Home Habari za michezo KISA SAFARI YA MO DEWJI ULAYA ….AHMED ALLY AWATUPIA DONGO LA GIZANI...

KISA SAFARI YA MO DEWJI ULAYA ….AHMED ALLY AWATUPIA DONGO LA GIZANI YANGA….

Habari za Simba leo

MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameonekana kuwatupia kijembe watani wao wa jadi, Yanga, kufuatia ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji (Mo Dewji), nchini Ujerumani.

Katika ziara hiyo, Mo Dewji alikutana na viongozi wa klabu ya VfB Stuttgart, inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Simba.

Kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Ahmed Ally aliweka wazi kuwa ziara za Mo Dewji zinakusudia kuifanya Simba kuwa “Global Brand”, yaani klabu inayotambulika kimataifa.

“Maono ya Simba na Mo Dewji ni kutengeneza taasisi ya mpira yenye maendeleo kwenye soka la vijana, soka la wanawake na ustawi bora wa kimaslahi kwa wachezaji wa timu zetu. Ndiyo maana Rais wetu yupo ‘busy’ kutafuta wabia wa kushirikiana nasi ili kutimiza malengo hayo. Muda si mrefu tutatoka kwenye soka la kimazoea na kupiga hatua kubwa za maendeleo yanayotambulika duniani kote,” aliandika Ahmed Ally.

Hivi karibuni, Mo Dewji amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Simba inapiga hatua kimataifa. Mazungumzo yake na VfB Stuttgart yanalenga kuinua timu za vijana, kufungua fursa kwa chipukizi wa Kitanzania, na kuimarisha nafasi ya Simba kwenye ramani ya kimataifa.

Kwa upande wake, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Mo Dewji aliweka bayana dhamira yake ya kuiendeleza Simba kwa viwango vya kimataifa.

“Tunawaza kimataifa lakini tunatamba ndani ya nchi, kuhakikisha kuwa ukuaji wa klabu yetu unawanufaisha wachezaji wa Kitanzania kwa kuinua hadhi ya soka letu. Lakini mafanikio hayaji kwa ushindi pekee, yanakuja kwa kuheshimu mchezo, kuwa na nidhamu, na kushindana kwa haki.

Soka duniani linaheshimiwa kwa sababu ya misingi hii, nasi lazima tushikamane na viwango vya juu vya kimataifa, sio tu uwanjani bali hata nje ya uwanja. Simba inaendelea kupiga hatua mbele tukizingatia maadili, uadilifu, na maono makubwa kwa soka la Tanzania,” aliandika Mo Dewji.

Kauli za viongozi hawa wa Simba zinaashiria dhamira yao ya kuifanya klabu hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa huku wakijinasibu kupiga hatua zaidi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga.

SOMA NA HII  KUTOKA KUWA MKIMBIZI MPAKA KUSAJILIWA SIMBA SC....HAYA NDIO MAPITIO HALISI YA KIBU DENIS...