiyo ulioamua mechi.

“Ugumu wa mechi ulikuja kutokana na ubora wa wachezaji, uwekezaji wa Yanga ni tofauti na timu yetu, makosa yaliyofanyika kwa wachezaji wangu ni kwa sababu hiyo tu ya uwekezaji wao mzuri umeamua mechi ya leo,” alisema Muya.

Kocha huyo akafichua kuwa kuna baadhi ya wachezaji ambao walikuwa kipaumbele kwenye usajili kabla ya kuanza kwa ligi, lakini hadi leo hii hawajacheza kwa kukosa vibali, wengine kukosa leseni za usajili.

Fountain Gate imebaki nafasi ya sita, ikisalia na pointi zake 20, ikicheza michezo 16, kushinda sita, sare mbili na kupoteza minane, mabao 24 ya kufunga, kufungwa mabao 32, ikiongoza kwa kuruhusu mabao mengi zaidi kwenye Ligi Kuu mpaka sasa.

SOMA NA HII  FT:- YANGA 4-0 CR BELOUIZDAD......PACOME DAY YAENDAA KIBABE....HISTORIA MPYA YAANDIKWA CAF..