Home Michezo ISHU YA SIMBA KUGOMEA DABI INAVYOWEZA KUIPA UBINGWA YANGA KILAINI…

ISHU YA SIMBA KUGOMEA DABI INAVYOWEZA KUIPA UBINGWA YANGA KILAINI…

habari za SIMBA NA YANGA

NDO hivyo bwana! Kitendo cha Simba ‘kugomea’ mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga kabla ya Bodi ya Ligi kubariki kwa kuahirisha bila kuzingatia kanuni za Ligi Kuu, kinaifanya timu hiyo ya Msimbazi kujiweka pabaya dhidi ya jinamizi la kutotwaa ubingwa.

Mashabiki wa soka kwa sasa wanasikilizia kujua nini itakuwa hatima ya sakata hilo ambalo limewaibua wadau mbalimbali kulaani kutokana namna lilivyohitimisha mchezo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu Jumamosi iliyopita, Machi 8.

Lakini, huku nyuma rekodi zinaonyesha katika michezo yote ambayo Simba iligomea kucheza na Yanga tangu miamba hiyo ilipoanza kukutana mwaka 1965, haijawahi kubeba ubingwa wa Ligi ya Bara, jambo linalosubiriwa kuona kama itatokea tena kwa msimu huu pia au la.

Kwa mara ya kwanza Simba kugoma kucheza na Yanga ilikuwa Machi 3, 1969, ambapo kikosi hicho cha Msimbazi kiligoma kabisa kupeleka timu uwanjani, kutokana na kilichoelezwa kutokubaliana na maelekezo ya Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa TFF).

Mwaka huo, Yanga ilikuwa ya moto kiasi cha kuitisha Simba kwani iliwakilisha nchi katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) baada ya kubeba ubingwa 1968 na kutolewa robo fainali na Asante Kotoko ya Ghana kwa penalti.

Yanga ilizitoa timu za Fitarikandro ya Madagascar kwa jumla ya mabao 4-3, kisha St George ya Ethiopia kwa mabao 5-0 na robo dhidi ya Asante ilitoka sare ya bao 1-1 nyumbani na ugenini na kupigwa penalti zilizowatupa nje kwa kuchapwa 4-3.

Kitendo cha Simba kuugomea mchezo huo, Yanga ikapewa ushindi wa pointi mbili na mabao mawili na kutangazwa rasmi mabingwa.

Juni 18, 1972, Simba iligoma tena kuingia uwanjani kipindi cha pili cha pambano hilo la marudiano la Ligi ya Taifa (sasa Ligi Kuu Bara) kupambana na watani zao Yanga iliyokuwa inaongoza pia bao 1-0, lililowekwa kimiani na Leonard Chitete.

Kitendo cha Simba kugomea kukaipa Yanga ushindi wa bure na kutwaa ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu, baada ya mchezo wa kwanza kuisha kwa sare ya 1-1, bao la Yanga likifungwa na Kitwana Manara, huku la Simba likifungwa na Willy Mwaijibe.

Simba ikagomea tena pambano la marudiano la Agosti 10, 1985, la Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu), baada ya miamba hiyo kufungana 1-1, la Yanga likifungwa na Omar Hussein ‘Keegan’ dakika ya 6, huku la Simba likifungwa na Mohammed ‘Bob’ Chopa, dakika ya 30.

Katika mechi hiyo ya marudiano, Yanga ilipewa ushindi wa bure, mabao mawili na pointi mbili kutokana na Simba kuvunja pambano hilo ikigomea penalti iliyotolewa kwa Yanga, baada ya beki wa kati, Twalib Hilal kuunawa mpira eneo la hatari.

Penalti hiyo ilipatikana dakika ya 84 na kutolewa na mwamuzi Bakar Bendera wa Tanga ambapo kitendo hicho cha kikosi cha Msimbazi kugomea mchezo huo ulivunjika na Yanga kupewa ushindi wa bure na kuchukua tena ubingwa wa Ligi Kuu mwaka huo.

Mwaka 1985 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Muungano, Simba iligoma kurudi uwanjani kipindi cha pili kwa ilichodai, Mwamuzi Hafidh Ali, aliwatisha wachezaji wa kikosi hicho ni lazima wafungwe na ndipo walipojivunja baada ya kuisha kipindi cha kwanza.

Kitendo hicho cha Simba kugoma, kiliifanya Yanga kupewa tena ushindi wa mezani, ingawa mwaka huo ubingwa ulichukuliwa na Majimaji.

Februari 25, 1996, Simba iligoma tena kupeleka timu uwanjani baada ya Chama cha Soka Tanzania (FAT, kwa sasa TFF) kugoma kuahirisha mchezo huo kama ilivyoombwa na klabu hiyo ikitaka kupata muda wa kujiandaa vyema kwa mechi yake ya kimataifa.

Mwaka huo, Simba ilikuwa inajiandaa na Kombe la Washindi ambalo halipo baada ya kuunganishwa kutoka Kombe la CAF hadi (Kombe la Shirikisho Afrika) dhidi ya Chapungu Rangers FC ya Zimbabwe na ndipo Yanga ikajikuta iko yenyewe tu uwanjani.

Kitendo hicho kikaipa Yanga ushindi wa mabao 2-0, huku mechi ya Simba na Chapungu Rangers ikashindwa kufanyika na ndipo Wekundu hao wa Msimbazi wakapewa ushindi wa mezani na kusonga mbele, licha ya mechi ya kwanza ugenini kuchapwa bao 1-0.

Simba ilipewa ushindi huo kutokana na Chapungu kushindwa kuja nchini na katika raundi iliyofuatia ikatupwa nje na El Mokawloon ya Misri kwa kanuni ya bao la ugenini, baada ya kushinda nyumbani 3-1 na kuchapwa ugenini 2-0, hivyo jumla kuwa 3-3.

Katika vipindi hivyo ambavyo Simba iligomea pambano la Dabi, rekodi zinaonyesha kuibeba zaidi Yanga tofauti na kikosi hicho cha Msimbazi, hivyo tukio la Machi 8, mwaka huu linasubiria kuona kama jinamizi litaendelea kuiandama.

Rekodi za mechi 12 za Kariakoo Dabi miaka ya nyuma ambazo Simba na Yanga kila moja ikigomea sita za michuano tofauti ikiwamo Ligi ya Bara, Kombe la Kagame na Ligi Kuu ya Muungano, Simba mara zote haijabeba ubingwa msimu husika wakati Yanga ikibeba mara tatu ambazo ni 1992, 2002 na 2021 kwenye Ligi ya Bara, wakati mara tatu ilipogoma na kukosa ubingwa ilikuwa 1965, 1966 kwenye ligi na 2008 Kombe la Kagame.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMAPILI