ACHANA na kile kinachoendelea Msimbazi kwa sasa juu ya Simba kugomea mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga uliotakiwa kupigwa Jumamosi, Machi 8, mwaka huu, kando ya hilo kuna mambo mengi yanayoendelea, lakini za ndaani ni kwamba mabosi Msimbazi wanaendelea kujipanga na msimu ujao.
Unaambiwa kwamba katika kipindi hiki ambacho ulimwengu wa wapenzi wa soka umepigwa na butwaa na kitendo cha kususia kwao mchezo dhidi ya mtani wao, Yanga, lakini hesabu zao ziko katika kujiimarisha zaidi ili kukabiliana na ushindani kwa ajili ya mashindano ya ndani na kimataifa.
Na wakati ikibaki miezi miwili na wiki mbili kabla ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 kufikia tamati, tayari mambo yameanza kuchangamka katika viunga vya Wanamsimbazi, Simba SC kufuatia kuihitaji huduma ya kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Simba ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 54 kufuatia kucheza mechi 21, inamuhitaji Fei Toto ambaye mkataba wake na Azam unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao 2025-2026.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, katika ripoti yake ya awali kabla ya kumalizika kwa msimu huu, amewataka mabosi wa klabu hiyo kumsajili Fei Toto kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini kwake aende kushirikiana na kiungo kutoka Ivory Coast, Jean Charles Ahoua.
Fei Toto ambaye anaichezea Azam FC ambapo alisaini mkataba wa miaka mitatu kuanzia msimu wa 2023-2024 akitokea Yanga, huu ni msimu wake wa pili akiwatumikia matajiri hao wa Dar es Salaam, akiwa ndie mchezaji mzawa mwenye rekodi kubwa katika ligi kwa sasa.
Kiungo huyo aliyewahi kuichezea Yanga kuanzia 2018 hadi 2023, msimu huu amefunga mabao manne na asisti 12 kwenye ligi, akiwa ni panga pangua katika kikosi cha Azam tangu alipotua.
RIPOTI YA KOCHA
Taarifa zinasema kwamba, viongozi wa Simba wamepokea ripoti kutoka kwa Fadlu huku ikija na taarifa ya maeneo ambayo yanavuja, ikiwemo eneo la kiungo mshambuliaji akihitaji nguvu kuongezwa.
Ripoti ya Fadlu ilisema kuwa, licha ya kuwa viungo wake wanafanya kazi nzuri kwa kushirikiana na washambuliaji katika kufunga mabao wakati timu hiyo ikiwa nayo 46 kwenye ligi, lakini bado anahitaji nguvu zaidi iongezwe ili Jean Charles Ahoua apate msaidizi.
“Fadlu amewaambia mabosi wa Simba kwamba kama kuna uwezekano anataka kumuona Feisal Salum kwenye kikosi chake msimu ujao kwani ni miongoni mwa viungo wanaomvutia sana.
“Anasema anataka kuwa na kiungo mwenye muendelezo wa ufanisi wake, atakayekuja kusaidiana na Ahoua ambaye ameonyesha kitu kikubwa msimu huu, lakini anahitaji usaidizi zaidi,” kimesema chanzo.
OFA ZA FEI
Ikumbukwe kuwa, kuliripotiwa ofa alizokuwa nazo Feisal Salum, huku ikiwekwa wazi kuwa miongoni mwa klabu iliyopania kumchukua msimu ujao ni Kaizer Cheif ya Afrika Kusini inayofundishwa na kocha wa zamani wa kiungo huyo, Nasreddine Nabi.
Habari kutoka Afrika Kusini zimefichua kwamba, kaizer Chiefs ipo tayari kutoa randi milioni tisa (Sh1.2 bilioni za Kitanzania) kwa ajili ya kuipata saini ya Fei Toto.
“Kaizer inajipanga kutoa dau ambalo Azam inalitaka, baada ya kufeli dirisha dogo kwa kutofikia kiwango wanachokitaka mabosi hao wa Chamazi ambacho sio chini ya bilioni moja,” zimedai habari hizo.
“Kwa sasa kuna mazungumzo yameanza kufanyika baina yao ambapo Kazier imefikia kiasi cha kukubali kutoa randi 9,000,000,” taarifa kutoka Afrika Kusini zimeripoti.”
KUHUSU SIMBA
Hii sio mara ya kwanza kwa Simba, hapo awali kiwango cha kiungo huyo kiliwatoa mate mabosi wa klabu hiyo na kuanza hesabu za kutaka kuwa naye msimu ujao, ndipo ikaamua kugonga hodi kwa Azam kuona kama wataweza kufanya biashara, lakini dau walilotajiwa ambalo si chini ya bilioni moja ili kununua mkataba wake lilionekana kuwa zito kidogo, mazungumzo yakasitishwa.
Kusitishwa huko kwa mazungumzo, kuliwapa Simba nafasi ya kujitafakari ni namna gani watampata Fei Toto kwa namna nyingine, ndipo waliopoamua kumvaa mchezaji mwenyewe ikimshawishi kuununua mkataba wake, kama ilivyokuwa kwa Yanga wakati anaondoka, ombi ambalo halikukubaliwa na uongozi wa mchezaji huyo, huku wakiweka wazi kuwa, historia mbaya iliyowahi kutokea akiwa Yanga hawataki ijirudie. Uamuzi wa mwisho ukaelezwa kwamba nyota huyo anataka kwenda kucheza nje ya nchi.
FEI MWENYEWE
Kupitia gazeti la Mwanaspoti, Fei Toto aliwahi kusema kuwa, amecheza ligi ya Bongo kwa muda mrefu na anaifahamu vizuri, hivyo anatamani kupata changamoto mpya nje ya nchi.
“Sasa nipo Azam nina amani kubwa, lakini pia nimecheza Yanga na kupata mafanikio makubwa, kwa hiyo kitu kilichosalia kwangu ni kwenda kucheza nje,” aliwahi kusema mchezaji huyo.
“Natamani nije kuongeza kitu kwenye timu ya Taifa, naamini pia Azam haitanizuia kama timu zitakuja kwa nia ya kunitaka, hivyo ninachokitamani zaidi ni changamoto mpya.”
AZAM WANASEMAJE?
Ofisa Habari wa Azam FC, Hasheem Ibwe, amenukuliwa akisema kwamba, bado wana uhitaji na mchezaji huyo ambaye amebakiwa na miezi 17 katika mkataba wake, hivyo wanapambana kumuongezea aendelee kusalia kikosini hapo kwa muda mwingine zaidi.
“Kama kuna mchezaji tunahitaji abaki, basi ni huyu kijana Feisal,” alisema Ibwe na kuongeza:
“Hatujafungua mazungumzo rasmi na klabu yoyote kwa sababu hauzwi. Feisal Salum ana miezi 17 katika mkataba wake na Azam, haendi popote, tutahakikisha anabaki kwani ni mchezaji muhimu.”
Credit:- MwanaSpoti