Home Habari za michezo KARIAKOO DABI YALIZA WENGI….MAWAKALA FIFA WALIA HASARA YA MIL 20…MZIZE ATAJWA…

KARIAKOO DABI YALIZA WENGI….MAWAKALA FIFA WALIA HASARA YA MIL 20…MZIZE ATAJWA…

habari za SIMBA NA YANGA

KUSHINDWA kupigwa kwa pambano la Dabi ya Kariakoo Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam bado ni gumzo, huku wadau mbalimbali wakilia hasara walizopata kutokana na kuahirishwa kwa pambano hilo kulikofanywa na Bodi ya Ligi.

Bodi ya Ligi iliahirisha mchezo huo saa chache kabla ya kupigwa saa 1:15 usiku baada ya awali Simba kutoa taarifa ya kugomea mchezo huo kwa sababu ya kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho Kwa Mkapa kulikofanywa na wanaodaiwa makomandoo wa Yanga. Katika taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo huo, Bodi ya Ligi ilijikanganya kwani kanuni za kuahirishwa mchezo zimetajwa katika Kanuni za Ligi Namba 34 na hakuna hata moja iliyoainisha timu ikiwa imezuiwa kufanya mazoezi mchezo hautachezwa.

Hata hivyo, licha ya mamlaka ya soka kuchukulia poa uamuzi huo wa kuiahirisha mechi hiyo ya watani wa jadi, Simba na Yanga, lakini ukweli wadau mbalimbali wakiwamo mashabiki waliosafiri umbali mrefu kutoka mikoani na wengine kutoka nje ya nchi wamelia kupata hasara kubwa.

Pia wapo wafanyabiashara na wajasiriamali ambao huitumia mechi ya watani kupiga fedha kujikuta wakila hasara ambao hakuna wa kuwalipa, ilihali Yanga waliokuwa wenyeji wakijifungia tangu jana ili kufanya tathmini ya hasara iliyopata klabu katika maandalizi ya mchezo huo wa Ligi Kuu.

Yanga imedaiwa inaandaa barua hiyo huku wakisikilizia Bodi ya Ligi inayodaiwa ilikuwa ikijiandaa kukutana kwa ajili ya kupanga tarehe mpya ya mchezo huo, ambao tayari klabu huiyo imeshasema haitacheza na wamepanga kwenda kudai haki hiyo, Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kutokana na kuahirishwa kwa pambano hilo bila kuzingatia kanuni zilizopo.

Licha ya kwamba hakuna uthibitisho wa moja kwa moja juu ya hasara ya kifedha zilizojulikana kwa kuahirishwa kwa pambano hilo kuanzia Yanga yenyewe, Simba iliyougomea mchezo mapema kabla ya kuahirishwa kwake na hata mamlaka za kosa, lakini wadau wengine wamefunguka hasara walizopata, huku wakitoa lawama kwa kupuuzwa kwa mashabiki wa soka waliosafiri ili kuja kuishuhudia mechi.

MASKAUTI WA SWEDEN

Kabla ya pambano hilo kuahirishwa mapema kuliripotiwa juu ya ujio wa maskauti wawili kutoka Sweden waliotaka kulishuhudia pambano hilo ili kumsoma vyema Clement Mzize aliyechangia kuwaleta nchini. Hata hivyo, kushindwa kufanyika kwa pambano hilo, maskauti hao wameshindwa kujizuia na kueleza hasara walizopata na kushindwa kwao kumuona Mzize wanayempigia hesabu kumtafutia dili nje kutokana na kiwango alichonacho kwa sasa.

Maskauti hao Jamal Osman na Nahom Tesfaye, walioondoka nchini jana Jumatatu, walisema kuikosa dabi kumegharimu zaidi ya milioni 20 (dola 7,619), zilizotumika katika safari kutoka Sweden hadi Tanzania. Gharama hizo zinajumuisha chakula, usafiri na malazi.

Osman na Tesfaye walikuja Tanzania kwa matumaini makubwa ya kumtazama Mzize katika mechi ya presha dhidi ya Simba, lakini hali ilibadilika ghafla kufuatia vurugu ambazo zilitokea siku moja kabla ya mchezo huo, jambo ambalo liliwafanya Simba kususia mchezo huo.

“Tulijipanga kwa muda mrefu, tukaacha kazi nyingine ili tumuangalie Mzize kwenye mechi kubwa. Sasa tumeondoka bila kufanikisha lengo letu,” alisema Osman kwa masikitiko akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Tesfaye aliongeza: “Tumepoteza muda na pesa nyingi, lakini haya ni mambo ya mpira. Tunapaswa kusonga mbele.”

Licha ya kuondoka bila kumwona Mzize uwanjani, maskauti hao wamesema bado wataendelea kufuatilia maendeleo yake.

“Tutajaribu kumfuatilia kwa njia zingine, lakini nafasi hii ilikuwa bora zaidi kwetu,”€ alisema Osman.

Kuondoka kwa maskauti hao ni pigo kwa Mzize, ambaye alikuwa na fursa ya kujionyesha moja kwa moja kwa wadau wa soka la Ulaya. Sasa, itabidi asubiri nafasi nyingine kuthibitisha ubora wake mbele ya maskauti wa kimataifa.

VIBANDA UMIZA

Kuahirishwa kwa dabi hiyo hakujaleta hasara kwa maskauti wa Sweden tu, bali hata wamiliki wa vibanda umiza waliowekeza fedha nyingi kuandaa mazingira ya kutazama mechi hiyo maarufu.

Maelfu ya mashabiki walikuwa wamejitayarisha kwa pambano hilo kwa kutenga fedha za tiketi na wale ambao hawakupata nafasi ya kwenda uwanjani walikuwa wamepanga kufuatilia mechi hiyo kwenye vibanda umiza vilivyojaa kila kona ya jiji la Dar es Salaam na miji mingine mikubwa.

Hata hivyo, tangazo la ghafla la kuahirishwa kwa mchezo huo liliwashtua wamiliki wa vibanda hivyo, ambao wapo ambao walikuwa tayari wamekodi televisheni kubwa, kuongeza viti na hata kuagiza vinywaji na vyakula vya kutosha kuhudumia wateja wao.

Mmoja wa wamiliki wa vibanda umiza eneo la Kinyerezi, Juma Athumani, alisema alitumia zaidi ya 150,000 kuboresha eneo lake, lakini hakufanikiwa kurudisha hata robo ya gharama hizo baada ya mechi hiyo kutofanyika.

“Nilikodi ‘screen’ kubwa na kununua spika mpya ili mashabiki wa Yanga na Simba wafurahie mechi, lakini sasa kila kitu kimeharibika. Pesa zimepotea bure,” alisema, huku mmiliki mwingine wa kibanda umiza eneo la Mabibo, alisema alilipia king’amuzi za Azam sambamba na kununua vinywaji kwa ajili ya kuviuza wakati wa mechi hiyo, lakini kila kitui kimeenda sivyo na hajui wa kumpungizia machungu.

“Ni kweli hata kama mechi imeahirishwa, vinywaji na king’amuzi bado zitabaki, lakini haikuwa lengo langu kutumia fedha za ziada kwa maandalizi ya mchezo huo na unajua vipato vyetu watanzania ni vya kuungaunga, unatoa fedha kimahesabu ili kuvuna faida, lakini mambo yamenichachia. Inaumiza.”

WAJASIRIAMALI

Shabiki kindakindaki wa Yanga anayejulikana kwa jina la Jesca Manji, amesema kitendo cha dabi ya Yanga na Simba kuahirishwa Machi 8 kimemuingiza katika madeni yaliyotaka kusababisha ajidhuru.

Jesca anayejishughulisha na biashara ya kuuza vyakula (mama lishe) alisema alikwenda kuchukua kuku kwa mtu kwa mali kauli, alitegemea baada ya dabi anakwenda kupeleka pesa za watu, lakini mambo yakaenda sivyo. “Nilichukua kuku wa Sh2 milioni na nilifanya maandalizi ya biashara kila kitu kikawa tayari, ajabu bodi ya Ligi Kuu Tanzania ikatoa taarifa saa 8:00 mchana hakuna mechi, nikajikuta naishiwa nguvu, nashindwa cha kufanya, kwa sababu mwenye kuku anataka pesa zake siyo maneno,” alisema Jesca na kuongeza;

“Nakajikuta natamani kunywa dawa ili nife, lakini kitu kilichonipa nguvu ni mama ninayelea watoto wangu mwenyewe, nikawaza nikiondoka duniani wataishi vipi, nikapata nguvu ya kuendelea kupambana kuona ni namna gani nitalipa deni la watu.”

Alisema kwa biashara ya aina yake kama hana friji la kuhifadhia kuku wanaharibika na ndicho kilichotokea kwa watu wengi Machi 8, ambao wakajikuta wanatupa vyakula. “TFF na Bodi ya Ligi wangefikiria kwa mapana katika uamuzi wao, wanajua kuna wafanye biashara wanawake ambao wanapambania maisha yao, acha ninyamaze maana nina hasira nashindwa cha kufanya,” alisema Jesca.

Wachuuzi wengine kando ya Uwanja wa Mkapa, walisema walitegemea kutengeneza pesa ya ziada kupitia dabi kama inavyokuwepo siku zote kukiwa na mechi kubwa, lakini wamejikuta wakipata hasara ya vyakula bila kujua wa kuwalipa gharama hizo.

“Inauma sana watu wachache wanafanya mambo kwa utashi wao, bila kujali hasara inayopatikana kwa waliopo nyuma ya mchezo mkubwa kama huo, ni kuwakosea heshima mashabiki na mpira wa miguu kwa ujumla, kwani nasikia hakuna kanuni za kuahirisha zilizotumika, ila maamuzi ya kulindana tu, hii sio sawa na inarudisha nyuma uchumi wa mtu mmoja mmoja na hata taifa kwa ujumla,” alisema Hellen Muro mama ntilie.

