Home Habari za michezo SIMBA, YANGA ZILIVYOANZISHWA UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA…WAARABU WATAJWA…

SIMBA, YANGA ZILIVYOANZISHWA UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA…WAARABU WATAJWA…

HABARI ZA SIMBA NA YANGA

Kesho, Jumanne ya Februari 11, 2025 Yanga watasherehekea miaka 90 ya kuanzishwa kwao.

Wenyewe wanasema klabu yao ilianzishwa tarehe kama hiyo mwaka 1935, kwa hiyo kesho itafikisha miaka 90.

Kwa umri huo, ni rasmi kwamba Yanga ni klabu kongwe zaidi ya mpira wa miguu katika Afrika Mashariki.

Siyo Kenya wala Uganda ambako kuna timu kongwe kiasi hicho.

Klabu kongwe zaidi kwa Kenya ni AFC Leopards iliyoanzishwa mwaka 1964 na Uganda ni Express iliyoanzishwa mwaka 1957.

Rwanda klabu kongwe zaidi ni Rayon Sports, iliyoanzishwa mwaka 1965.

Hakuna ubishi kwenye umri wa Yanga kwa sababu vyanzo vingi vinaonyesha kwamba kweli klabu hiyo ilianzishwa mwaka 1935.

Lakini hakuna chanzo hata kimoja kinachoitaja Februari 11 kama ndiyo tarehe rasmi ya kuanzishwa kwa klabu hiyo.

Maandiko mengi, likiwemo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lililoandikwa na Twalib Twalib na George K. Ambindwile kutoka idara ya historia ya chuo hicho linaloitwa Football Associations and Development of Football Leagues in Tanganyika, 1929-1960, yameeleza chimbuko la mpira hapa nchini na ligi zake, lakini siyo tarehe za kuanzishwa timu hii.

Matukio mengi yameandikwa kwa tarehe rasmi, kwa mfano tarehe ya kuanza kwa ligi ya Dar es Salaam, Juni Mosi 1929, tena kwa kulinukuu Gazeti la Tanganyika Times.

Mtendaji Mkuu wa Kwanza wa Chama cha Soka Dar es Salaam (DFA) A.B. Humphrey, alichapisha ratiba ya ligi kwenye gazeti hilo.

Lakini hakuna sehemu iliyoandikwa tarehe rasmi ya kuanza kwa klabu hii.

Ila wameandika kwamba Yanga haikuwa timu mpya huo mwaka 1935, bali ni timu iliyokuwa na asili ya Jangwani Sports Club, ambayo ni ya zamani zaidi.

Kwamba ligi ya kwanza ya mpira wa miguu hapa nchini ilianza Juni Mosi, 1929, ikiitwa LIGI YA DAR ES SALAAM.

Bahati mbaya sana ligi hii iliendeshwa kibaguzi, Waafrika (wazawa) hawakuruhusiwa kuwa na timu.

Kitu pekee walichoruhusiwa ni kushangilia timu zilizokuwepo ambazo zilikuwa za wageni tupu.

King’s African Rifles Club (K.A.R) Government School

Police

Railways

Gymkhana

Government Service.

Hata hivyo, Waafrika walitamani kuwe na timu yao pia kwenye hii ligi, ambayo iliitwa Jangwani Sports Club, iliyoanza 1926.

Hatimaye mwaka 1935 Waafrika wakaruhusiwa kuwa na timu yao.

Timu iliyoshiriki ni New Young SC ambayo ilitokana na Jangwani SC.

Hii New Young SC ndiyo inayotajwa kuwa ilianzishwa Februari 11, 1935.

Hakuna maelezo kama Jangwani SC ilikufa kwanza halafu ndiyo ikaanzishwa New Young SC, au ilibadili tu jina.

Na hakuna sehemu yoyote inayoitaja hii tarehe hii, Februari 11, kama ndiyo ya kuanzishwa klabu.

New Young SC ikashiriki ligi hiyo ikianzia daraja la pili kwa sababu ndiyo lilikuwa daraja la kuanzia wakati huo.

Ikashinda ubingwa wa daraja la pili na kupanda hadi daraja la kwanza 1936.

Lakini bahati mbaya ikashuka mwaka huohuo na kurudi daraja la pili.

Kushuka kwao kukasababisha mpasuko, baadhi ya wanachama wakajitenga na kuanzisha klabu yao.

Klabu hiyo ikaitwa Stanley SC kwa sababu ilianzia mtaa wa Stanley ambao kwa sasa ni Aggrey.

Stanley SC ikapitia majina kadhaa kama Queens SC na Knight Eagles.

Mwaka 1939, timu hii ikaungana na Arab Sports Club, timu ya Waarabu, na kuzaliwa timu mpya ya Sunderland SC ambayo mwaka 1972 ikabadili jina na kuwa Simba SC.

Agosti 8 ya kila mwaka, kuanzia 2009, klabu hii imekuwa ikisherehekea siku ya kuanzishwa kwake.

Kwamba ilianzishwa Agosti 8, 1936, hii si kweli hata kidogo.

Maandiko yote, likiwemo la aliyekuwa kiongozi wao Mwina Kaduguda ambaye aliandika kitabu cha historia ya Simba, hayataji tarehe rasmi.

Lakini hakuna shaka hata kidogo kwamba Simba haikuanzishwa Agosti 8, kwa sababu kuu moja.

Klabu hii ilianzishwa baada ya wanachama wa New Young SC kujitenga.

Na walijitenga baada ya timu yao kushuka daraja.

Ile ligi ambayo walishuka ilichezwa hadi Novemba, ndiyo ikaisha, iweje wao waanzishe timu Agosti?

Hizi tarehe za kuanzishwa kwa vilabu hivi bado zina utata.

Yawezekana kweli Yanga ikawa Februari 11, lakini haiwezekani hata kidogo Simba ikawa Agosti 8.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  MAAFISA CAF KUTEMBELEA UWANJA WA MKAPA KUONA KAMA 'YALIYOMO YAMO AU LAAH'..FAINAL ITAPIGWA...