Home Habari za michezo MASTAA SIMBA ‘WAJIVIKA MABOMU’ DK CHACHE KABLA YA KUKIPIGA NA WAARABU LEO…

MASTAA SIMBA ‘WAJIVIKA MABOMU’ DK CHACHE KABLA YA KUKIPIGA NA WAARABU LEO…

Habari za Simba leo

WACHEZAJI wa Simba wamesema watapambana na kujitoa katika kiwango cha juu ili kuhakikisha wanashinda mechi ya hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien itakayochezwa leo mapema kwa sababu msimu huu hawataki kusubiri hadi mchezo wa mwisho.

CS Sfaxien itawakaribisha Simba kwenye Uwanja wa Olympique Hammadi Agrebi ulioko jijini Tunis leo kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania.

Nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, alisema katika kikao cha wachezaji wamekubaliana safari hii wanataka kutinga hatua ya robo fainali mapema zaidi na hawataki kusubiri hadi mechi ya mwisho kuamua hatima yao.

“Tumeambizana hatutaki kusubiri hadi mechi za mwisho ndiyo ziamue hatima yetu kila msimu, safari hii tunataka tufuzu mapema, tunakata kushinda hii mechi ili zinazokuja iwe rahisi kwetu, tuwe tunacheza bila presha na mashabiki wetu. Huwa tunaona mechi za mwisho za maamuzi pale Uwanja wa Benjamin Mkapa zinavyokuwa na heka heka,” alisema Zimbwe Jr.

Kuhusu hali ya hewa ya baridi, beki huyo alisema haiwezi kuwaathiri kwa sababu wamekuwa ni wazoefu wa kucheza katika nchi mbalimbali kwenye hali kama hiyo.

“Hali ya hewa haiwezi kutuathiri kwa sababu tumeshacheza sana mechi katika hali kama hii nchi mbalimbali, wiki kadhaa tulitoka kucheza Algeria na Constantine, kulikuwa na hali ya hewa ya baridi kama hii, tena afadhali ya hii, ya huku kidogo imepoa tofauti na kule,” Zimbwe Jr alisema.

Naye kiungo mkongwe, Mzamiru Yassin, alisema kwa misimu kadhaa wamekuwa wakisubiria hadi mchezo wa mwisho ili kuamua hatima ya kucheza hatua ya robo fainali, lakini safari hii wanahitaji kuona wanakamilisha kibarua hicho mapema.

Mzamiru alisema ingawa wanajua mechi itakuwa ngumu lakini yeye hana wasiwasi wa hali ya hewa, wala ugeni kwa sababu wameshacheza kwenye uwanja huo mara kadhaa akiwa na kikosi cha timu ya taifa, (Taifa Stars).

“Kwangu mimi ni mzoefu, haitakuwa mara ya kwanza kucheza kwenye uwanja huu, hivyo ni mwenyeji, nimewahi kuwa hapa mara kadhaa nikiwa na kikosi cha timu ya taifa, hata hali ya hewa ya baridi hainisumbui, pamoja na hayo siku zote mechi ya ugenini zinakuwa ngumu, haijalishi mnacheza na nani, muhimu ni kuwa makini, yoyote atakayepata dakika za kucheza azitumikie ipasavyo,” alisema Mzamiru.

Wakati wachezaji wakisema hayo, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema wamefanya mazoezi mara tatu wakiwa huko na wanachomalizia ni mpango mkakati jinsi ya kuicheza mechi hiyo.

“Tunajaribu kuzoea hali ya hewa ya hapa, lakini kikubwa ni kutengeneza mpango mkakati wa mchezo wenyewe na jinsi ya kwenda kukabiliana na CS Sfaxien, kwa vile tulivyowaona na kuwasoma wanavyocheza,” alisema Fadlu.

Simba inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita sawa na CS Constantine na Bravo do Maquis ya Angola, huku CS Sfaxien ikiwa haina pointi yoyote mpaka sasa katika kundi lao.

SOMA NA HII  FEI TOTO AULA NDANI YA YANGA