NYOTA wawili wa Simba SC, kipa Moussa Camara na beki Che Malone Fondoh, wanatarajiwa kurejea uwanjani kwa mchezo muhimu wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri.
Wawili hao wamekosekana kwenye michezo miwili ya Simba kutokana na majeraha lakini wanaendelea na matibabu na wanatarajiwa kuwa fiti kwa ajili ya pambano hilo la hatua ya mtoano.
Kwa mujibu wa Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, wachezaji hao wamepata takribani wiki mbili za matibabu tangu walipoumia katika mechi dhidi ya Azam FC.
“Wamepata muda wa kutosha kwa ajili ya matibabu, na sasa afya zao zinaimarika. Baada ya mchezo wa leo dhidi ya Dodoma Jiji FC, hatutakuwa na mchezo mwingine, hivyo watapata muda zaidi wa kupona na kujiandaa kwa Al Masry,” amesema Ahmed Ally.
Simba SC, wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye mashindano hayo, wataanza robo fainali ugenini dhidi ya Al Masry mnamo Aprili 2, kabla ya kurudiana nyumbani Aprili 9.