Home Habari za michezo HIVI NDIVYO ‘UBAYA UBWELA’ ILIVYOIBEBA SIMBA KIMATAIFA…REKODI MPYA YAWEKWA🫡🫡…

HIVI NDIVYO ‘UBAYA UBWELA’ ILIVYOIBEBA SIMBA KIMATAIFA…REKODI MPYA YAWEKWA🫡🫡…

Meridianbet

IMEKUWA ni kama jambo la kawaida kwa mashabiki wa Simba kuiona timu yao ikifuzu robo fainali kwenye michuano inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya juzi kufanya hivyo kwa mara sita katika misimu saba kuanzia 2018-19.

Simba juzi ilikuwa Angola ikicheza mchezo wake wa tano wa makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos ambapo dakika 90 zilitamatika kwa sare ya bao 1-1 na kuipa tiketi timu hiyo kutinga robo fainali.

Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 10 na kujihakikishia kusonga mbele kabla ya mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya vinara CS Constantine (12).

Achana na matokeo hayo yaliyoifanya Simba itinge robo fainali ya sita katika kipindi cha misimu saba iliyopita, lakini hesabu zilizopigwa hadi kuvuka hatua hiyo ni hatari.

HESABU ZA KIUBAYA UBWELA

Unaweza kuichukulia poa Simba kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho lakini mnyama alipiga hesabu kali mapema tu.

Ukomavu wa Simba ulionyeshwa kwenye hatua hii baada ya kukusanya pointi tatu nyumbani dhidi ya Bravos ya Angola ikiitandika bao 1-0, kisha ikaenda ugenini na kupokea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya CS Constantine ya Algeria.

Baada ya kupoteza mchezo wa pili ikarudi Uwanja wa Benjamin Mkapa ikikusanya pointi tatu nyingine kwa CS Sfaxien ya Tunisia ikiichapa mabao 2-1 na kufikisha pointi sita kwenye kundi A.

Ikarudiana na Watunisia hao ugenini na Simba ikachukua pointi nyingine tatu baada ya ushindi wa bao 1-0 ikasogea nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa sawa na Constantine. Kisha juzi pointi moja katika sare ya 1-1 ugenini na Bravos, ikafikisha 10 zilizowavusha.

Ukiangalia hesabu zilivyopigwa kama huna D mbili huwezi kuelewa haraka kwani Mnyama alihakikisha mechi za nyumbani haangushi pointi yoyote zaidi ya kuchukua zote kila anaposhuka dimbani.

Kisha Simba ilitazama timu gani inaweza kupambana nayo ugenini na kuambulia pointi. Ilianza kwa Constantine mambo yakawa magumu licha ya kuanza kufunga bao lakini ikachapwa 2-1. Baada ya hapo, ikamkanda kibonde wa kundi Sfaxien ambayo imefungwa nje ndani na kuichangia Simba pointi sita.

Mtihani ukabaki kwa Bravos ambapo Simba hesabu zake zimeenda vizuri kwa kuhakikisha inaambulia pointi moja kwao, ikawa hivyo na jumla zikawa nne baada ya ushindi wa nyumbani, hivi sasa inapepea robo fainali.

ZILIZOFUZU

Simba iliyofuzu juzi inaungana na RS Berkane ya Morocco, Zamalek (Misri), CS Costantine (Algeria), Stellenbosch FC (Afrika Kusini) na USM Alger (Algeria). Bado timu mbili kukamilisha idadi ya timu nane zitakazocheza robo fainali ya michuano hiyo. Kundi C na D ndilo linasubiriwa kukamilisha idadi hiyo kwani vinara wao wameshafuzu, bado timu mojamoja ambapo itafahamika katika mechi za mwisho wikiendi hii.

Stellenbosch iliyopangwa kundi B, ilifuzu baada ya kuitandika Stade Malien mabao 2-0 na kufikisha pointi tisa ikiwa nyuma ya RS Berkane ambayo ilikuwa tayari imefuzu mapema kabla ya wikiendi iliyopita.

Constantine ambayo inaongoza kundi A ikiwa na pointi 12 ilitinga robo baada ya kuitandika CS Sfaxien, huku USM Alger ikipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Orapa United na kufuzu hatua inayofuata.

ROBO FAINALI YA SITA

Hii ni robo fainali ya sita Simba inakwenda kucheza katika kipindi cha misimu saba kuanzia 2018-19 kunako michuano ya CAF, lakini huwa haivuki zaidi ya hapo. Msimu huu nini kitatokea?

Baada ya kuishia hatua hiyo katika kila msimu ilioingia robo fainali, Simba imejiwekea malengo ya kufika fainali kama ilivyokuwa kwa Yanga msimu wa 2021-22, lakini pia ikiwezekana kubeba kombe lenyewe na kuweka rekodi mpya katika soka la Tanzania.

Uzoefu wa zaidi ya miaka saba ambao Simba imeupata kwenye michuano ya CAF, una maana kubwa kwao kuelekea malengo ya kuvuka hatua hiyo hadi fainali.

Kocha wa Simba raia wa Afrika Kusini, Fadlu Davids anaweka rekodi ya kuipeleka timu hiyo robo fainali ikiwa ugenini kwa mara ya kwanza kwani mara nyingine zote ilifuzu ikiwa nyumbani.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Simba, Zubeda Sakuru alisema hatimaye matarajio ya Simba kutinga hatua inayofuata yametimia akiamini timu hiyo inaweza kufika hatua kubwa zaidi.

“Najisikia faraja kama shabiki wa Simba na Mtendaji Mkuu, najua matarajio ya mashabiki ni kufanya vizuri katika mashindano ya kitaifa na kimataifa, kila Mtanzania alikuwa na matarajio ya ushindi au sare ili kutinga robo fainali,” alisema kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu alisema licha ya kufuzu robo fainali lakini bado Simba haijamaliza ikiahidi kulipiza kisasi cha kufungwa na Constantine.

“Haikuwa rahisi, tunashukuru hilo limeisha lakini bado haijaisha, tunataka kuongoza kundi kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Constantine, mechi hiyo ina mambo matatu kwanza kulipiza kisasi na la pili tunataka pointi zaidi na mwisho wachezaji wanataka kutoa shukrani zao,” alisema Mangungu.

Naye Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wameingia robo fainali kwa rekodi ya kipekee wakiwa ugenini.

“Tumeingia robo fainali kwa aina yake sana, kwanza tukiwa ugenini, mchezo haukuwa mwepesi, ni mpinzani ambaye kila timu ilikuwa inachapwa mabao matatu.”

SOMA NA HII  HUKUMU YA MKUDE KUFAHAMIKA LEO.. KAMANDA KOVA AFUNGUKA A-Z