WA MIKOANI NAO

Getruda Emmanuel kutoka Mafinga, alisema Dabi hii imejua kuwakomesha kwani walisafiri kutoka Mafinga hadi Dar es Salaam kwa usafiri wa gari mbili aina ya coaster ambazo walikodi wakiwa mashabiki jumla 60 na kila mmoja alilipa nauli kiasi cha shilini 60,000 ya kwenda na kurudi.

Mbali na nauli, Getruda amebainisha kuwa alilipia sehemu ya kulala kwa siku mbili huku kila siku ikiwa ni shilingi 20,000.

“Sisi tumechangishana kila mmoja ametoa shilingi 60,000 ya nauli kwenda na kurudi, tulikodi gari mbili ambapo tulikuwa mashabiki 60. Ukiangalia gharama za kukodi gari zote hizo nauli jumla shilingi milioni tatu na laki sita,” alisema Getrude.

Getrude alisema kwa upande wake jumla alitumia zaidi ya Shilingi 150,000 ikiwemo usafiri, kula, kulala pamoja na kununua jezi.

“Achana na gharama hizo, pia mimi ni mfanyabiashara, nimelazimika kufunga biashara yangu kwa siku mbili kwa ajili ya kuja kuiangalia mechi hii, hivyo sijaingiza kitu na nilichokifuata nimekikosa,” alisema Getrude na kuongeza.

“Kutokana na haya yanayoendelea, sidhani kama wakati mwingine mashabiki kutoka mikoani tutakuja kuangalia mechi hizi za dabi au mechi yoyote kubwa, kwani imekuwa haina uhakika kama inachezwa kwani unaweza kujiandaa ukifika hamna mechi.”

YANGA SASA

Ulipotafutwa uongozi wa Yanga kutaka kujua hasara iliyopata klabu hiyo iliyokuwa wenyeji, lakini simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa, ila chanzo cha ndani kutoka klabuni alilidokeza Mwanaspoti kuwa, viongozi walikuwa wakijadiliana na kufanya tathmini ya jambo hilo.

“Huwezi kuwapata kwa sasa, kwani wanajadiliana na kufanya tathmini ya pamoja ya kujua hasara nzima ili kuwekwa kwenye barua ya kisheria itakayotumwa CAS, ili kudai pointi tatu za mchezo huo wa Machi 8 kama ilivyoainishwa kwenye taarifa kwa umma,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Kuna gharama kubwa zilizopatikana kuanzia maandalizi ya kambi, matangazo na mambo mengine, hivyo sio rahisi kufahamika, ndio maana wanakutana kwa sasa kuweka sawa kisha watatoa taarifa, ila ukweli ni kwamba Yanga imepata hasara za mamilioni ya fedha kwa sababu ya ubinafsi wa wachache.”

Mapema Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alikaririwa kwamba kabla ya mechi kuahirishwa tayari tiketi zaidi ya 40,000 zilizokuwa zimeuzwa kwa mashabiki, ambao hata hivyo hawakupata nafasi ya kulishuhudia pambano hilo kutokana na kuahirishwa na Bodi ya Ligi baada ya tishio la Simba kugoma.

Maofisa wa Simba na wale wa Bodi ya Ligi walipotafutwa ili kupata ufafanuzi wa hasara ambazo walipata katika maandalizi ya mchezo huo kabla ya kuahirishwa muda mchache hazikuzaa matunda kwani simu zilikuwa zikiitwa bila kupokelewa.

Bodi ya Ligi ndio wasimamizi wakuu wa mchezo huo, wakibeba gharama za kuwahudumia maofisa wa mchezo huo wakiwamo waamuzi, kamisaa na wengine iwe ni kutoka Dar es Salaam au mikoani. Hii ni mara ya 13 kwa Simba na Yanga kukachana kwa sababu mbalimbali katika mechi za Ligi ya Bara tangu ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 1965, huku rekodi zikionyesha Simba inaongoza kwa kufanya hivyo mara saba dhidi ya sita za watani wao na kwa miaka karibuni hii ni mara ya pili kwa dabi kuahirishwa ndani ya muda mfupi ikiwamo lile la Mei 8 mwaka 2021 na Yanga iligoma kucheza. Mechi hiyo ya Mei 8, ilipangiwa kuchezwa upya Julai 3, mwaka huo na Yanga kushinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Zawadi Mauya, huku mchezo ulioahirishwa wikiendi bado haujapangiwa muda na tayari Yanga imesisitiza haitaucheza kwani ilishamaliza kazi Machi 8.

Credit:- MwanaSpoti.

SOMA NA HII  MASTAA SIMBA 'WAJIVIKA MABOMU' DK CHACHE KABLA YA KUKIPIGA NA WAARABU LEO...